Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

May Day: Siku ya Wafanyakazi isiyowahusu wastaafu!

Siku chache zilizopita, tumetoka kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi, ambayo kwa hapa Tanzania Siri-kali ilifanya jambo jema la kuwatangazia nyongeza ya mshahara wa kima cha chini kutoka shilingi laki tatu na hamsini elfu hadi shilingi laki tano kwa mwezi.

Ninaomba kurudia tena hapo: Siri-kali ilitangaza nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi, na tena ikatamka wazi kuwa nyongeza hiyo itapatikana kwenye mifuko ya wafanyakazi hao mwisho wa mwezi wa Julai.

Kwa kuwa nyongeza hiyo ilitangazwa Mei Mosi – Siku ya Wafanyakazi – itawabidi wasubiri hadi mwisho wa mwezi Julai, miezi mitatu baadaye, ili kuiona nyongeza hiyo mifukoni mwao!

Mstaafu wetu akajikuta akikumbuka Oktoba mwaka jana ambapo Siri-kali iliwatangazia wastaafu waliokuwa kwenye kima cha chini cha mshahara nyongeza ya shilingi elfu hamsini – narudia hapo – elfu hamsini, baada ya kilio chao cha miaka 21 cha kuitaka Siri-kali iwakumbuke (miaka 21!).

Hatimaye Oktoba mwaka jana (2024) ikafanya hivyo kwa kuwatangazia wastaafu nyongeza ya shilingi elfu hamsini, nyongeza ambayo – kama hawa wafanyakazi wa Mei Mosi – ingeingia mifukoni mwao miezi mitatu baadaye, yaani mwishoni mwa mwezi Januari, ili kuboresha maisha yao!

Januari ikafika mwisho wa mwezi, na ikawa ni kilio kwa wastaafu walipoona kuwa hakuna nyongeza ya shilingi elfu hamsini iliyoongezwa kwenye pensheni yao ya laki moja na elfu tano kwa mwezi kwa miaka 21! No, hakukuwa na chochote.

Wastaafu wakaishia kupata kati ya shilingi elfu tano mpaka elfu kumi tu, badala ya shilingi elfu hamsini iliyoahidiwa na Siri-kali, huku ikidai kuwa ilikuwa inataka kuboresha maisha ya mstaafu!

Kuyaboresha kwa nyongeza ya shilingi elfu hamsini kwa mwezi, na mwishoni kuishia kuwa elfu kumi? Usitake nicheke, tafadhali!

Mstaafu wetu bado anatafuta nani kati ya wastaafu wenzake wachache waliokuwa kwenye kima cha chini cha mshahara ambaye amepata shilingi elfu hamsini kama nyongeza iliyoahidiwa na Siri-kali Oktoba mwaka jana. Hajampata hata mmoja.

Wote wameishia kupata shilingi elfu tano hadi elfu kumi, yeye akiwa mmojawapo wa waliopata nyongeza ya shilingi elfu kumi – sijui kwa hesabu gani!

Wahusika, hebu acheni mizaha na maisha ya wazee wenu. Hebu angalau muungwana mmoja ajitokeze na kuweka wazi kumetokea nini hadi yeye mstaafu, na wenzake, wapate nyongeza ya kati ya shilingi elfu saba mpaka kumi badala ya shilingi elfu hamsini walizoahidiwa na Siri-kali katika kile kilichoelezwa kwamba ni juhudi za kuboresha maisha yao!

Mstaafu wetu anarudia tena kuwaomba Waheshimiwa wanaohusika waache kufanya hii mizaha mibaya na maisha ya wastaafu wa taifa. Elfu hamsini wanayodai kuwaongezea kwenye pensheni yao baada ya miaka 20 ni kichekesho – hii inayoishia kubaki elfu kumi ni nini? Shilingi elfu arobaini zetu zimekwenda wapi?

Mbona mlijitokeza mbele ya vyombo vya habari kwa mbwembwe kuitangaza nyongeza ya shilingi elfu hamsini mliyotupa, lakini hamjitokezi tena mbele ya vyombo hivyohivyo kwa mbwembwe zilezile kueleza kwa nini tuishie kupata elfu kumi badala ya elfu hamsini tuliyoahidiwa? Shilingi elfu arobaini zetu zimechepukia wapi? Je, kikokotoo kimetukokotoa wastaafu?

Yaani hiki kikokotoo chenu kinakokotoa hata juhudi za Siri-kali za kuboresha maisha ya wastaafu? Kikokotoo kinafanya nini huku kwenye nyongeza ya wastaafu waliobakiza miaka michache kuelekea Kinondoni? Uboreshe maisha yao yepi? Yale ya Kinondoni?

Au ndiyo tubaki kupapasa-papasa ili kujua kwamba labda nyakati hizi za watu kuruhusiwa kula kwa urefu wa kamba zao wameamua kuhomola kikweli kweli (kumbuka uchaguzi ni mwaka huu!) na kumuacha mstaafu wa taifa akishia kupiga miayo na kuiona Kinondoni ikimkaribia kwa kasi!

Tapikeni haraka nyongeza yetu ya elfu hamsini – siyo elfu kumi – iliyotupangia Siri-kali! Fasta!


 0754 340606 / 0784 340606