Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zitto Kabwe: Tunahitaji dhamira safi kisiasa, uchaguzi ulio huru na haki

Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadharauliofanyika Bangwe, Kigoma.

Muktasari:

  • Kiongozi huyo mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, jana alichukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chake kugombea tena ubunge Kigoma Mjini, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, baada ya kukaa nje kwa miaka mitano.

Kigoma. Kiongozi wa zamani wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hali ya kisiasa nchini kwa sasa si ya kuridhisha huku akidai kuwa baadhi ya viongozi hawana dhamira njema hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Zitto ametoa kauli hiyo jana Jumapili Mei 4, 2025, wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Bangwe, Jimbo la Kigoma Mjini.

Amesema ingawa Taifa linaweza kuwa na sheria na maadili ya uchaguzi, hayo pekee hayatoshi kama hakuna dhamira safi ya kisiasa kutoka kwa viongozi.

“Tunaweza kuwa na sheria bora kabisa, lakini kama dhamira ni mbovu, sheria hizo hazitaheshimiwa. Vilevile, hata kama sheria si nzuri, dhamira njema inaweza kuzifanya zikae pembeni kwa ajili ya haki,” amesema Zitto.

Baadhi ya wanachama wa ACT-Wazalendo wakimsikiliza Zitto Kabwe ambaye ametia nia kugombea ubunge Kigoma Mjini.

Ameongeza kuwa kwa sasa, mjadala wa kisiasa umejikita zaidi katika nani yuko sahihi badala ya kuangalia hoja gani ni sahihi.

“Juzi mmesikia kiongozi wa TEC alivyoshambuliwa kwenye maeneo yao. Hatuwezi kuwa na taifa ambalo mtu anapozungumza huangalia nani anamwona au kumsikiliza. Tunahitaji mjadala wa hoja, si wa watu,” amesisitiza.

Amewataka viongozi wote wa kisiasa wa chama tawala na wa upinzani, kukaa pamoja kwa mazungumzo ya dhati ili kulinda amani ya nchi. Amesema wajibu wa kuongoza mchakato huo uko mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Zitto pia amekumbusha kuhusu mapendekezo ya kuanzishwa kwa Tume ya Uangalizi wa Utendaji wa Jeshi la Polisi na Haki Jinai, akibainisha kuwa kwa sasa jeshi hilo limepoteza uaminifu kwa wananchi.

“Leo (juzi) nimeambiwa kuna kijana alitekwa kule Mbozi na DCI ametuma timu ya kuchunguza. Lakini polisi wanawezaje kujichunguza wao wenyewe? Tunahitaji chombo huru cha kuchunguza matendo ya jeshi hilo ili kurejesha imani ya wananchi,” amesema.

Amesema kamati iliyoundwa zamani ilishatoa mapendekezo ya kuanzisha chombo huru, lakini mpaka sasa hilo halijatekelezwa.

Kwa upande wake, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya ACT-Wazalendo Kanda ya Magharibi, Juma Ramadhani amesema chama hicho kupitia vikao vyake vya Halmashauri Kuu kimeamua kuachana na siasa za maridhiano na kuanza siasa za mapambano.

Amesema hiyo ni baada ya kuona juhudi za maridhiano kupitia Baraza la Vyama vya Siasa chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, zimeshindwa kuleta matokeo yaliyotarajiwa.