Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mabalozi mmelala, amkeni Taifa linawahitaji

Muktasari:

  • Hali halisi ilivyo sasa, ni dhahiri kwamba mabalozi wetu wengi walioko nje ya nchi hawatimizi wajibu huu kwa kiwango kinachotarajiwa.

Mabalozi ni wawakilishi wa Taifa letu  nje ya mipaka, wakiwa wametumwa rasmi na Serikali kuendeleza maslahi ya nchi  katika nyanja mbalimbali kama vile siasa, uchumi, utamaduni na diplomasia.

Wale wanapopewa jukumu hili, wanapaswa kuwa macho, wabunifu na waliojitoa katika kuitangaza nchi, kufungua fursa kwa Watanzania na kujenga taswira chanya ya taifa kimataifa.

Hata hivyo, hali halisi ilivyo sasa, ni dhahiri kwamba mabalozi wetu wengi walioko nje ya nchi hawatimizi wajibu huu kwa kiwango kinachotarajiwa. Kwa maneno mepesi, wanatuangusha.

Moja ya maeneo ambayo mabalozi wetu wengi wameonyesha udhaifu mkubwa ni katika kutangaza fursa zilizopo katika nchi wanazohudumu.

Dunia ya sasa imefunguka; kuna fursa lukuki katika elimu, biashara, teknolojia, sanaa, na hata ajira.

Lakini ni mara chache sana kusikia ubalozi wa Tanzania ukitoa taarifa za wazi kuhusu nafasi za masomo, mikutano ya kibiashara, au hata maonesho ya kimataifa yanayoweza kuwafaidisha Watanzania.

Hali hii inaacha maswali mengi; je, mabalozi hawazifahamu hizi fursa au wamezichukulia kama si sehemu ya wajibu wao?

Kwa mfano, lugha ya Kiswahili sasa imepata hadhi kubwa duniani. Mataifa mengi barani Afrika, Asia, Ulaya na hata Amerika yameonyesha nia ya kujifunza Kiswahili.

Baadhi yameanza hata kukifundisha katika shule na vyuo vikuu. Huu ni mlango mkubwa wa fursa kwa Watanzania. Walimu wa Kiswahili wanaweza kupata ajira nje ya nchi, vitabu vya Kiswahili vinaweza kuuzwa nje, na hata utalii wa kitamaduni unaweza kuchochewa kupitia lugha hii adhimu.

Lakini ni mara ngapi tumesikia mabalozi wetu wakijitokeza kuhamasisha upatikanaji wa fursa

Kiswahili au kuanzisha madarasa ya lugha katika nchi wanazowakilisha?

Natambua wapo waliojaribu akiwamo Balozi Humprey Polepolee, lakini kwa hali ilivyo mabalozi wengi zaidi wanapaswa kujitokeza kueleza fursa za Kiswahili hasa kipindi hiki ambacho natambua balozi zetu kupewa mwongozo maalumu wa kukiuza Kiswahili.

Ninachokiona, wapo ambao wamepewa nafasi hizi lakini wamezichukulia kama likizo ya maisha na sifa ya hadhi ya ubalozi pekee.

Hawajihusishi na jamii ya Watanzania walioko nje, wala kushiriki katika mijadala au mikutano ya kukuza ushirikiano wa nchi.

Wengine huonekana tu wakati wa mapokezi ya kidiplomasia, lakini katika shughuli za msingi za kuitangaza nchi na kuonyesha fura kwa Watanzania,  wapo mbali mno.

Ni nadra kuona taarifa za kazi au mafanikio ya mabalozi wetu kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii. Wamekaa kimya kana kwamba wanahifadhi utulivu wa pensheni zao badala ya kuwatumikia wananchi waliowaamini.


Hali hii imesababisha Watanzania wengi kukosa taarifa muhimu zinazoweza kubadili maisha yao. Vijana wetu wangeweza kufaidika kwa kujua kuhusu nafasi za masomo nje, wajasiriamali wangepata masoko mapya ya bidhaa zao, na walimu wa Kiswahili wangeweza kutumika kama wajumbe wa kueneza utamaduni wetu duniani. Lakini kwa sababu mabalozi wetu wengi hawafanyi kazi kwa bidii, hizi ndoto hubaki hewani.


Hata hivyo, haimaanishi kwamba wote ni wabovu. Wapo mabalozi wachache wanaoonyesha mfano bora kabisa. Kwa mfano, tumeshuhudia baadhi ya balozi zikianzisha madarasa ya Kiswahili.

Mabalozi wengine wamekuwa mstari wa mbele kuwakaribisha wawekezaji, kuandaa makongamano ya biashara, na hata kushiriki kwenye maonesho ya kimataifa wakitangaza vivutio vya Tanzania kama utalii na bidhaa nyingine za kipekee.

Mabalozi hawa wachache wanaonyesha kwamba, pale ambapo dhamira ya kweli ipo, matokeo chanya yanawezekana.


Wengine wamekuwa na ushirikiano wa karibu na Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora), wakiwapa nafasi ya kushiriki katika shughuli za maendeleo ya nyumbani.

Hawa ndio mabalozi tunaowahitaji – wale wanaojua kuwa nafasi waliyopewa ni heshima na dhamana kubwa kwa Taifa.

Wanatumia kila fursa waliyonayo kuitangaza Tanzania, kusaidia Watanzania wanaohitaji msaada, na zaidi ya yote, kutengeneza mazingira bora ya ushirikiano wa kimataifa.

Serikali nayo ina jukumu kubwa la kuhakikisha mabalozi wake wanawajibika. Haitoshi tu kuwateua na kuwaacha wafanye wanavyotaka.

Ufuatiliaji, tathmini ya utendaji na kuwekewa malengo ya kila mwaka,  ni mambo muhimu yanayopaswa kufanywa. Ikiwezekana, wananchi wapewe nafasi ya kutoa mrejesho kuhusu mabalozi hawa kupitia mitandao au njia rasmi  ili kujua namna wanavyotimiza majukumu yao. Wasiowajibika wakae kando.

Tunahitaji mabalozi wachapakazi, wabunifu, wazalendo;  watu watakaowakilisha Taifa kwa fahari, si kwa kujitapa kwa hadhi ya ubalozi pasipo utekelezaji wa majukumu ya kibalozi.


Abeid Poyo ni mhariri wa makala wa Mwananchi