Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Starmer anang’oka uwaziri mkuu, zinawadia zama mpya za siasa UK

Muktasari:

  • Starmer amebainisha mchakato wa kumpata atakayempokea kijiti, kwamba Julai 9, 2026, uteuzi wa kumpata kiongozi wa Labour utaanza, ili wenye nia ya kuwania uongozi wa chama hicho kuchukua fomu. Julai 16, dirisha la uteuzi wa wagombea litafungwa.



Haijatimia hata miaka miwili tangu, Keir Starmer, alipokiongoza Chama cha Labour, kushinda uchaguzi UK (United Kingdom) na kupata ridhaa ya kuongoza serikali.

Starmer kwa nafasi yake ya kiongozi wa Labour, akathibitishwa na Mfalme Charles III, kuwa Waziri Mkuu.

Ulikuwa umepita muongo mmoja na miaka minne, Labour kikiwa chama kikuu cha upinzani, tangu anguko la chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu Mei 6 2010.

Labour iliingia kwenye uchaguzi ikiongozwa na Gordon Brown, ambaye ndiye waziri mkuu wa mwisho wa Labour, kabla ya Starmer.

Baada ya Brown, zilifuata zama za utawala wa Conservative. Waziri Mkuu wa kwanza wa Conservative baada anguko la Labour Mei 2010, alikuwa David Cameron, akafuata Theresa May, akaingia Boris Johnson, kisha Liz Truss, halafu Rishi Sunak aliyekabidhi kijiti kwa Starmer, na kuirejesha Conservative kwenye dawati la kupinga na kukosoa.

Pamoja na kushinda uchaguzi Julai, 2024 na kutoa hotuba iliyowasisimua wafuasi wa Labour, kwamba alikuwa akianza safari ya kurejesha zama za misuli mikubwa ya chama hicho, hali ilibadilika ghafla.

Mara Starmer akapoteza umaarufu. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika Mei 2026, ukawa pigo. Presha ikawa kubwa ndani ya Labour.

“Swali ambalo chama changu kinauliza sasa ni kama mimi ni mtu sahihi zaidi kukiongoza kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Nimelisikia jibu la kambi ya chama changu bungeni kuhusu swali hilo, nalipokea jibu hilo kwa neema,” Starmer aliviambia vyombo vya habari, Jumatatu, Juni 22, 2026, nje ya kasri la Waziri Mkuu wa UK, Mtaa wa 10 Downing “Namba 10”.

Hayo ni sehemu ya maneno ya Starmer, katika taarifa yake ya kujiuzulu. Starmer amebainisha mchakato wa kumpata atakayempokea kijiti, kwamba Julai 9, 2026, uteuzi wa kumpata kiongozi wa Labour utaanza, ili wenye nia ya kuwania uongozi wa chama hicho kuchukua fomu. Julai 16, dirisha la uteuzi wa wagombea litafungwa.

Kiongozi wa Labour atapatikana mwishoni mwa Agosti (mwishoni mwa majira ya joto). Bunge la UK litakaporejea kwenye vikao vyake Septemba Mosi, 2026, wakati huo Waziri Mkuu mpya atakuwa ameshapatikana. Kiongozi mpya wa Labour baada ya Starmer, ndiye atakuwa Waziri Mkuu, kwa sababu chama hicho ndicho kina wabunge wengi.

Mbunge wa Makerfield, Manchester, Andy Burnham, ndiye anapewa nafasi kubwa ya kumrithi Starmer. Burnham, ambaye ni meya wa zamani wa Jiji la Greater Manchester, alishinda ubunge kwenye uchaguzi mdogo, uliofanyika Juni 18, 2026, baada ya aliyekuwa mbunge, Josh Simmons, kujiuzulu.

Wakati Simmons, ambaye alikuwa mbunge kwa tiketi ya Labour, alipokuwa anajiuzulu ubunge, tayari zilishakuwepo fununu kwamba alishakuwa na makubaliano na Burnham, ili agombee uchaguzi mdogo, ashinde, kisha Starmer alazimishwe kujiuzulu uwaziri mkuu, halafu Burnham awe waziri mkuu mpya.

