Vituo 413 kutumika maboresho ya daftari la wapigakura Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule
Muktasari:
- Idadi ya vituo hivyo imegawanyika katika maeneo yanye mtawanyiko lakini sehemu kubwa wamelenga kwenye makao makuu ya kata, ambapo amesisitiza kuwa vituo vitafunguliwa kuanzia saa mbili asubuhi na kufungwa saa 12 jioni kwa siku zote saba.
Dodoma. Mkoa wa Dodoma umetangaza vituo 413 vitakavyotumika kwa ajili ya uboreshaji wa daftari la kudumu la mpigakura awamu ya pili , huku ikielezwa kuwa kipaumbele ni kwa makundi ya wenye ulemavu na vijana ambao wanaandikishwa kwa mara ya kwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa taarifa hiyo leo Jumatatu Mei 13, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya uboreshaji wa daftari ambayo kwa mkoa huo inatarajia kuanza Mei 16 hadi 22, 2025.
Amesema idadi ya vituo hivyo imegawanyika katika maeneo yenye mtawanyiko lakini sehemu kubwa wamelenga kwenye makao makuu ya kata, akisisitiza kuwa vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni kwa siku zote saba.
“Uboreshaji huu ni sehemu muhimu ya mchakato wa uchaguzi na unalenga kuhakikisha kuwa wapigakura wote wanahakiki taarifa zao ili waweze kutimiza haki ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu,” amesema Senyamule.
Ametaja idadi ya vituo kwa kila wilaya ambapo Dodoma Mjini itakuwa na vituo 105, Mpwapwa (67), Chemba (58), Chamwino (50), Kongwa (41), Kondoa Vijijini (44), Bahi (32) na Kondoa mji yenyewe imepangiwa vituo 16.
“Vituo hivyo vitakuwa katika ofisi za watendaji wa kata, aidha kwa kata ambazo ni kubwa utaratibu umeshafanyika vituo vimegawanywa, hivyo kutakuwa na vituo katika maeneo mengine ambayo wananchi watatangaziwa na viongozi wao wa kata, mitaa au vijiji,” amesema.
Kazi zitakazofanyika kwenye uboreshaji huo ni kuandikisha wapigakura wapya wenye umri kuanzia miaka 18, kuhakiki taarifa za wapigakura, kufanya marekebisho ya taarifa na kuweka pingamizi kwa wapigakura wasio na sifa kuendelea kuwemo kwenye daftari.
Mkoa wa Dodoma una wilaya saba, majimbo ya chaguzi 11 baada ya kuzaliwa kwa jimbo la Mtumba na mkoa mzima una kata 209.