Prime
Je, mwananchi anakuwaje TRA?

Kodi ni chanzo kikuu cha mapato kwa serikali yoyote duniani. Katika Tanzania, kodi huchangia sehemu kubwa ya bajeti ya taifa, hivyo ina umuhimu wa kipekee katika kugharamia huduma za jamii kama afya, elimu, maji safi na miundombinu.
Ingawa jukumu la kisheria la kukusanya kodi lipo mikononi mwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wananchi nao wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa kodi hiyo inakusanywa ipasavyo kwa kushiriki kikamilifu katika udhibiti wa ukusanyaji wake.
Ukweli mchungu ni kwamba idadi ya walipa kodi halali nchini bado ni ndogo ukilinganisha na ukubwa wa uchumi wa taifa na ndiyo maana mara kwa mara wachumi wamekuwa wakishauri kupanua wigo wa kodi ili jukumu hilo litekelezwe na wengi.
Hali ya uchache wa walipakodi husababisha mzigo wa kodi kubebwa na wachache huku wengine wengi wakiwa hawachangii chochote, jambo linalosababisha mapato ya taifa kupungua na hivyo kuathiri kasi ya maendeleo.
Hata sehemu ndogo ya kodi inayopaswa kukusanywa kutoka kwa walipa kodi waliopo haikusanywi ipasavyo kutokana na mianya ya ukwepaji kodi na michezo mibaya inayofanywa na baadhi ya watu waliotakiwa kulipa kodi.
Sheria ya kutaka anayenunua kutoa risiti na anayeuza kudai risiti ilianzishwa kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa kodi na kuhakikisha kuwa kila mauzo yanaambatana na risiti halali kutoka kwenye mashine za kielektroniki (EFD).
Hata hivyo, bado baadhi ya wananchi hawatimizi wajibu huu kwa sababu ya kutokujali au kushawishika kushirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu wanaokwepa kodi.
Katika hali kama hiyo, mwananchi anakuwa sehemu ya tatizo, badala ya kuwa sehemu ya suluhisho.
Kudai risiti pekee hakutoshi. Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa risiti husika ni halali kwa kuangalia alama za usalama na stempu za kielektroniki kulingana na miongozo ya TRA.
Aidha, ni muhimu kukataa kushirikiana na wafanyabiashara wanaoandika thamani pungufu kwenye risiti ili kupunguza kiwango cha kodi kinachopaswa kulipwa.
Wananchi wanapaswa kutambua kuwa kwa kufanya hivyo, wanaiibia serikali yao, na kwa kufanya hivyo, wanajinyima wenyewe huduma muhimu kama madarasa, dawa hospitalini na barabara bora.
Kushiriki kwa wananchi katika udhibiti wa ukusanyaji wa kodi si suala la hiari, bali ni wajibu wa kizalendo.
Hatuwezi kuwa na Tanzania yenye maendeleo bila kuhakikisha kuwa kila mmoja wetu anatimiza wajibu wake kwa kutoa na kudai risiti, kufichua wakwepaji wa kodi, na kutokubali kushiriki kwenye vitendo vyovyote vinavyozuia mapato kuingia serikalini. Kila kodi inayokusanywa inajenga daraja, zahanati au shule mahali fulani nchini.
Kwa mantiki hiyo, wananchi ni mhimili muhimu katika kuhakikisha mfumo wa kodi unafanya kazi. Ushiriki wao unapaswa kuimarishwa kupitia elimu, uwazi na ushirikiano wa karibu kati yao na mamlaka za mapato.
Kila risiti unayodai ni mchango wako wa moja kwa moja katika maendeleo ya taifa. Hivyo basi, tuchukue hatua leo kwa kuwajibika, kudai risiti, na kutokushirikiana na wakwepaji – kwa sababu maendeleo ya Tanzania yanatubeba sote.
Ukishiriki katika ukwepaji kodi au kuacha mapato ya nchi yakavuja mwathirika mkubwa ni wewe ambaye itakosa huduma muhimu.