Zitto: Msivunje madirisha, mnaotaka kuja ACT Wazalendo milango ipo wazi

Muktasari:
- Kauli hiyo ya Zitto inakuja wakati ambao baadhi ya makada na wafuasia wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakidaiwa kuwa njia panda baada ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kutangaza kuwa chama hakitashiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Dar es Salaam. Kiongozi wa zamani wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewakaribisha wanasiasa wanaotaka kufanya siasa, akisema milango ipo wazi kujiunga na chama hicho.
Kauli ya Zitto inakuja wakati ambao baadhi ya makada na wafuasia wa Chadema wakidaiwa kuwa njia panda baada ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), kutangaza hakitashiriki Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Uamuzi huo ulitangazwa Aprili 12, 2025 Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima baada ya Chadema kususia kusaini kanuni za maadili hivyo, kukosa sifa ya kushiriki uchaguzi mkuu na ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano.
Kwa mujibu wa INEC Kanuni za Maadili zimeandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha 162 (1), (2) na (3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kinachoitaka Tume baada ya kushaurina na vyama vyote vya siasa na Serikali, kuandaa na kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitakazoainishwa na maadili ya vyama vya siasa.
Hata hivyo, kumeibuka mgogoro kuhusu ukomo wa kanuni hizo huku Chadema ikiituhumu INEC kuwa na ajenda ya kukidhoofisha. Wakati hayo yakifanyika, tayari Chadema ilishatangaza kutoshiriki kwenye uchaguzi hadi mabadiliko kwenye mfumo wa uchaguzi yafanyike ili kuhakikisha haki inatendeka kwa vyama vyote.
Msimamo huo umechagizwa na kampeni yake ya No reforms, no election ambapo, viongozi wa chama hicho wamekuwa wakifanya ziara kutoa elimu kwa wananchi.
Lakini, Leo Jumatano Aprili 16, 2025 kupitia akaunti ya mtandao X, Zitto ameandika, “Kwa wale wanasiasa ambao wanataka kufanya siasa, lakini milango imefungwa kwenye vyama vyao, wasivunje madirisha wala nyumba! Karibu@ACTwazalendo tufanye Siasa.
“Tunaweza kuleta mageuzi tukiwa mchezoni. Uchaguzi ni jukwaa la kuelimisha na kuamsha umma (mobilization). Uchaguzi ni jukwaa la kuionyesha dunia tunachopigania (exposing the flaws),” ameandika Zitto.
Baadhi ya wadau wa mtandao huo, walikuwa na mtazamo tofauti wakati wakichangia mada ya andiko hilo la Zitto aliyewahi kuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini 2005/15.
Glory Tausi alitoa mrejesho akimjibu Zitto kuwa “asante kiongozi” wakati Zingberm ameandika kitu pekee ACT Wazalendo wanaweza kufaidi ni kupata wagombea, jambo ambalo ni zuri kwa chama kupata wanachama.
“Ila suala la kuleta mabadiliko ni uongo uliochangamka, ikiwa hatutakuwa wote pamoja kupigania mifumo kwa kuilazimisha basi tusahau kuleta mabadiliko ya kitaifa,” ameandi.