Kwa nini tunahitaji kuulinda uhuru wa vyombo vya habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limelaani kitendo cha Mamlala ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kukifungia kituo cha televisheni mtandaoni ya Jambo TV kwa muda wa siku 90 kutokana na kilichodaiwa kuwa maudhui yasiyo sahihi TEF tumesikitishwa na uamuzi huo.
Taarifa ya TEF iliyosainiwa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile imesema TEF inaamini kuwa iwapo kuna makosa ya kitaaluma yaliyofanywa na mwanahabari mmoja, basi hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya mhusika binafsi badala ya kuadhibu chombo kizima cha habari.
Kwa mtazamo wa kitaaluma, kuwajibisha taasisi nzima kwa makosa ya mtu mmoja, ni kinyume cha misingi ya haki ya kupata taarifa na uhuru wa vyombo vya habari.
Balile amesema hatua hiyo, ambayo haikutokana na uamuzi wa Mahakama, ndiyo imekuwa malalamiko yetu ya muda mrefu kwa hivi vyombo vinavyoundwa vikachukua nafasi ya Mahakama kinyume cha Ibara ya 107 ya Katiba ya Jamhuri Muungano wa Tanzania.
Amesisitiza kwamba hiyo siyo sahihi. Uamuzi huo si tu unaathiri uhuru wa vyombo vya habari na kuiweka Tanzania miongoni mwa mataifa yasiyo na uvumilivu wa haki ya kupata habari, bali pia inazuia haki ya umma kupata taarifa na kudhoofisha maendeleo ya taaluma ya habari nchini.
Balile ametolea mfano lile tukio la Novemba Mosi, 2007 katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), lilitokea kosa la kitaaluma kwa daktari kufanya upasuaji wa goti badala ya kichwa na upasuaji wa kichwa badala ya goti, lakini hawakusikia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ikifungiwa, bali wahusika binafsi waliwajibishwa.
Kwa msingi huo, TEF inaamini kuwa makosa ya kitaaluma yanapaswa kushughulikiwa kitaauma badala ya fungiafungia ya vyombo vya habari na kuharibu heshima ya Taifa katika uhuru wa vyombo vya habari. TEF inaamini kuwa kufungia chombo cha habari ni adhabu inayowaathiri wananchi kwa kuwakosesha habari.
Hatua hii sio tu itaathiri wananchi kupata uchambuzi mahiri wa habari, unaofanywa na wachambuzi mahiri, wabobezi na wabobevu, hatua hiyo itawaathiri wafanyakazi wote wa Jambo TV, ambao wanaitegemea Jambo TV kuendesha maisha yao.
Jambo TV ina vipindi vingii, ikiwa ndio TV inayoongoza kwa kurusha matangazo ya moja kwa moja (Mubashara) kuliko TV zote za mtandaoni hapa Tanzania, mfano kama sio Jambo TV kurusha Live mkutano wa Tundu Lisu, serikali isingekuwa na ushahidi wowote wa kauli ya “tutakinukisha”.
Jambo TV ndiyo TV pekee iliyorekodi tukio hilo na serikali ilipoomba video hizo, Jambo TV ilikubali na kuwapa bure, ningekuwa mimi ndio mkurugenzi wa Jambo TV, ningewalipisha mamilioni ya kutosha kuwapa video za ushahidi huo, huu ni uthibitisho Jambo TV imetanguliza mbele maslahi ya umma.
Kwa kuzingatia msingi huo, TEF itafanya mazungumzo ya kitaaluma kati ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, TCRA, Jambo TV na mwandishi husika ili kumaliza kadhia hii. TEF inalenga kulinda maslahi ya Taifa, taaluma ya habari, na hadhira ya ndani na nje ya nchi inayoshuhudia minyukano.
Hiki kinachofanywa na TCRA kuvifungia vyombo vya habari vya utangazaji, kwa tuhuma za kufanya makosa mbalimbali, si sawa, uamuzi wa TCRA kufungia vyombo vya utangazaji kwa sababu zozote zile, sio uamuzi wa haki, kwa sababu TCRA hawezi yeye kuwa ndiye mshitaki, kisha kugeuka ndie hakimu wa kusikiliza kesi, na baada ya hukumu anageuka bwana jela kufungia media.
Kama kuna kipindi kimoja kimefanya kosa, kipindi hicho ndio kinasitishwa, huwezi kufungia matangazo ya vipindi vyote vya TV kwa kosa la kipindi kimoja.
Hivi karibuni, TCRA walianza na kuifungia Jamii Forums kwa kosa la kuchapisha picha za lile Bonge la Zimbabwe likionekana limekuja nchini mara kadhaa na kupiga picha tano tofauti tofauti likiwa na mmoja wa viongozi wetu tena wakiwa ndani ya patakatifu petu, tena picha nyingine zikiwa si za heshima.
Wachangiaji wa JamiiForums, wakauliza hili bonge linakuja kufanya nini? TCRA ilichukua uamuzi huo wakati hakuna mtu yoyote aliyelalamika kukashifiwa.
Hapa naomba kwanza kutangaza maslahi, mimi ni mtangazaji na mchambuzi wa Jambo TV, hivyo naomba andiko hili lisichukuliwe kuwa nalalamika kwa sababu nimeguswa.
Katika moja ya mijadala yetu ya nyuma, niliwahi kusema kiongozi fulahi hakufurahishwa na kushangiliwa kwa viongozi wastaafu, hakuna mtu aliyelalamika kukashifiwa, lakini tukaitwa kuhojiwa na Bodi ya Ithbati ya Waandishi wa Habari (JAB) na kupewa onyo kisha TCRA ikaishukia Jambo TV.
Sasa tena, kwa mujibu wa Kifungu cha 114 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura 306, TCRA imesitisha kwa muda wa siku 90 leseni ya maudhui mtandaoni ya Jambo Online TV katika chaneli na akaunti zake zote za mtandaoni kwa tuhuma ya kuchapisha maudhui ambayo hawakuwa na uhakika nayo na yasiyo na uthibitisho.
Maudhui hayo, pia, yaliupotosha umma kuhusu hali ya matukio mbalimbali yanayoendelea nchini na matokeo yanayotarajiwa kutoka kwa Tume ya kuchunguza matukio wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, kinyume na Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020.
Sisi waandishi na uwezo wa media, ni kuandika tu na kupiga kelele, kama kuandika tumeandika sana kuhusu kuheshimiwa kwa ibara ya 18 ya Katiba ili media tutendewe haki ni tusiishie kuandika tuu na kupiga kelele, lazima sasa tuchukue hatua.
Mungu Ibariki Tanzania.