MAONI: Tunalaani taarifa za uvumi za KLM

Juzi Serikali imekanusha taarifa iliyotolewa na Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM) ya kuwepo kwa hali ya hatari nchini na hivyo kusitisha safari zake zilizopangwa kufanyika Dar es Salaam na Kilimanjaro.

KLM Januari 27, 2023 ilitoa taarifa kwenye tovuti yake ikitahadharisha abiria wake na kueleza kusitisha safari katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA).

Tunalaani kitendo cha KLM cha kutaka kuleta taharuki ndani na nje ya nchi huku Tanzania ikijulikana ni salama na imechukua hatua zote za kuzuia na kupambana na vitendo vya kihalifu ikiwemo ugaidi kwa kutunga sheria na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa.

Tunasema hivyo tukiamini kwamba kama KLM ilifuata tahadhari iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini kutahadharisha raia wake wanaoishi Tanzania, ilipaswa kwanza kuwasiliana na mamlaka husika za ndani kujua ukweli.

Ubalozi uliotoa tahadhari hiyo wala haukufunga ubalozi wake au kuwakusanya raia wake, pia safari za ndege za kimataifa ziliendelea kufanyika nchini, tunajiuliza kwa nini iwe kwa KLM pekee?

Hii ni kwa sababu uamuzi uliochukuliwa na KLM una athari mbaya kwa nchi yetu kwa maana ya utalii, usafiri wa anga na biashara kwa ujumla, jambo ambalo lisiposahihiswa na kuelezwa kwa uhalisia linaweza kuathiri vibaya uchumi wetu.

Kwa kuwa hatujui lengo la KLM kutoa taarifa hiyo lilikuwa ni nini, lakini tunawakumbusha kuwa Tanzania imekuwa mstari wa mbele kupambana na vitendo vya kihalifu ikiwemo ugaidi.

Tunaikumbusha KLM kwamba Bunge la Tanzania limetunga Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002 na kutungiwa Kanuni zake mwaka 2014.

Kama KLM hawafahamu basi dunia inafahamu, tangu kutungwa kwa sheria hiyo kuna watuhumiwa wengi wa ugaidi walikamatwa, wengine wamehukumiwa vifungo jela na wengine bado wako mahabusu huku kesi zao zikiendelea mahakamani. Na wengi wa watuhumiwa hao ni Watanzania.

Kwa kuonyesha Tanzania kipaumbele chake kikubwa ni ulinzi na usalama, Septemba 2022, Bunge liliridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004 ili kudhibiti vitendo vya kigaidi.

Wakati akiwasilisha azimio hilo bungeni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni alitaja bila kificho kwamba kumekuwa na matukio yenye viashiria vya ugaidi katika mikoa ya Arusha, Geita, Mwanza, Pwani na Tanga na vimedhibitiwa.

Pia, Masauni alitoa mfano wa tukio la kigaidi lililotokea Uganda mwaka 2010 na kuwa watuhumiwa wawili ambao ni raia wa Uganda walikamatwa Tanzania na kurudishwa huko.

Bunge liliridhia itifaki hiyo kwa lengo la kuzuia na kupambana na kuenea kwa itikadi za msimamo mkali zinazosababisha watu kuhamasika na kujiunga na vikundi vya kigaidi na vikundi vyenye misimamo mikali nje ya nchi.

Pia, tunaikumbusha KLM kuwa Tanzania mbali na kutunga sheria na kuridhia itifaki mbalimbali pia inashirikiana na nchi jirani kulinda mipaka, mfano Msumbiji wanako kabiliwa na vitendo vya kigaidi.

KLM inatakiwa kufahamu kuwa Tanzania ndio makao makuu ya kituo cha kupambana na ugaidi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Nchi 15 wanachama wa Sadc kuamua kuiamini Tanzania na kuweka kituo hicho jijini Dar es Salaam ni kiashiria muhimu kwamba usalama wa nchi uko imara.

Pamoja na kulaani uvumi huo, tunatoa wito pia upuuzwe.