Mbunge atilia shaka maandalizi ya AFCON 2027
Mbunge wa Korogwe Vijiji, Timotheo Mzava. pI
Dodoma. Mbunge wa Korogwe Vijiji, Timotheo Mzava ameonyesha hofu kuhusu uhamasishaji wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 akitaka Serikali na wadau kuingilia kati.
Mzava ametoa kauli hiyo alipokuwa akichangia kwenye mjadala wa hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan alioutoa Novemba 14, 2025 wakati akizindua bunge la 13.
Amesema bado Tanzania haijawekeza vya kutosha kwenye sekta ya michezo jambo linalotia mashaka kwenye mashindano ya mwakani.
Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu wenyeji wa fainali za AFCON 2027 nyingine zikiwa ni Uganda na Kenya na hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa nchi hizo tatu kuandaa mashindano hayo.
Awamu ya mwisho ya AFCON ilikuwa Morocco ambako Fainali hizo zilimalizika Januari 18, 2026 ambapo Senegal ilitwaa ubingwa baada ya kuwafunga wenyeji kwa bao 1-0.
“Niombe Serikali tuwekeze nguvu kwenye sekta ya michezo ili kukuza uchumi wa nchi. AFCON inafanyika lakini hatuoni amsha amsha ya mashindano haya, ni muhimu tukalitazama hilo,” amesema Mzava.
Mzava pia ameomba hamasa ya mashindano hayo iendane na mkazo kwenye miundombinu katika vituo vya utalii ili watalii wakija wafurahie lakini kuwepo na mfumo wa kudhibiti Vyuo vya utalii ili wanaotoka kwenye humo wawe na uwezo wa kuleta tija kwenye sekta hiyo.
Fainali za AFCON 2027 zimepangwa kufanyika kuanzia Juni hadi Julai 2027 katika tarehe ambazo bado hazijawekwa wazi.