Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maandalizi AFCON yazingatie haya

Mshambuliaji wa Taifa Stars, Salum Mwalimu akimtoka beki wa Morocco. Picha na Mtandao

Baada ya Tanzania, Kenya na Uganda kumaliza kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), macho ya Afrika tayari yanaelekezwa kwenye mtihani mkubwa zaidi.

Haya ni maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027. Huu si mtihani wa michezo pekee, bali ni jaribio la uwezo wa nchi katika mifumo ya uendeshaji, miundombinu, teknolojia na taswira ya kimataifa. Kwa Tanzania, huu ni wakati wa kihistoria unaohitaji maandalizi ya mapema na ya kina.

Kipaumbele cha kwanza ni miundombinu ya viwanja na mazingira yake. Ni kweli kuwa baadhi ya viwanja vinajengwa upya na vingine vinaboreshwa, lakini kasi ya utekelezaji ni jambo lisilopaswa kubezwa.

Muda unasonga, na AFCON si tukio la kusubiri dakika za mwisho. Viwanja vinavyotarajiwa kutumika lazima vikidhi viwango vya CAF na FIFA.

Zaidi ya hapo, miundombinu inayovizunguka viwanja kama barabara, maegesho, usafiri wa umma na huduma za dharura ni lazima ipangwe na kutekelezwa sasa.

Pili, usafiri na malazi vinapaswa kupewa uzito unaostahili. AFCON huvutia maelfu ya mashabiki kutoka mataifa mbalimbali, hivyo viwanja vya ndege, reli, mabasi ya mijini na huduma za teksi vinapaswa kuboreshwa.

Kwa upande wa malazi, Tanzania imewahi kuandaa mashindano makubwa bila changamoto kubwa, lakini maboresho ya ziada hayakwepeki, hasa ikizingatiwa kuwa zaidi ya mataifa 24 yatashiriki mashindano hayo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Tatu, uwekezaji katika teknolojia na ubunifu wa kidijitali ni jambo lisiloepukika. Mashindano ya kisasa hayawezi kufanikiwa bila mifumo ya tiketi za kielektroniki, mawasiliano ya haraka, intaneti yenye kasi na mifumo ya kisasa ya ulinzi na udhibiti wa umati.

Hatua hizi zitaboresha ufanisi wa uendeshaji na kuongeza imani ya mashabiki pamoja na wadau wa kimataifa.

Nne, rasilimali watu ni nguzo muhimu ya mafanikio. Waandaaji, wahudumu wa viwanja, vyombo vya ulinzi, wahudumu wa afya na wajitolea wanapaswa kupata mafunzo ya viwango vya kimataifa.

AFCON ni zaidi ya mechi za mpira; ni tamasha linalohitaji huduma bora na ukarimu. Hapa ndipo taswira ya Mtanzania mkarimu na mchangamfu inapaswa kung’ara.

Zaidi ya yote, AFCON 2027 inapaswa kutumika kama jukwaa la kutangaza utalii, utamaduni na fursa za uwekezaji.

Kupitia muziki, vyakula, sanaa na vivutio vya utalii, Tanzania inaweza kujenga taswira chanya itakayodumu hata baada ya mashindano kumalizika.

Taasisi zinazohusika na utalii zinapaswa kuanza sasa kuitangaza nchi na kuwavutia mashabiki kutembelea vivutio vyetu kabla, wakati na baada ya mashindano.

Kwa ujumla, maandalizi ya AFCON 2027 hayapaswi kusubiri kesho. Yanahitaji mipango thabiti, uwazi na ushirikishwaji wa sekta zote kuanzia sasa. Huu ni wakati wa kuchukua hatua, si wa ahadi.

Serikali na wadau  wanapaswa kufanya kazi kwa karibu, kila mmoja akitekeleza wajibu wake. Uzoefu wa mashindano ya CHAN utolewe kama funzo la kubaini upungufu na kuurekebisha mapema. AFCON 2027 ni fursa ya kujitangaza, kujifunza na kuacha alama ya kudumu.