Mbinu hizi zinaweza kusaidia kuboresha elimu yetu
Muktasari:
Mojawapo ni kuona yale mazuri yaliyofanyika ya kuzishirikisha idara mbalimbali za elimu, kwa lengo la kuwafanya wanafunzi wawe wadadisi na wabunifu ili waweze kujitegemea wakiwa wakubwa.
Viongozi wapya wa Serikali wanapoteuliwa hawana budi kuchunguza juhudi mbalimbali zilifanyika siku za nyuma za kuimarisha elimu yetu.
Mojawapo ni kuona yale mazuri yaliyofanyika ya kuzishirikisha idara mbalimbali za elimu, kwa lengo la kuwafanya wanafunzi wawe wadadisi na wabunifu ili waweze kujitegemea wakiwa wakubwa.
Utaratibu wa ushirikiano baina ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), Idara ya Mafunzo ya Ualimu na Idara ya Ukaguzi wa Elimu wizarani ni mfano mmojawapo.
Zamani, idara hizi tatu (utatu katika elimu) zilishirikiana katika utafiti kwa lengo la kutoa elimu bora. Mfano mzuri ni katika somo la mwandiko.
Hatua ya kwanza ni kuumba herufi mchangani. Kwa kutumia vidole vyao, wanafunzi walijifunza kuumba herufi na pia kuandika tarakimu. Hatua ya pili ni kuumba herufi na tarakimu kwa kutumia vibao na kalamu za mawe. Vibao vilimsaidia mwanafunzi kurudia umbo la neno au kuandika tarakimu na kufuta mara kwa mara pale ambapo amekosea.
Hatua inayofuata ni kutumia karatasi, penseli na kifutio. Mafunzo ya aina hii huanzia kwa watoto wa chekechea na darasa la kwanza. Wanapofika darasa la pili, wameshakomaa na hivyo kuanza kutumia kalamu za wino zenye nibu.
Kalamu za kisasa za ‘bic’ hazikupendekezwa kutumika kwani ziliharibu mwandiko. Ndiyo maana wanafunzi wa shule za msingi hawakuruhusiwa kuandika kwa kutumia ‘bic’ bali kalamu zenye nibu.
Wakaguzi wa shule walikuwa na nafasi nzuri ya kushadidia mwandiko mzuri walipokagua. Kwa hiyo wakaguzi wa shule walisaidia ubora wa elimu katika taaluma, mwandiko, nidhamu, usafi wa wanafunzi, walimu na mazingira ya shule kwa jumla.
Eneo jingine lililosaidia kuimarisha elimu ni kuwa na mwendelezo wa kitaaluma kwa elimu ya msingi na sekondari. Ni dhahiri kuwa mfumo wa ufundishaji wa elimu ya msingi darasa la kwanza hadi la saba ni kwa kutumia Kiswahili. Wanafunzi wanapoingia kidato cha kwanza wanakumbana na hali tofauti kwani wanaanza kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia.
Hali hii inaleta mkanganyiko mkubwa kwa wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza na kuwafanya washindwe kuelewa masomo wanayofundishwa kwa kuwa na kiwango duni cha uelewa wa lugha ya Kiingereza.
Ili kuwasaidia wanafunzi hawa, Serikali katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 1992 hadi 1966 walianzisha mpango uliojulikana kama ‘English Language Teaching Support Project’ (ELTSP) chini ya Ofisi ya Kamishna wa Elimu. Mpango huu ulifadhiliwa na Wakala wa Maendeleo wa Uingereza (‘Overseas Development Agency’ - ODA) kwa ajili ya nchi Jumuiya ya Madola.
Wataalamu walioendesha mafunzo haya waliunda kamati ya uratibu wakiwamo wakufunzi wa mafunzo ya ualimu, wakaguzi wa elimu na wawakilishi kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania. Hawa walitayarisha kitabu cha mwongozo chenye lengo la kuziba ‘ombwe’ lililokuwapo la kitaaluma kati ya wanafunzi wa darasa la saba na kidato cha kwanza.
‘Ombwe’ hili lilikuwa ni la kitaaluma kwani kiwango cha taaluma kwa mwanafunzi wa darasa la saba na kidato cha kwanza ni kikubwa. Kwa hiyo ili kuziba ombwe hili kilitayarishwa kitabu chenye vielelezo vya ufundishaji.
Tangu awali waliona kuna tatizo kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza kuweza kumudu masomo yote kwa lugha ya Kiingereza. Hivyo kamati iliyoundwa kutokana na idara zilizotajwa hapo awali ilikuwa na manufaa makubwa kwa walimu na wanafunzi. Masomo yaliyoandaliwa kufundishwa ni ya masomo ya Kiingereza, Kiswahili, sayansi, hisabati, jiografia, historia na uraia.
Kipindi maalumu cha kuwasaidia wanafunzi waliofaulu kujiunga na elimu ya sekondari ilikuwa ni kati ya mwezi Desemba na Januari. Hiki ni kipindi wazazi nao walipenda kuwapeleka watoto wao twisheni badala ya kukaa nyumbani na kuangalia runinga au kucheza michezo ya kompyuta. Kitabu hiki kilijulikana kama ‘Pre-form 1 Manual’.
Maandalizi ya kitabu hiki yalitokana na utafiti wa pamoja wenye lengo la kutumia kipindi cha likizo cha takriban mwezi mmoja na nusu kuanzia mwezi Desemba hadi mwezi Januari mwanzoni ili kuwasaidia vijana hawa.
Baada ya mafunzo haya wanafunzi walianza masomo yao ya kawaida ya kidato cha kwanza bila matatizo. Huu ulikuwa ni utaratibu uliopendwa na wazazi, walimu na pia wanafunzi. Haya ni mafanikio makubwa.
Katika tathmini iliyofanyika baada ya mafunzo haya ya ‘Pre-form One’ ilionyesha kuwa yako mabadiliko chanya kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza. Wanafunzi walipata ari mpya ya kujiamini kwa kuzungumza lugha ya Kiingereza ndani na nje ya darasa.
Ushauri wangu ni kuwa Wizara iangalie upya mpango huu ili kuziba mwanya uliopo wa kitaaluma kati ya darasa la saba na kidato cha kwanza na hivyo kuondoa kabisa utapeli unaofanywa na baadhi ya walimu wanaoendesha twisheni kiholela.