UN yaonya maendeleo ya M23 kuibua mgogoro zaidi DRC Mashariki

Askari wa M23 wakipita mitaa ya Bukavu Mashariki ya DRC.
Muktasari:
- Tahadhari ya UN inakuja wakati M23 ikichukua udhibiti wa maeneo makubwa Mashariki mwa DRC, yakiwemo miji ya Goma na Bukavu.
Katika wiki za hivi karibuni, kundi la M23, linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, limechukua udhibiti wa maeneo makubwa mashariki mwa DRC, yakiwemo miji ya Goma na Bukavu.
“Taarifa tulizonazo, M23 inaendelea kusonga mbele kuelekea maeneo mengine ya kimkakati katika Kivu Kaskazini na Kivu Kusini,” amesema Huang Xia, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa UN kwa Kanda ya Maziwa Makuu, alipohutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akinukuliwa na Al Jazeera.
Ameongeza kuwa, ingawa “nia halisi ya M23 na wale wanaoiunga mkono haijulikani,” hatari ya kuzuka kwa mzozo wa kieneo ni halisi zaidi kuliko wakati wowote,” akionya kuwa mzozo huo unaweza kuwa na madhara makubwa.
Mapigano ya hivi karibuni yameongeza hofu ya kurejelewa kwa Vita vya Pili vya Congo, vilivyodumu kuanzia 1998 hadi 2003, ambavyo vilihusisha mataifa kadhaa ya Afrika na kusababisha vifo vya mamilioni ya watu kutokana na ghasia, magonjwa, na njaa.
Bintou Keita, mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani DRC (Monusco), pia ameelezea wasiwasi kuhusu kuendelea kusonga mbele kwa waasi wa M23, ambao sasa wako “katika makutano ya mipaka ya DRC, Rwanda, na Burundi.”
M23 waimarisha ulinzi Bukavu
Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameimarisha udhibiti wao mjini Bukavu, mji wa pili kwa ukubwa mashariki mwa DRC kuangukia mikononi mwao tangu mwishoni mwa mwezi uliopita.
M23 iliteka mji huo wenye wakazi milioni 1.3 Jumapili ya Februari 16, baada ya vikosi vya Serikali ya Congo kuondoka Bukavu. Mji huo, ambao ni mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kusini, upo kilomita 101 (maili 63) kusini mwa Goma, mji uliotekwa na waasi mwishoni mwa Januari.
Waasi walipoingia Bukavu, mitaa ya mji huo ilifurika wakazi waliokuwa wakikimbia, huku waporaji wakijaza magunia ya unga na bidhaa nyingine walizoweza kupata.
Baada ya muda, hali ya utulivu ilirejea huku wakazi na wafanyabiashara wakisubiri kwa tahadhari M23 kuingia katikati mwa jiji.
Asubuhi ya Jumatatu, watu walianza kutoka nje taratibu, huku waasi wakifanya doria kwenye makutano makuu ya barabara mjini humo.
Mpaka wa Bukavu na Rwanda ulifungwa asubuhi ya Jumatatu, huku maduka mengi yakibaki yamefungwa, ingawa usafiri ulianza kurejea polepole.
M23 ni kundi kubwa zaidi kati ya zaidi ya makundi 100 ya waasi yanayopigania udhibiti wa utajiri mkubwa wa madini Mashariki mwa DRC. Madini hayo ni muhimu kwa teknolojia ya kisasa duniani.
Kulingana na wataalamu wa Umoja wa Mataifa, waasi hao wanapata msaada wa takriban wanajeshi 4,000 kutoka nchi jirani ya Rwanda.
Mashambulizi ya M23 yamezua wasiwasi wa kimataifa, huku Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres, akisema kuwa “lazima kuzuka kwa vita vya kieneo kuzuiwe kwa gharama yoyote.”
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Februari 15, alitoa wito wa kusitishwa mapigano mara moja, kuondoka kwa waasi, na kurejeshwa kwa mamlaka ya Serikali ya Kongo mjini Bukavu.