Shambulizi la Russia laua 18 Ukraine, wamo watoto tisa

Muktasari:
- Mamlaka nchini Ukraine zimesema watu wasiopungua 50 wamejeruhiwa huku 18 wakiuawa katika shambulizi la Russia lililolenga Mji wa Kryvyi Rih katikati mwa nchi hiyo jana Ijumaa.
Kyiv. Mamlaka nchini Ukraine zinasema watu wasiopungua 18, wakiwemo watoto tisa, wameuawa katika shambulio la kombora la Russia kwenye eneo la makazi katika mji wa Kryvyi Rih uliopo katikati ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa mamlaka za Ukraine, shambulizi hilo lililotekelezwa jana jioni ni miongoni mwa mashambulizi mabaya zaidi kutekelezwa katika ardhi ya Ukraine tangu Russia itangaze kuanza operesheni yake ya kijeshi Februari 2022.
Al Jazeera imeripoti kuwa shambulio hilo la Ijumaa katika mji aliozaliwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, limefanyika wakati Rais wa Marekani, Donald Trump anasukuma mbele mpango wa kusitisha vita hiyo, na linatajwa kuwa limeharibu vibaya majengo ya makazi na kusababisha moto.
Gavana wa Mkoa wa Dnipropetrovsk, Serhiy Lysak aliandika katika mtandao wa Telegram, kuwa miili ya waliouawa na majeruhi ilionekana ikiwa imetapakaa barabarani, mmoja wao karibu na uwanja wa michezo wa watoto, katika video ambazo hazijathibitishwa zilizokuwa zikisambaa kwenye Telegram huku moshi mweusi ukitanda angani.
Taasisi za kutoa huduma za dharura nchini humo zilisema watu wasiopungua 50 walijeruhiwa, na kuongeza kuwa idadi hiyo inaendelea kuongezeka.
Kwa mujibu wa Lysak, zaidi ya watu 30, wakiwemo mtoto mchanga wa miezi mitatu, walilazwa hospitalini.
Mlinzi wa haki za binadamu wa Ukraine, Dmytro Lubinets alisema Jeshi la Russia lilitumia kombora la ‘Balistiki’ katika shambulio hilo.
Silaha kama hizo huchukua dakika chache tu kufikia malengo na ni vigumu kuzikabili isipokuwa kwa mifumo ya juu kabisa ya ulinzi wa anga.
“Hakukuwa na kituo hata kimoja cha kijeshi ni miundombinu ya kiraia tu,” Lubinets aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa Telegram.
Wizara ya Ulinzi ya Russia ilisema ilikuwa imelenga mkusanyiko wa wanajeshi wa Ukraine na wakufunzi wa kigeni katika mji huo.
Zelenskyy alisema Ijumaa kuwa juhudi za uokoaji zilikuwa zinaendelea huku akizitaka nchi za Magharibi kuongeza shinikizo dhidi ya Russia ili kudhibiti mashambulizi hayo.
“Ulimwengu mzima unaliona hili. Kila kombora, kila drone ya shambulio linathibitisha kuwa Russia inataka vita tu,” aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa Telegram.
Awali, Russia ilianzisha mashambulizi ya usiku kwa kutumia ndege zisizo na rubani (droni), na kuua watu wasiopungua wanne na kujeruhi 35 katika mji wa Kaskazini Mashariki wa Kharkiv.
Katika shambulio la nne la aina hiyo wiki hii katika mji huo, drone za Russia zililenga maeneo ya makazi, zikiharibu majengo kadhaa ya ghorofa na kusababisha miali ya moto.
Zelenskyy pia alisema Russia ilishambulia kwa kutumia ‘droni’ kituo cha kuzalisha umeme wa joto katika mji wa Kherson kusini, akilaumu kukiukwa makubaliano ya maridhiano yaliyoongozwa na Marekani ya kutoshambulia miundombinu ya nishati.
Baadaye Ijumaa, drone za Russia zilifanya tena shambulio kubwa dhidi ya Kryvyi Rih, maofisa wa eneo walisema, na kuongeza kuwa mashambulio hayo yalisababisha moto katika maeneo manne tofauti ya mji huo.
Marekani ilisema wiki iliyopita kuwa imekubaliana na Russia na Ukraine kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya kila upande, hatua ya kwanza ya aina yake tangu Trump aingie madarakani Januari.
Pande zote mbili tangu wakati huo zimekuwa zikituhumiana kwa kukiuka makubaliano hayo.
Kyiv ilisema ilikubali mapendekezo ya Marekani ya kusitisha vita kwa siku 30 bila masharti yoyote, lakini Russia ikakataa hatua hiyo katika mazungumzo tofauti na maofisa wa Marekani.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.