Maporomoko Same yapate suluhisho
Novemba 2019 watu 24 walifariki dunia katika ukanda wa milimani katika kitongoji cha Manja, Kata ya Mamba Myamba wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro.
Tukio kama hilo lilitokea tena mwaka jana wilayani humo na pia juzi, ingawa idadi ya vifo inatofautiana.
Huu ni wakati wa kusema inatosha, maporomoko haya ya udongo na magema katika maeneo ya ukanda wa milimani wilayani humo yatafutiwe suluhisho la kudumu.
Katika tukio la 2009 lililopoteza watu 24 katika kata hiyo ya Mamba Myamba, mtoto Zainabu Bakari (12) alinusurika, licha ya wazazi wake na wadogo zake kupoteza maisha.
Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete wakati huo alisema Serikali itamsomesha mtoto huyo hadi elimu ya chuo kikuu, na kugharimia ujenzi wa nyumba mpya nane zilizokuwa zimefunikwa na maporomoko hayo ya mawe na udongo.
Kikwete baada ya kutembelea eneo la maafa, alisema wataalamu wa miamba walikuwa wamemwarifu kuwa yapo mawe katika vijiji vya Goha na Kambeni yanayoweza kusababisha maafa makubwa kama hatua hazitachukuliwa.
Hata hivyo, wataalamu hao wa miamba walikuwa wamemhakikishia kuwa jiwe moja litapasuliwa kwa baruti na lingine lingejengewa kulipa uimara kuepusha maafa.
Ni imani yetu kwamba wataalamu walifanya hivyo na pengine kuifanyia uchunguzi miamba yote iliyopo.
Leo miaka 15 imepita tangu tukio hilo, bado maafa yanayotokana na maporomoko ya miamba na magema yanaendelea kuathiri wananchi wanaoishi ukanda huo wa milimani.
Taarifa kutoka katika wilaya hiyo zinaeleza kuwa watu wengine sita wamefariki dunia katika wilaya hiyo kati ya Desemba 20 hadi 22, 2024 baada ya nyumba zao kuangukiwa na gema katika vijiji vya Mjema na Miomo wilayani humo.
Ukiacha maafa hayo, Januari mwaka huu, watu wawili, akiwamo mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Lugulu walifariki dunia baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuangukiwa na gema kutokana na mvua.
Ni ukweli usiobishaniwa kuwa wananchi wengi katika ukanda huo wamejenga nyumba zao ama karibu kabisa na miamba au chini ya miamba au magema na wameishi huko miaka nenda rudi bila kupata maafa.
Lakini ni ukweli pia nchi yetu kama yalivyo mataifa yote duniani, inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha baadhi ya maeneo kupata mvua nyingi juu ya wastani, hivyo miamba na magema haviwezi kubaki salama miaka yote.
Ni raia yetu kwa Serikali kupitia watalaamu wake ifanye ukaguzi wa miamba iliyopo katika Wilaya ya Same kujiridhisha uimara wake wa kuhimili mvua nyingi na ile yenye hatari basi hatua zichukuliwe.
Utafiti huo uende kuchunguza pia nyumba zilizojengwa kwenye magema au chini ya magema ya udongo ili kuona uimara na usalama wa maeneo hayo na kama ni hatarishi basi wananchi waelezwe na kushirikishwa hatua za kuchukua.
Tunafahamu wapo ambao maeneo hayo ni ya asili na wanaweza kuona ugumu wa kuhama na kutafuta makazi mapya kwa sababu wameishi hapo miaka mingi, lakini watambue kuwa uhai hauwezi kununuliwa dukani, ukishaondoa umeondoka.
Serikali inaweza kuiga njia iliyotumia kutafuta suluhisho kule Hanang, baada ya maporomoko yaliyoua watu 68 na kujeruhi maelfu ili kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakazi hao wa Same wanaoishi maeneo hatarishi.