Trump acharuka, amtaka Putin kusitisha mashambulizi Ukraine

Muktasari:
- Ni kauli za nadra kutolewa hadharani, Rais wa Marekani, Donald Trump amemtaka Rais wa Russia, Vladimir Putin kukomesha mashambulizi yake nchini Ukraine.
Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump amemkosoa vikali Rais wa Russia, Vladimir Putin huku akimtaka kusitisha mashambulizi dhidi ya Ukraine.
Aprili 24, 2025, Rais Trump kupitia mtandao wa Truth Social aliandika: “Rais Vladimir Putin, sifurahishwi na unachokifanya. Ukome kuishambulia Ukraine.”
Baadaye, akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Norway, Trump amesema hafurahishwi na kinachofanywa na Russia.
“Sifurahishwi na mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukraine. Hayakuwa ya lazima na muda wake ni mbaya sana. Vladimir, Ukome! Wanajeshi 5,000 wanakufa kila wiki,” aliandika Trump kupitia ukurasa wake wa Truth Social.
Russia jana iliendesha mashambulizi mazito jijini Kyiv, Ukraine kwa makombora na ndege zisizo na rubani (droni) kwa saa kadhaa.

Katika taarifa yake kwa umma, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema takriban watu 12 waliuawa katika mashambulizi hayo na wengine 90 kujeruhiwa. Shambulizi hilo linatajwa kuwa hatari zaidi kufanywa na Russia nchini Ukraine tangu Julai, 2024.
Hasira za Trump zinaongezeka kadri juhudi zinazoongozwa na Marekani kufanikisha makubaliano ya amani kati ya Ukraine na Russia zinavyochelewa.
Matamshi kuhusu Putin yalikuja baada ya Trump kumshambulia Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, Jumatano akimtuhumu kwa kuendeleza mapigano ambayo anadai yanagharimu maisha ya raia na maelfu ya wanajeshi.
Rais Trump ameenda mbali na kuitaka Ukraine kukubaliana na takwa la Russia la kukabidhiwa mikoa ya Donetsk, Lugansk, Kherson, Zaporizhia na Pokrovisk ambayo hadi sasa vikosi vyake vinaikalia kimabavu tangu uvamizi wa Februari 2022 na Crimea iliyotwaliwa tangu 2014.
Trump amesema Putin alifanya shambulio kwa wakati mbaya huku akiongeza kuwa kiongozi huyo wa Russia anajidhuru mwenyewe katika juhudi za kupata masharti ya Kremlin kwamba, makubaliano ya amani yamruhusu Russia kuendelea kuimiliki Crimea na maeneo mengine ya Ukraine.
Baadaye, wakati wa kikao katika Ofisi ya Oval na Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Støre, Trump amesema kuwa Crimea ilichukuliwa kutoka Ukraine bila mapigano.

Pia amebainisha kuwa uvamizi huo wa rasi ya Bahari Nyeusi ulifanyika chini ya uongozi wa Rais Barack Obama na si wakati wa utawala wake.
Alipoulizwa kuhusu kile ambacho Putin anafanya kwa sasa kusaidia kufanikisha makubaliano ya amani, Trump amejibu: “Kuacha kuchukua nchi nzima, hiyo ni ustahimilivu mkubwa.”
Lakini, wazo hilo limepingwa vikali na Ukraine na sehemu kubwa ya Ulaya, wakisema Russia kusitisha kuteka ardhi si jambo la kweli badala yake imeendelea kujitanua.
Hata hivyo, Rais Zelenskyy amesisitiza mara kadhaa kuwa kutambua maeneo yaliyokaliwa kuwa ya Russia kuongeza hatari zaidi kwa Ukraine kuendelea kuvamiwa.
Zelensky amesema Ukraine ilikubali pendekezo la Marekani la usitishaji mapigano siku 44 zilizopita kama hatua ya kwanza ya kuelekea mazungumzo ya amani, lakini mashambulizi ya Moscow yameendelea.
Ukosoaji wa Trump dhidi ya Putin ni wa kipekee, kwani awali amesema mara kadhaa kwamba, Russia iko tayari zaidi kuliko Ukraine kufanikisha makubaliano.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.