Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAGUZI MKUU 2025: Sababu za Kunje kuitaka Ikulu, kuwatumikia Watanzania

Walioinua mikono, Mgombe Urais wa AAFP, Kunje Ngombale-Mwiru wa kwanza kulia, Katibu Mkuu Rashid Rai na Mgombea Mwenza, Chuma Juma Abdallah kushoto wakitambulishwa kwa umma.

Muktasari:

  • Mgombea urais kwa tiketi ya AAFP, Kunje Ngombale-Mwiru atambulishwa rasmi kwa umma akieleza azma yake na atakachoanza kuwafanyia Watanzania punde baada ya kushinda dola.

Dar es Salaam. Mgombea urais wa Tanzania, kwa tiketi ya Chama cha AAFP, Kunje Ngombale-Mwiru amesema kiu ya Watanzania kuwa na maendeleo ya kubadilisha maisha yao na itatimia baada ya chama hicho kushinda dola nay eye kuingia ikulu Oktoba 2025.

Mteule huyo anayesubiri uteuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kabla ya kuingia kwenye kinyang'anyiro cha urais kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, atakiwakilisha chama hicho huku mgombea mwenza wake akiwa Chuma Juma Abdallah.

Kunje ambaye aliwahi kugombea nafasi ya uspika wa Bunge la Tanzania, alichaguliwa kwa kura 70 kati ya 97 zilizopigwa na wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa chama hicho, uliofanyika Temeke Dar es Salaam, ambao hata hivyo haukufanikiwa kupata mgombea urais Zanzibar.

Walikosa mgombea baada ya aliyekuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo, Said Said Soud kupigiwa kura nyingi za hapana, hivyo chama hicho kutakiwa kuandaa mkutano mwingine kwa kuzingatia katiba yake, ili wapate mgombea urais wa Zanzibar.

Hatua hiyo, inaifanya AAFP iungane na vyama vya CCM, SAU, UPDP, NLD na NCCR- Mageuzi ambavyo vilishateua wagombea wake.

Vyama vingine viko kwenye hatua za mwisho kukamilisha hatua hiyo, ikiwemo ACT – Wazalendo, CUF, ADC na Chaumma.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Mei 4, 2025 kwenye hafla ya kutambulishwa kwa umma, Kunje amesema ili Watanzania waifikie kiu ya ndoto ya maisha hayo mabadiliko ya haraka na kasi yanahitajika.

"Tunachukua dola Oktoba mwaka huu baada ya uchaguzi, kama mgombea najua naikaribia Ikulu lakini kama haitoshi najua kiu ya Watanzania ni kupata maendeleo ya kubadilisha maisha yao. Niwahakikishie na kuwaondoa hofu Watanzania wasiwe na wasiwasi, chama hiki kipo kwa ajili ya mbadiliko ya lazima na si hiyari," amesema Kunje.

Kunje amesema baada ya kuapishwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, Serikali atakayoiunda itakuwa ya mchakamchaka na si ya kukaa na kubweteka ofisini, ili kukidhi haja ya kiu ya Watanzania ya kubadilisha maisha yao.

"Watanzania wanahitaji mabadiliko kila sekta ya nchi hii, nitaunda Serikali ya mchakamchaka itakayokuwa inafanya kazi saa 24, kuyafikia mabadiliko ya lazima,

"Tumejipanga tutaenda kwenye uchaguzi tukiwa na sera nzuri ya kuleta mabadiliko ya wananchi ambayo yote yatabainishwa kupitia ilani ya chama chetu, siwezi kumwaga mchele kwenye kuku wengi, maana itazinduliwa na kutangazwa hadharani siku za usoni," amesema Kunje.

Walioinua mikono, Mgombe Urais wa AAFP, Kunje Ngombale-Mwiru wa kwanza kulia, Katibu Mkuu Rashid Rai na Mgombea Mwenza, Chuma Juma Abdallah kushoto wakitambulishwa kwa umma.

Sababu za kugombea

Kunje ambaye ni mtoto wa marehemu Kingunge Ngombale-Mwiru, ametaja sababu kuitafuta nafasi hiyo ni baada ya kuangalia wagombea waliopatikana na vyama vingine ambayo haviwajapata, hakuna mgombea atakayekuwa na sera bora na zinazokubalika na umma kama za chama hicho.

"Pili nina imani na refarii, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, atatenda haki licha ya na baadhi kuwa na wasiwas. AAFP tuna matumaini makubwa na tumejipanga, unajua ukifanya vizuri hata kama watakuwa na nia ya kutaka kuiba wataona aibu," amesema Kunje.

Tatu, Kunje ametaja msingi wa chama hicho kuanzia kwa wakulima, sekta inayojumuisha Watanzania wengi ambao wanashiriki shughuli ya kupiga kura, hivyo hawatamwangusha.

"Nikiingia Ikulu siku ya kwanza na mipango yangu itakuwa kuanza kuboresha mawasiliano, miundombinu ya barabara ifikike kila eneo linaloweza kuchochea ukuaji uchumi," amesema.

Kwa upande wake, Mgombea Mwenza, Chuma Juma Abdallah amesema hawahofii ushindani kutoka chama chochote kitakachoweka wagombea katika uchaguzi huo.

"Tuna sera bora, tutaenda kuifafanua kwa Watanzania kupitia majukwaa ya kisiasa, kikubwa tunaomba mshikamano kwa Watanzania, kufikia nchi ya neema inawezekana," amesema Abdallah.

Naye, Katibu Mkuu wa AAFP, Rashid Rai amesema Kunje ni mgombea wao wa urais ameandaliwa na amepikwa na wamempitisha hivyo wapo tayari kusimama naye kwenye majukwaa kumuuza katika uchaguzi mkuu.

"Tuna matumaini makubwa naye, alichaguliwa na wajumbe wengi katika mkutano mkuu Maalumu, tunaamini tunawasogezea dhahabu isiyo na doa,  kazi kwao. Nawasihi wasikosee, wampigie kura, kijana huyu ni mzalendo na mwenye wivu mkubwa na kuona nchi yake inapiga hatua," amesema Rai.

Katika hatua nyingine Rai amesema mkutano wa kumpatam urais upande wa Zanzibar utajulikana baada ya uongozi wa chama hicho, kuketi kikao cha ndani Mei 16, 2025.