Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI WA MAYALA: Uhuru wa habari unahitaji uhuru wa kiuchumi



Pesa imekuwa mhimili mkuu wa maisha ya kisasa. Kauli kwamba “hakuna tena cha bure” si kauli ya mzaha bali ni uhalisia unaojidhihirisha katika kila sekta ya uchumi na kijamii.

Katika muktadha huo, mjadala kuhusu thamani ya habari na mustakabali wa uhuru wa vyombo vya habari unahitaji kutazamwa upya kwa jicho la kiuchumi.

Hoja kwamba hakuna uhuru wa habari bila uhuru wa kiuchumi si nadharia, bali ni hitimisho linalotokana na uzoefu wa muda mrefu wa tasnia hii.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Habari yaliyofanyika kitaifa jijini Arusha yameibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya fedha katika kuimarisha sekta ya habari.

Kauli ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwamba wanahabari na vyombo vya habari wanapaswa kutafuta fedha ili kulinda uhuru wao imegusa kiini cha changamoto inayoikabili tasnia hii. Ukweli ni kwamba, bila msingi imara wa kiuchumi, uhuru wa habari hubaki kuwa nadharia isiyotekelezeka kwa vitendo.

Kauli mbiu ya mwaka huu, inayolenga kuunda mustakabali wa amani kwa kukuza uhuru wa vyombo vya habari kwa ajili ya haki za binadamu, maendeleo na usalama, inaendana moja kwa moja na hoja hii.

Hakuna amani bila haki, hakuna haki bila uhuru, na hakuna uhuru wa habari bila vyombo vya habari na wanahabari kuwa na uhuru wa kiuchumi.

Hii ni mnyororo usiovunjika unaobainisha umuhimu wa fedha katika kuhakikisha tasnia ya habari inafanya kazi yake kwa ufanisi na uadilifu.

Kwa muda mrefu, sekta ya habari imekuwa ikitegemea mifumo isiyo rasmi ya mapato, hali inayochangia kudhoofisha misingi ya taaluma. Wanahabari wengi hulazimika kufanya kazi katika mazingira magumu, bila uhakika wa kipato, jambo linalowaweka katika hatari ya kushawishika au kudhibitiwa na maslahi ya nje.

Hali hii inapunguza ubora wa habari na kuathiri uaminifu wa vyombo vya habari mbele ya umma.

Ni wazi kuwa mwanahabari asiye na uhakika wa kipato yuko katika mazingira magumu ya kufanya uamuzi huru. Anapokosa uhuru wa kiuchumi, uhuru wake wa kitaaluma huwekwa rehani.

Katika mazingira hayo, si ajabu kuona baadhi ya wanahabari wakijihusisha na upotoshaji au upendeleo, si kwa hiari bali kwa kulazimishwa na hali ya maisha.

Hivyo, hoja ya kutaka wanahabari na vyombo vya habari kutafuta na kumiliki vyanzo halali vya mapato ni ya msingi na ya lazima.

Tukiangalia historia, kulikuwa na kipindi ambapo huduma nyingi za kijamii zilikuwa bure au zinapatikana kwa gharama ndogo sana.

Elimu, afya, hata baadhi ya mahitaji ya msingi vilitolewa kwa mfumo wa kijamaa uliolenga ustawi wa wote.

Hata hivyo, mabadiliko ya kiuchumi yameleta uhalisia mpya ambao karibu kila huduma inalipiwa.

Katika mazingira hayo ni ajabu kuona kuwa habari ambayo ni nyenzo muhimu ya maendeleo na uwajibikaji bado inachukuliwa kana kwamba haina gharama.

Uzalishaji wa habari una gharama kubwa; kuanzia ukusanyaji wa taarifa, uchambuzi, uchapishaji hadi usambazaji.

Kila hatua inahitaji rasilimali fedha na watu wenye ujuzi. Ni vigumu kudumisha ubora wa habari ikiwa hakuna uwekezaji wa kutosha katika mnyororo mzima wa uzalishaji.

Hivyo basi, hoja kwamba habari zilipiwe si ya kupuuzwa bali inahitaji mjadala wa kina na utekelezaji wa sera madhubuti.

Aidha, kuna haja ya kutafakari upya mfumo wa ruzuku katika jamii. Ikiwa sekta nyingine zinapewa kipaumbele cha kifedha kwa sababu ya umuhimu wake, basi sekta ya habari nayo inastahili kuangaliwa kwa jicho hilo hilo. Vyombo vya habari vina jukumu la msingi la kuelimisha, kuhabarisha na kuhimiza uwajibikaji.

Huu ni mchango mkubwa katika kujenga taifa lenye misingi imara ya demokrasia na maendeleo endelevu.

Ni wakati sasa kwa wadau wa sekta ya habari, watunga sera na jamii kwa ujumla kukubaliana kuwa habari si bidhaa ya bure. Inahitaji uwekezaji, inaleta thamani, na inapaswa kulipiwa kwa njia inayohakikisha uendelevu wa tasnia.

Hii haimaanishi kuzuia upatikanaji wa habari kwa umma, bali ni kujenga mfumo unaowezesha uzalishaji wa habari bora, huru na yenye kuwajibika.

Kwa ujumla uhuru wa habari hauwezi kutenganishwa na uhuru wa kiuchumi.

Ili kulinda misingi ya taaluma ya uandishi wa habari, ni lazima kuwe na mikakati thabiti ya kiuchumi inayowawezesha wanahabari kufanya kazi zao bila hofu wala upendeleo.

Pesa si kila kitu, lakini katika muktadha wa tasnia ya habari ya leo, ni nguzo muhimu ya kulinda uhuru, uadilifu na ubora wa habari.