Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sugu anavyotoa somo la siasa za kizalendo akiwa Marekani

Februari 28, 2025, Mwenyekiti wa Cha cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi “Sugu”, aliposti picha kwenye akaunti yake ya Instagram. Picha hizo, alikuwa yeye na watu wengine, mmojawapo ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai.

Wengine katika picha hizo ni watu wasio na asili ya Afrika, halafu yupo pia msaidizi wa Sugu, Abraham Mwakabaga. Katika picha hizo, Sugu aliandika: “Mapema leo baada ya kikao changu na maofisa waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ambacho kilifanyika hapa Washington DC.”

Machi 4, 2025, Sugu aliposti picha mnato na video, akiwa na viongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara wa jiji la Winston Salem, jimbo la North Carolina.

Aliandika: “Mimi na jopo langu, tumekuwa na kikao na kikao kizuri cha biashara na wajasiriamali Weusi (Black Enterpreneurs) wa jiji la Winston Salem, jimbo la North Carolina.”

Katika video ambayo Sugu aliposti, inamwonesha akizungumza na wafanyabishara watatu wenye asili ya Afrika.

Mazungumzo yanasikika Sugu akiwajibu wafanyabiashara hao kutozitazama Ghana na Nigeria peke yake, akachukua nafasi hiyo kuwaalika kuwekeza Afrika Mashariki, hususan Tanzania.

“Tunajua kila mtu anakwenda Ghana, kila mtu anakwenda Nigeria. Ndiyo maana tupo hapa sasa kualika kila mtu aje Afrika Mashariki, kila mtu aje Tanzania,” anasikika Sugu akiwashawishi wafanyabiashara hao ambao kwa sehemu kubwa inaonekana wana taarifa za uwekezaje Afrika Magharibi, na siyo Afrika Mashariki.

Kisha tena, Sugu aliposti video ikionesha anavyotambulishwa na Meya wa Jiji la High Point, Cyril Jefferson, kwa madiwani wa baraza la jiji hilo. Meya Jefferson wakati akisoma utambulisho wa Sugu kwa madiwani wa High Point, alisema:

“Tunakupongeza kwa juhudi zako za kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Marekani kupitia mazungumzo kuhusu utawala, biashara na uwekezaji.”

Meya Jefferson pia alisema, Tanzania na Afrika Mashariki kuna fursa kubwa kwa sasa za ushirikiano katika maeneo ya kilimo, miundombinu na huduma za kifedha. Bila shaka, hayo ni mambo ambayo Sugu aliyafungua kumweleza Meya Jefferson, ndiyo maana naye akawasomea wadiwani.

Anachokifanya Sugu akiwa Marekani, kinanielekeza kwenye andiko la Frank de Roose, kutoka Taasisi ya European University (EUI), lenye kichwa “Politics of Patriotism” - “Siasa za Uzalendo”. Roose ameweza kujenga hoja kuhusu siasa za utaifa (politics of nationalism) na kwa nini siasa za uzalendo ndiyo muhimu zaidi.

Mantiki ni kuwa siasa za uzalendo zinaelekeza kutanguliza mbele masilahi ya nchi au eneo asilia.

Sugu, kiongozi wa Chadema, hasikiki akilalamikia matatizo ya nchi yake kisiasa, badala yake anashawishi wafanyabiashara wa Marekani, kuona fursa Afrika Mashariki, hususan ndani ya Tanzania yake.

Katika video akiwa na wajasiriamali wa Winston Salem, North Cartolina, inaonekana Wamarekani hao Weusi wana shauku ya kujua kuhusu biashara ya mali zisizohamishika (real estate), yaani ardhi na majengo. Sugu anawajibu: “Real estate ni biashara inayokuwa kwa kasi kubwa Tanzania.”

Mwanasiasa aliyebarikiwa ni yule ambaye huchagua maneno kulingana na muda au mahali. Ziara ya Sugu Marekani, japo yeye siyo kiongozi wa Serikali wala haonekani kubeba maagizo ya chama chake (Chadema), lakini manufaa yake ni makubwa.

Sugu anazungumza ustawi wa nchi kibiashara na kiuchumi. Anajenga ushawishi wa kuunganisha fursa baina ya Tanzania na Marekani. Hizo ndiyo siasa za kizalendo.

Inafahamika kuwa Sugu ni mfanyabiashara katika kofia nyingine. Katika ziara yake Marekani, haonekani kuwa amekwenda kujadili fursa zake kibiashara, bali kushawishi uwekezaji Tanzania, vilevile kuwaonesha Wamarekani fursa za ushirikiano wa kibiashara zilizopo ili wazichangamkie.

Anachokifanya Sugu, kwa rekodi za wazi, ni mwanasiasa wa kwanza wa upinzani, kuwahi kufanya hivyo. Ongeza kwamba Sugu kwa sasa siyo mbunge.

Nani ambaye bila ubunge, halafu wa chama cha upinzani, amewahi kufanya ziara kama ambayo Sugu anaendelea nayo Marekani?

Inawezekana alipokuwa na maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, walizungumza siasa, lakini sehemu nyingi ambazo anatembelea, Sugu anazungumzia fursa na mazingira mazuri ya uwekezaji Tanzania. Sugu ni mwanasiasa mzalendo. Anaipenda Afrika Mashariki, ana mapenzi makubwa na Tanzania.

Jambo lingine la muhimu ni nguvu ya mtandao. Ziara ya Sugu Marekani, inampambanua kuwa mwanasiasa na mfanyabiashara ambaye ana mtandao mpana unaomuunganisha.

Haitokei tu mwanasiasa asiye mbunge au mfanyabiashara wa kati mithili ya Sugu kuzuru makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje Marekani, Washington DC, bali kulikuwa na mipango.

Anachokifanya Sugu, ndani ya Serikali ya Tanzania, kuna watu ndiyo kazi yao, lakini pengine hawana maarifa au wamekosa ubunifu, inawezekana mitandao haifiki mbali.

Sugu anathibitisha kwamba siyo mpaka uwe mbunge au waziri, ndiyo uisaidie nchi. Unaweza kuwa kiongozi kwenye nchi bila cheo. Sugu ni kiongozi wa kitaifa bila cheo.