Prime
Maswali magumu ya Mstaafu yanapokosa majibu rahisi

Mheshimiwa Rais – Salamu Mheshimiwa Rais na pole kwa kazi ngumu za kuongoza kulijenga taifa letu hili. Mheshimiwa Rais wetu, ninajua kuwa muda wako ni muhimu sana lakini ninakuomba sana ukubali kupoteza dakika chache tu za muda wako muhimu ili kusoma kilio cha miaka mingi cha wastaafu wa kima cha chini wa nchi hii, ambao walimwaga damu na jasho lao kuifikisha nchi yetu ilipo sasa
Mheshimiwa, je, wasaidizi wako uliowateua kushughulika na wastaafu wamepata kukujulisha kuwa wastaafu wa kima cha chini wa taifa hili inawabidi sasa kuishi kimiujiza kwa pensheni ya Sh105,000 kwa mwezi kwa miaka 21 sasa, toka yule muungwana mstaafu wa Msoga alipowapandishia pensheni yao kutoka Sh50,000 waliyokuwa wakipata hadi kuwa hiyo laki moja na elfu tano, ambayo miaka michache baadaye iligeuka kuwa ‘Laki si Pesa’?
Je, wasaidizi wako hawa wamekujulisha kuwa mwezi Oktoba mwaka jana (2024) walitutangazia kuwa siri-kali yako ilikuwa imeamua kuwaongeza wastaafu wa kima cha chini Sh50,000 kwenye pensheni yao ya Sh105,000 katika kile walichoeleza kuwa ni juhudi za siri-kali yako kutupa nafuu ya hali ngumu ya maisha inayotukabili, kama alivyokuwa amefanya yule muungwana wa Msoga miaka 21 iliyopita?
Wamekufahamisha kuhusu kututaka wastaafu tuisubiri nyongeza hiyo kutoka Oktoba 2024 hadi Januari 2025 ndipo itakapoingia mifukoni mwetu? Januari imefika na hakuna, rudia hapo Mheshimiwa Rais, hakuna kilichoingia mifukoni mwetu, bali Sh10,000 tu na sio Sh50,000 kama walivyoahidi Oktoba, na hakuna msaidizi wako yeyote ambaye amejitokeza kulieleza hili kama walivyojitokeza kwa bashasha Oktoba kutujulisha kuhusu nyongeza hiyo!
Mheshimiwa Rais, tunakuomba sana, wakati ukifuatilia kujua kilichotokea, tunakuomba ufanye kama vile vitabu vyetu vya dini visemavyo, “Sema neno moja tu, na roho zetu (wastaafu) zitapona.” Wakati ukitafuta ukweli wa hili, tafadhali sana tamka ‘neno moja tu’ kuwa ‘walipeni wastaafu wetu wa kima cha chini 300,000 tu kwa mwezi, kwani wameteseka vya kutosha kwenye nchi waliyoijenga wenyewe’…na roho zetu zitapona! Mheshimiwa, unao uwezo huo. Wastaafu tunakuomba uutumie.
Rais Mstaafu – Salamu na pongezi sana Mheshimiwa Rais Mstaafu kwa ustaafu wako hapo Msoga. Wastaafu wenzio tunaomba kukujulisha tu kuwa bado tunapokea pensheni ya Sh105, 000 ileile uliyotupa miaka 21 iliyopita. Tumemshtua Mheshimiwa Rais aliyepo madarakani atafute jibu ya nini kimetokea hadi nyongeza ya pensheni yetu iishie kwenye makaratasi tu na sio mifukoni mwetu.
Tunakuomba sana Mheshimiwa Rais Mstaafu ukiombwa msaada na wasaidizi wanaohusika ili kujua wewe uliwezaje kutuongeza Sh50,000 nzima kwenye pensheni yetu bila kututaka tusubiri miezi mitatu kwanza ndipo tuipate, wakati ule tukitumia mataipureta mazito tofauti na sasa wanapobonyeza tu kizenji ‘vipakata paja’ wanavyoviita Lap top, lakini imebidi wastaafu tukae miezi mitatu mizima ili kuiona nyongeza kwenye mifuko yetu, ambayo hatujaiona, tafadhali wasaidie ili watusaidie!
