Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mikakati ya Polisi kupunguza ajali iwe endelevu

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, limetangaza mikakati ya kupunguza ajali za barabarani nchini, hususan kuelekea msimu wa mwisho wa mwaka.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuongeza kamera za tochi, kusimamia ratiba za mabasi, kukagua vyombo vya moto, kuongeza askari barabarani na kuhakikisha madereva wa mabasi wanaendesha kwa kupokezana.

Wakati Jeshi la Polisi likitangaza mikakati hiyo, juzi Rais Samia Suluhu Hassan alipotoa salamu za pole kwa familia, ndugu kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, kutokana na ajali iliyohusisha magari matatu wilayani Karagwe na kusababisha vifo vya watu saba na majeruhi tisa, aliliagiza jeshi hilo kuhakikisha madereva wanaongeza umakini na kuzingatia sheria za barabarani, hasa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.

Rais Samia alisema utekelezaji wa agizo hilo unatakiwa uende sambamba na uhuishaji na uwekaji wa alama za barabarani kwenye maeneo hatarishi, pamoja na kuzingatia umbali na maeneo sahihi ya uwekaji wa vituo vya ukaguzi ili vionekane kwa urahisi zaidi.

Pamoja na mikakati ya Jeshi la Polisi, agizo la Rais Samia linapaswa kuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa katika usimamizi wa usalama barabarani.

Inafahamika ajali za barabarani zimekuwa janga kubwa nchini, zikiathiri uchumi na kupoteza nguvukazi ya Taifa. Chanzo kikubwa, kama ilivyoelezwa na Kamanda wa wa kitengo cha usalama barabarani, Ramadhani Ng’anzi, ni mwendokasi na uzembe wa madereva.

Tunaamini hatua za kuziba mianya hiyo ni muhimu, hivyo ni wajibu wa kila mdau kuunga mkono. Kutumia kamera za tochi na askari wa kificho, pia ni mbinu inayoweza kuchochea nidhamu kwa madereva. Hata hivyo, utekelezaji wake unapaswa kufuata misingi ya haki na uwazi, ili kuepuka malalamiko ya ukiukwaji wa haki za msingi za watumiaji wa barabara. Pia tunaona suala la kuwapo kwa usimamizi wa ratiba za mabasi na kuwepo kwa madereva wawili kwa safari ndefu ni hatua nzuri itakayosaidia kupunguza uchovu wa madereva.

Pamoja na hayo, ni vema mkakati wa kuhakikisha magari yanakaguliwa kikamilifu kabla ya safari, unatiliwa mkazo zaidi. Magari mabovu au yenye hitilafu nyingine hayatakiwi kuruhusiwa kuendelea na safari.

Katika muktadha huo, ni muhimu mamlaka husika ihakikishe kuna vifaa vya kutosha vya kukagulia magari pamoja na mafunzo kwa askari wa barabarani.

Ulevi ni moja ya sababu kuu za ajali, na ukaguzi wa mara kwa mara, unaweza kupunguza tatizo hili, hivyo ni muhimu matumizi ya vipima ulevi kwa madereva vitumike kwa uwiano wa haki kwa madereva wote bila ubaguzi. Mikakati iliyotangazwa na Jeshi la Polisi ni mizuri na itakuwa na tija zaidi iwapo itasimamiwa kikamilifu.

Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwapo kwa changamoto katika utekelezaji endelevu wa mikakati, kwani historia inaonyesha mipango mingi mizuri imekuwa ikitelekezwa muda mfupi kutokana na ukosefu wa rasilimali, ufuatiliaji duni au ushirikiano hafifu kutoka kwa wadau.

Jeshi la Polisi linapaswa kuhakikisha usimamizi wa mikakati hiyo unakuwa endelevu, huku wananchi wakielimishwa kuhusu umuhimu wa kufuata sheria za barabarani.

Tunasema hivyo kuwa kuwa inafahamika kuwa si kwamba kipindi cha mwisho wa mwaka pekee ndiko hutokea matukio ya ajali, bali katika kipindi chote cha mwaka, hivyo tunasisitiza umuhimu wa kuwapo kwa utekelezaji endelevu ili kupunguza janga hilo nchini.