Suzan Kiwanga, vigogo wengine watatu waondoka Chadema

Suzan Kiwanga akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wake wa kuondoka Chadema. Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Mbali na Suzan Kiwanga, wengine walioondoka Chadema ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Kilosa, David Chiduo, aliyewahi kuwa Diwani wa Kata ya Viwanja Sitini na Mwenyekiti wa Bawacha Wilaya ya Kilombero, Magreth Lipindi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bawacha Wilaya ya Kilosa, Sheila Mkubwa.
Morogoro. Viongozi wanne wa Chadema kutoka wilaya za Kilosa, Kilombero na Halmashauri ya Mlimba, mkoani Morogoro na wanachama wengine 50, wametangaza kujivua uanachama wa chama hicho.
Wamesema wamefikia uamuzi huo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo msimamo wa chama wa kutoshiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Viongozi wa Chadema walioondoka ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mlimba na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) Wilaya ya Kilombero, Suzan Kiwanga, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) Wilaya ya Kilosa, David Chiduo, aliyewahi kuwa Diwani wa Kata ya Viwanja Sitini na Mwenyekiti wa Bawacha Wilaya ya Kilombero, Magreth Lipindi na Sheila Mluba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bawacha Wilaya ya Kilosa.
Wakitangaza uamuzi wao wa kuondoka Chadema katika kikao na waandishi wa habari leo, Mei 13, 2025 viongozi hao wamesema licha ya kukitumikia chama hicho kwa miaka mingi yenye changamoto ikiwemo kukamatwa, kufungwa, na kuzurura maeneo mbalimbali ya nchi wakikijenga, “kwa sasa hatuoni tena sababu ya kuendelea kubaki ndani ya chama hicho kutokana na mwenendo wa baadhi ya viongozi na wanachama.”
Kiwanga amedai kuwa tangu uchaguzi mkuu wa Chadema ulipomalizika Januari 21, amekuwa akipokea jumbe za matusi na kejeli kupitia simu yake kutoka kwa baadhi ya viongozi na wanachama wa chama hicho, wakimtuhumu kuwa msaliti kwa kushindwa kumuunga mkono Mwenyekiti aliyechaguliwa, Tundu Lissu.
“Baada ya uchaguzi ule ambao uliwaacha baadhi ya wanachama, viongozi na majeraha, pia uchaguzi uliogubikwa na changamoto na kasoro mbalimbali, nilitarajia kuwa mwenyekiti aliyechaguliwa, Tundu Lissu, angechukua hatua ya kutuita na kutuunganisha ili tuwe na mshikamano kama chama.”
"Lakini cha kushangaza, hakufanya hivyo. Badala yake, alitangaza msimamo wa chama kutoshiriki uchaguzi mkuu kwa lengo la kushinikiza mabadiliko, akiwasilisha kaulimbiu ya ‘No reforms, no election’," amesema Kiwanga.
Ameongeza: "Kauli na msimamo wa 'No reforms, no election' tafsiri yake ni kwamba Chadema haitashiriki uchaguzi wowote hadi pale mabadiliko yatakapofanyika.
“Mimi binafsi siwezi, wala siko tayari, kukubaliana na uamuzi huo wa Lissu. Lengo la chama chochote cha siasa ni kushika dola hiki si chama cha ngoma, upatu, wala kikoba, bali ni chama cha siasa.
"Kama hatutashiriki uchaguzi, hatutakuwa na wagombea wa ubunge, udiwani, wala urais. Na tunapouliza au kuhoji kuhusu uamuzi huu, tunawekewa alama ya usaliti na kuitwa 'timu Mbowe' kana kwamba kuwa na mtazamo tofauti ni kosa."
Kiwanga amesema yeye ni mtu mzima na mkongwe wa siasa na mtu aliyekipigania chama, hayuko tayari kuona anadhalilishwa, anatukanwa na kushambuliwa huku viongozi wakiwa kimya.
Akizungumzia mwelekeo wake wa kisiasa baada ya kuondoka Chadema Kiwanga amesema kwa sasa yuko kwenye kutafakari chama ambacho anaweza kwenda, hata hivyo amesema hafikirii na haitatokea kuhamia CCM, japokuwa wapo baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM wamemshauri akajiunge na chama hicho.
"Wapo viongozi na wanachama wa CCM wananipigia simu na kunitumia ujumbe wa kunishauri kuelekea CCM. Mimi nasema siwezi kwenda huko, kitu ambacho wananchi hasa wa Mlimba wanapaswa kujua ni kwamba nimetia nia na leo hii natangaza rasmi kuwa nitagombea ubunge wa Jimbo la Mlimba kupitia chama ambacho nitaona kinanifaa kunadi sera zangu na sio CCM.
Naye David Chiduo amesema amefikia uamuzi wake wa kuondoka Chadema kutokana na mwelekeo wa chama hicho kwa sasa, ambao malengo ya chama yamepotea na kimekuwa na watu wasiokuwa na uchungu nacho.
Chiduo amesema yeye kama kijana mwenye umri mdogo na mwenye maono hawezi kuendelea kubaki Chadema katika mwelekeo uliopo sasa, kwani binafsi alijiunga nacho kwa lengo la kuisaidia jamii ya wana Kilosa, lakini kwa sasa hawezi kutimiza lengo hilo kwa kuwa chama alichokuwa akikitumia kama jukwaa hakishiriki uchaguzi.
"Ni kweli tunahitaji mabadiliko ya katiba na mifumo yote ya uchaguzi, lakini kama tulishindwa kubadilisha kwa zaidi ya miaka 30 itawezekana vipi tufanye mabadiliko kwa miezi hii minne iliyobaki,” amedai.
Chiduo ameahidi na kutangaza nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Kilosa kupitia chama ambacho ataelekea baada ya kuondoka Chadema.
Kwa upande aliyekuwa diwani wa Kata ya Viwanja Sitini na mwenyekiti wa Bawacha wilaya ya Kilombero Magreth Lipindi amesema kama kiongozi ambaye aliweza kuipigania Chadema na kuhakikisha Kilombero inakuwa ngome ya Chadema, hawezi kukubali kutukanwa na kudhalilishwa na watu wachache.
"Mimi nilijiunga na Chadema mwaka 2013 na pamoja na nafasi mbalimbali za kichama, lakini pia niliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara,” amesema.