Bunge – Nyinyi ni wawakilishi wetu zaidi ya 350 mnaopokea mshahara na marupurupu hadi shilingi milioni 16 kwa mwezi! Hivi ni kweli mnakuwa na amani gani mnaposikia kuwa mpiga kura wenu mstaafu wa kima cha chini anapokea pensheni ya shilingi laki moja na alfu tano tu kwa mwezi? Kama hali ni ngumu kwa vijana, kwetu wastaafu wa kima cha chini tunaolazimika kuishi kimiujiza itakuwaje?
Waheshimiwa Wastaafu – Wastaafu mawaziri, wakurugenzi, makatibu, wakuu wa mikoa na kadhalika mnapaswa kuwa wenzetu pamoja na pensheni zetu kututofautisha. Wakati sisi wenzenu wa kima cha chini tukipambana na pensheni ya shilingi laki moja na elfu tano kwa mwezi kwa miaka 21 sasa, nyinyi waheshimiwa wetu tunaamini kuwa mnapata pensheni kuanzia laki tano hadi milioni kadhaa kwa mwezi, ambayo kwenye hiyo miaka 21 tunayopambana na ’laki si pesa’ yetu, tuna hakika nyinyi mmepata nyongeza ya kueleweka mara kadhaa!
Tukumbushe tu kidogo hapa kuwa nyinyi ndio mlikuwa viongozi wetu wakati sisi wa kima cha chini tukiwa ndio watekelezaji wa mliyopanga wakati tukipitia sera za taifa kama za ‘Uhuru ni kazi’, ‘Kisomo cha watu wazima’, ‘mtu ni afya’ na kadhalika, na waheshimiwa mkatuongoza hadi kule Arua tulipomfanya Nduli Idi Amin Dada aliyevamia nchi yetu akione cha moto na achape lapa’ pamoja na wenzetu wengine kupata vilema vya maisha. Mbona mmetusahau?
Unganisheni sauti zenu kama waheshimiwa wastaafu mumkumbushe Mheshimiwa Rais kuwa sisi wastaafu wa kima cha chini tunastahili kupata pensheni ya japo shilingi Laki tatu tu kwa mwezi, ambazo kutokana na umri wetu hatutaitia hasara sana siri-kali maana baada ya muda mfupi tu tutarudi mavumbini tulikotoka ambako sasa tumebaki wachache tu baada ya wenzetu wengi kutangulia! Waheshimiwa wastaafu wenzetu tunaotofautiana kwa hadhi tu ya pensheni zetu tunaomba mpaaze sauti zenu katika hili. Mnatufahamu.
Viongozi wa dini– Mko na sisi toka tulipoipa uhuru nchi yetu na mlituona tulivyotoka damu na jasho letu ili kuijenga. Walimu, madakitari, wakunga, wanajeshi, polisi, makarani na wengine wote tuliokuwa kima cha chini cha mshahara. Bila shaka mmegundua kuwa kasi yetu katika kutoa zaka na sadaka zinazohusu dini zetu imepungua mno miaka ya karibuni. Msitulaumu na mtusamehe tu.
Tunaomba tu kwenye ibada zetu za Ijumaa na Jumapili muweke maombi maalumu ili mstaafu wa kima cha chini wa nchi hii apate kinachomstahili aweze kurudi mavumbini kwa amani, huku akiweza kurudisha sio tu kasi yake ya kutoa sadaka na zaka zinazohusu dini zetu, bali pia baada ya ajira yake ya miaka 40 ya kima cha chini awezeshwe kutoka huko chini aliko mpaka watu wanamsahau! Shime, wote tupaze sauti zetu maana sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, ‘Vox Populi Vox Dei’, ‘kisambaa’ ni ili kuweka msisistizo!