Zitto achukua fomu kuomba ridhaa ya kugombea Ubunge Kigoma Mjini

Muktasari:
- Uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa nafasi za udiwani, ubunge na Urais ndani ya ACT – Wazalendo utafungwa rasmi Mei 28, 2025.
Kigoma. Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT - Wazalendo Taifa, Zitto Kabwe amechukua fomu ya kuomba ridhaa kwa chama chake kugombea ubunge Jimbo la Kigoma Mjini katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Zitto amekabidhiwa fomu hiyo leo Jumapili Mei 4, 2025 na Katibu wa ACT - Wazalendo Jimbo la Kigoma Mjini, Idd Adam ofisini kwake akiwa ameambatana na wananchama na wafuasi wa chama hicho alioambatana nao kushuhudia tukio hilo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, Zitto amesema ameamua kugombea Ubunge kupitia Jimbo hilo kutokana na mwenendo usioridhisha wa uchumi katika mkoa,
Aidha, ameeleza sababu nyingine iliyomsukuma kuchukua fomu ya kuwania Ubunge ni imani kubwa ambayo wananchi wa Kigoma, hususan wanawake, wanaendelea kumuonesha wakiamini kuwa ataweza kutetea masilahi ya wananchi.
Pia, amebainisha kuwa ongezeko la matukio ya rushwa ndani ya Baraza la Madiwani limechangia uamuzi wake wa kuomba ridhaa ya wanachama na wananchi ili kulirekebisha jambo hilo.
Ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanawachagua pia madiwani watakaogombea kupitia ACT - Wazalendo ili kufanikisha jitihada za kuondoa mianya ya rushwa katika baraza hilo.

Zitto Kabwe akionyesha fomu ya kuwania Ubunge Jimbo la Kigoma Mjini.
Hata hivyo, amesema mazingira ya uchaguzi yamekuwa ya kutia shaka tangu mwaka 2019. Licha ya changamoto hizo, amewahimiza wananchi wa Kigoma waendelee kuwa na imani naye na kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi badala ya kususia.
“Tangu mwaka 2019, mazingira ya uchaguzi yamekuwa ya mashaka, lakini nawahakikishia wana Kigoma kuwa tutajitahidi kukabiliana na changamoto hizo kwa kushiriki kikamilifu uchaguzi. Jimbo hili hatujawahi kulipata kwa urahisi, hivyo tunatakiwa kupambana,” amesema Zitto.
Baadhi ya wanachama waliohudhuria tukio hilo wameeleza imani yao kwa Zitto, wakisema ni kiongozi mzalendo anayesikiliza wananchi tofauti na wengine.
Zuwena Omar amesema; “Tunamwamini sana Zitto, yeye ndiye mkombozi wetu. Tumejipanga vizuri na mwaka huu tutamchagua kwa kishindo.”
Zitto alifanya mkutano wa hadhara jana, Aprili 3, 2025, katika eneo la Stendi ya Mwandiga, ndani ya Jimbo la Kigoma Kaskazini.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya Mkoa, Kiza Mayeye alichukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge kupitia jimbo hilo, ambalo Zitto aliwahi kuliongoza kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 kupitia chama cha Chadema.

Wengine ambao tayari wamechukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chao kugombea nafasi za ubunge mkoani Kigoma ni pamoja na Frank Ruhasha, Jimbo la Buhigwe, aliyekabidhiwa fomu na Katibu wa chama hicho wa jimbo, Dickson Bungwa.
Uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa nafasi za udiwani, ubunge na Urais ndani ya ACT – Wazalendo utafungwa rasmi Mei 28, 2025.