Waipaisha Tanzania jumuiya ya kimataifa

Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta akimpa maua Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson baada ya kuwasili katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma. Picha na Ofisi ya Bunge
Tanzania ni nchi yenye heshima kubwa mbele ya jumuiya ya kimataifa na imekuwa ikitoa watu makini wa kusimamia mashirika au taasisi za kimataifa kwa mafanikio makubwa na kuwa chachu ya maendeleo.
Heshima hiyo ilianza kujengwa zamani wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere na kuendelea katika awamu zilizofuata ambapo baadhi ya Watanzania walifanya kazi za kiuongozi kwenye mashirika na jumuiya hizo.
Baadhi ya Watanzania hao ni Brigedia Jenerali Hashim Mbita, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) kuanzia mwaka 1974 hadi 1994 baada ya Afrika Kusini kupata uhuru.
Wengine ni Dk Salim Ahmed Salim, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambayo sasa inajulikana Umoja wa Afrika (AU) kati ya mwaka 1989 – 2001 na Getrude Mongella, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake (1996 - 1997) na Rais wa Bunge la Umoja wa Afrika (2004 - 2008).
Vilevile, yupo Anna Tibaijuka ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat) na Dk Asha-Rose Migiro aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) kati ya mwaka 2007 – 2012.
Uwakilishi huo umeendelea hadi sasa wakati wa Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan ambapo baadhi ya Watanzania wameteuliwa au kuchaguliwa kuongoza mashirika ya Umoja wa Mataifa, taasisi za kimataifa au jumuiya za kikanda.
Huwezi kutenganisha mafanikio hayo na utashi wa Rais Samia wa kuifungua nchi kwa kufanya ziara mbalimbali za kimataifa ambazo siyo tu zinaleta manufaa kwa wananchi, bali pia zinaitangaza Tanzania kimataifa.
Rais Samia kwa wadifa wake ni raia namba moja, anapeperusha bendera ya Tanzania duniani kupitia ziara zake katika mataifa na kushiriki mikutano ya kimataifa ya ngazi ya juu na mingine kuandaliwa na Serikali yake, jambo lililoleta neema kwa nchi.
Akiwa mmoja kati ya marais wanawake wachache duniani, Rais Samia amekuwa kivutio kikubwa kwa mataifa mengine kwa namna anavyoleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali na kuirudisha Tanzania kwenye uso wa kimataifa.
Tangu ameingia madarakani Machi 19, 2021, Rais Samia ametembelea nchi za India, China, Marekani, Kenya, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Falme za Kiarabu (UAE), Malawi, Msumbuji, Rwanda na Burundi.
Rais Samia amehudhuria mikutano mikubwa ya kimataifa ikiwemo mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Marekani, mkutano wa masuala ya mazingira (Cop27) huko Misri na mkutano wa mataifa yanayochipukia kiuchumi (Brics) uliofanyika Afrika Kusini.
Tanzania pia imekuwa mwenyeji wa mikutano kadhaa ya kimataifa kama vile Jukwaa la mifumo ya chakula Afrika (AFSF) uliofanyika Septemba 2023, mkutano wa rasilimali watu Afrika (Julai 2023) na mkutano wa wakuu wa nchi wastaafu uliofanyika jijini Arusha.
Mbali na mkuu huyo wa nchi, wapo Watanzania wengine ambao pia wamepata nafasi katika taasisi za kimataifa, jambo linaloelezwa na wachambuzi wa siasa za kijiografia kwamba linaitangaza Tanzania kimataifa.
Baadhi ya Watanzania wanaofanya kazi kwenye mashirika au taasisi za kimataifa ni Dk Tulia Ackson, Dk Tulia Ackson, Joyce Msuya, Elizabeth Mrema, Jaji Imani Aboud na Ghaamid Abdulbasat.
Dk Tulia na IPU
Spika wa Bunge, Dk Tulia alichaguliwa Oktoba 27, mwaka huu, kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), chombo kinachowakutanisha pamoja maspika wa mabunge 120 duniani kwa ajili ya kujadili masuala yao.
Dk Tulia alichaguliwa kwa kura172 kati ya 303 zilizopigwa huku akiwaangusha washindani wake watatu ambao wote ni wanawake na wanatoka katika bara la Afrika, jambo ambalo linaelezwa kwamba halijawahi kutokea.
Katika miaka 25 iliyopita, nafasi ya urais wa IPU imekaliwa na wabunge kutoka Misri, Hispania, India, Chile, Italia, Namibia, Morocco, Bangladesh, Mexico na Ureno.
Kwa nafasi hiyo, Dk Tulia kwa mara ya kwanza anaifanya Tanzania kuingia kwenye orodha ya mataifa yaliyowatoa marais wa chombo hicho kikubwa duniani.
Dk Tulia alitaja vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika bunge hilo, kuimarisha amani na ustawi wa IPU na kustawisha ushiriki wa makundi mbalimbali katika siasa kwenye Bunge hilo.
Joyce Msuya
Desemba 2021, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres aliteua Mtanzania, Joyce Msuya kuwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Masuala ya Kibinadamu na Naibu Mratibu wa Misaada ya Dharura (UNOCHA).
Kabla ya uteuzi huo, Msuya alikuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) lenye makao makuu yake mjini Nairobi, Kenya, nafasi aliyoitumikia tangu mwaka 2018.
Mwanamke huyo alichukua nafasi iliyoachwa na raia wa Ujerumani, Ursula Mueller ambaye Guterres alimshukuru kwa uongozi na utumishi wake wa kujitolea wakati wa uongozi wake. Msuya ana shahada ya uzamili ya Sayansi ya Mikrobiolojia na Kinga kutoka Chuo Kikuu cha Ottawa, Canada na shahada ya kwanza ya Sayansi ya Biokemia na Kinga kutoka Chuo Kikuu cha Strathclyde, Scotland.
