UVCCM yahamasishana kujiandikisha kupiga kura

Baadhi ya vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM, (UVCCM), wakiwa katika mkutano baada ya matembezi ya kijani first time voters (uchaguzi kwa mara ya kwanza).
Muktasari:
- Wakati Watanzania wakiendelea na shughuli ya kujiandikisha na kuboresha taarifa zao, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umewataka vijana kuhamasishana kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.
Dodoma. Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), umewataka wapiga kura wapya kuwahamasisha vijana wengine kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ili kushiriki ipasavyo kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka 2025.
Kauli hiyo imetolewa huku kukiwa na changamoto ya idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28,2020.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, waliopiga kura waliokuwa ni watu milioni 14.8 sawa na asilimia 49.8 ya Watanzania milioni 29.8 waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura.
Akizungumza leo Jumamosi Mei 24, 2025 katika matembezi ya kijani first time voters (wapiga kura wa mara ya kwanza), Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohamed Kawaida amesema matembezi hayo yanalenga kuwaunganisha vijana ambao ni mara ya kwanza kupiga kura ili kushiriki ipasavyo kwenye uchaguzi.

Amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa kuwahimiza vijana kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu.
“Kawahamasisheni vijana wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kupiga kura katika uchaguzi mkuu. Katika zoezi hili hakikisheni kuwa mnalinda amani,” amesema.
Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi amewaasa vijana kutodhoofisha amani ya Tanzania kwa sababu haina athari kwao bali na kwa vizazi vijavyo.
“Niwaambie vijana wa kitanzania hususan Dodoma, sisi vijana wa CCM tunaamini Dodoma ni Makao Makuu ya chama na Serikali. Tukumbuke kupitia sensa ya watu na makazi sisi vijana tuna akidi kubwa twende tukajiandikishe na kupiga kura,” amesema.

Amesema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu umekidhi haja ya makundi yote na kuwakumbusha vijana ni kundi muhimu la CCM kwenye kupiga kura.
Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Nasra Mohamed Ramadhan ametoa rai kwa vijana kutunza vitambulisho vyao vya kupigia kura ili kushiriki ipasavyo katika uchaguzi mkuu mwaka huu.