Sugu akumbuka miaka saba ya mateso, kukaa jela
Muktasari:
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) amesema amepitia kipindi kigumu na kukaa jela kisa kuikataa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mbeya. Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) amesema amepitia kipindi kigumu na kukaa jela kisa kuikataa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Sugu amesema leo Jumamosi Februari 25, 2023 wakati wa ufunguzi wa mikutano ya hadhara Kanda ya Nyasa ambao umefunguliwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe katika viwanja vya Ruanda Nzovwe Jijini Mbeya.
Amesema kuwa ole wao wanaosema CCM haiwezi kuachia dola, kuna mawili, waachie kistaarabu au wang'olewe kwa nguvu ya umma kwani wanashindwa kuwatumikia wananchi.
“Halafu hawa wananiita mimi yoyo, niliwapiga chini vipindi viwili sasa wamekuja kupora uchaguzi na kushindwa kujiongoza, hiyo ni sawa na ndoa ya mkeka,”amesema.
Sugu amezungumzia mradi wa maji Mto Kiwira na barabara njia nne amedai kuwa ni maombi yao Chadema ambayo walivutana bungeni kwa kipindi kirefu huku akimtaja Dk Mery Mwanjelwa kama shahidi.
“Nikiwa mbunge suala la barabara njia nne nakumbuka nikiwa bungeni wananchi walivunjiwa nyumba kwa lengo la kuleta maendeleo ambayo yamepiganiwa kwa kipindi cha miaka 10.
“Ucheleweshwaji wa miradi mikubwa kwa Mkoa wa Mbeya ilishindwa kutekelezwa kwa wakati ni kutokana na chuki na wana kila sababu ya kuishukuru Serikali ya mama Samia Suluhu Hassan,”amesema.
“Naye Waziri wa Maji anakuja kutudanganya kuhusiana na mradi wa maji, mimi sitaki kuwa Spika, nahitaji kuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini,”amesema.
Sugu amesema kuiondoa CCM madarakani ni muhimu na hakuna atakayeweza kuwadanganya, mimi baada ya kuzindua mikutano naanza kupita kwa nyumba kwa nyumba,”amesema.