Akiwa UNEP, Msuya aliwajibika kusimamia bajeti ya Dola za Marekani 455 milioni na miradi na operesheni yenye thamani ya zaidi ya dola 1 bilioni, iliyotolewa kupitia wafanyakazi 2,500 katika ofisi 41 na makao makuu.
Elizabeth Mrema
Desemba 2022, Katibu Mkuu Guterres alimteua Mtanzania mwingine, Elizabeth Mrema kuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, akichukua nafasi ya Msuya ambaye alihamishiwa shirika la UNOCHA.
Kabla ya uteuzi huo, Mrema alikuwa Katibu Mtendaji wa Shirika la UN Biodiversity.
Hadi anateuliwa katika nafasi hiyo mpya, Mrema alikuwa mshauri wa Makamu Rais wa Benki ya Dunia (WB) katika ukanda wa Asia Mashariki na Pacific jijini Washington DC, wadhifa alioutumikia tangu mwaka 2017.
Mrema alisishika nyadhifa mbalimbali katika ngazi ya uandamizi kwenye Benki ya Dunia ikiwemo mwakilishi wa Benki ya Dunia na Mkuu wa ofisi ya benki hiyo hiyo Korea Kusini na mratibu wa taasisi ya Benki ya Dunia inayosimamia Asia Mashariki na Pasifiki nchini China.
Jaji Imani Aboud
Mtanzania mwingine anayepeperusha bendera ya Tanzania kimataifa ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu (ACHPR) ni Jaji Imani Aboud ambaye Juni 13, mwaka huu, alichaguliwa tena kwa kipindi cha pili cha miaka miwili kuiongoza Mahakama hiyo.
Jaji Imani ambaye kabla ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kushika wadhifa huo katika Mahakama hiyo, alikuwa ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi.
Mahakama hiyo ilianza shughuli zake rasmi 2006 mjini Addis Ababa, Ethiopia na baada ya mwaka mmoja ikahamishiwa jijini Arusha, Tanzania. Mahakama hiyo inaundwa na majaji 11, raia wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.
Mbali na Jaji Aboud, majaji wengine ni Sacko Modibo (Mali), Ben Kioko (Kenya), Rafaa Ben Achour (Tuniasia), Jaji Ntyam Ondo Mengue (Cameroon), Tujilane Chizumila (Malawi), Bensaoula Chafika (Algeria).
Wengine ni Stella Anukam (Nigeria), Blaise Tchikaya (Jamhuri ya Congo), Dumisa Ntsebeza (Afrika Kusini), Denis Adjei (Ghana).
Ghaamid Abdulbasat
Mei 11, mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulimteua Ghaamid Abdulbasat kuwa mjumbe wa Kamati ya Ushauri (IAC) kwa niaba ya vijana wa Afrika na dunia kwa ujumla, katika kutekeleza itifaki ya Nagoya ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Bioanuwai/Mazingira.
Kama mwanachama wa IAC, Abdulbasat atachangia katika maendeleo ya programu za kujenga uwezo zinazolenga kuimarisha utekelezaji wa Itifaki ya Nagoya.
Akizungumza na Mwananchi baada ya kuteuliwa, Abdulbasat alisema uteuzi huo ni fursa kwa nchi kusogea karibu na wafanya uamuzi kwa kile kilichoelezwa kuwa kwa kawaida idara ya vijana huwa inawekwa pembeni.
Abdulbasat ni balozi wa mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, pia, ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Biodiversity Organization. Amepokea tuzo mbalimbali zikiwemo za Umoja wa Mataifa katika kuhamasisha, kushirikisha na kufundisha vijana kuhusu uhifadhi na utunzaji wa mazingira tangu mwaka 2017.
Maoni ya wadau
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema manufaa makubwa ambayo nchi inayapata kwa kuwepo kwa Watanzania wanaofanya kazi kwenye taasisi za kimataifa, ni nchi kuaminika.
“Manufaa tunayopata ni ile kuaminika. Kuaminika kuna maana kubwa katika ushirikiano kwenye diplomasia ya uchumi kwa sababu kila Taifa litapenda kuchangamana au kushirikiana na sisi,” anasema Dk Loisulie.
Anaongeza kwamba hilo linaipa nafasi Tanzania kushirikishwa kwenye utatuzi wa migogoro kwenye mataifa mengine. Anasisitiza kwamba imani hiyo ndiyo inazaa ushirikiano kwenye masuala ya kisiasa, kiuchumi na jamii.
Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo anasema jina la Tanzania kwenye uwanja wa diplomasia linapiga hatua kutokana na Watanzania kupewa nafasi kwenye mashirika makubwa.
“Kwa muda mrefu watu wetu wamekuwa ni hazina kubwa kwa jumuiya ya kimataifa. Ni watu wanaoaminika kwa utendaji na wameonyesha uwezo kila wanapopata nafasi kwenye maeneo yao,” anasema mwanazoni huyo.
Akiwa na mtazamo tofauti, mchambuzi wa masuala ya siasa, Buberwa Kaiza anasema kila taasisi ya kimataifa ina misingi yake ambayo inatofautiana na ya Tanzania, hivyo kuna baadhi ya maeneo mabadiliko hayawezi kuonekana kutokana na tofauti hizo.
“Ni vigumu kueleza kama kuna faida au la kwa sababu kila taasisi ya kimataifa ina utaratibu na misingi yake na siyo lazima ifafanane na misingi ya Tanzania. Kwa hiyo manufaa binafsi ni mengi kuliko ya Taifa,” anasema Kaiza wakati akizungumza na Mwananchi.