Ushindi wa Burnham kuwa mbunge wa Makerfield, umesafisha njia, na kuonesha ni mwanasiasa mwenye mvuto. Maana, matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa, uliofanyika Mei 7, 2026, yalionesha vyama vya Labour na Conservative, vinapoteza uungwaji mkono. Hivyo, Burnham anaweza kuipa Labour pumzi mpya.

Matokeo yenye kuonesha uungwaji mkono wa chama kipya, Forum UK, kinachoongozwa na Nigel Farage, na Chama cha Green, ambacho kinara wake ni Zack Polanski, wakati huohuo Labour na Conservative, vikipoteza viti vingi, imeleta tafsiri kwamba wananchi wamechoshwa na ukiritimba wa vyama viwili, na sasa wanataka mwanzo mpya.

Kwa karne moja sasa siasa za UK zimekuwa chini ya ukiritimba wa vyama viwili (two-party dominant system), ambavyo ni Labour na Conservative. Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Uchaguzi UK, vyama vya siasa vilivyosajiliwa ni zaidi ya 400. Katika hivyo, 11 ndivyo vyenye uwakilishi bungeni (House of Commons).

Tangu mwaka 1920 (karne nzima iliyopita), Labour kiliibuka na kusababisha utawala wa vyama viwili uwe Labour na Conservative. Kabla ya hapo, vyama vilivyokuwa vikitawala siasa za UK vilikuwa Conservative na Liberal. Baada ya Liberal kupoteza uungwaji mkono na Labour kukubalika, upepo wa utawala wa vyama vya siasa ulibadilika.

Hata sasa, jinsi Forum UK inavyokubalika, ishara ni kuwa Labour na Conservative vitapoteza nguvu na kuondoa ukiritimba wa vyama viwili, au kuna chama, kati ya Conservative au Labour, kitapisha kingine, hivyo kukaribisha zama mpya za ushindani wa kisiasa. Conservative wana hali mbaya zaidi.

Ni ujumbe kuwa kipindi Starmer anandoka kwenye kiti. Haiwi sawa na waziri mkuu mmoja anaondoka na kuingia mwingine, bali kuna dalili za ujio wa zama mpya. Siasa za UK zinakwenda kuwa tofauti na ilivyokuwa kipindi chote cha karne moja iliyopita.


Historia ya vyama UK

Mpaka kufikia Karne ya 17, yaani miaka ya 1600, duniani kote hakukuwa na vyama vya siasa, ingawa siasa zilizungumzwa na kujadiliwa tangu Karne ya 5 baada ya kalenda.

Mwanzoni kabisa katika uliokuwa utawala wa Roma ya kale, seneti yake iliwakilishwa na makundi mawili ambayo yaliitwa Patricians na Plebeians. Patricians ni kundi la viongozi na watu wenye hadhi kubwa kwenye jamii, wakati plebeians walikuwa wafanyabiashara wakubwa.

Hivyo, Patricians na Plebeians huwezi kuita mwanzo wa vyama vya siasa kwa sababu makundi mawili ya watu waliojiona wapo daraja la juu (the elites), walikutana kujadili masilahi yao na jinsi ya kuwatawala wananchi maskini.

Vyama vya siasa vilianza mwaka 1678 kutokana na nadharia inayoitwa Popish Plot. Kwa ufafanuzi ni kuwa Popish Plot ni uzushi uliotungwa na Muingereza Titus Oates, ukieleza kuwa Kanisa Katoliki lilipanga kumuua aliyekuwa Mfalme wa England, Charles II.

Titus hutambulika kama mla kiapo cha uongo (perjurer), vilevile hutambulishwa kama Titus the Liar (Titus cha uongo). Katika uzushi huo, alilitumia Kanisa Katoliki kumchonganisha Mfalme Charles II na mdogo wake, James ambaye alikuwa na cheo cha Duke wa York.

Katika uzushi wake, Titus alisema kuwa Kanisa Katoliki lilipanga kumuua Mfalme Charles II kisha kumsimika ufalme James, ambaye alikuwa Mkatoliki.

Kutokana na uzushi huo, Bunge la England liliamua Wakatoliki wote waondoke kwenye ofisi za umma, vilevile walifanya jaribio la kutaka kumwondolea James haki ya kurithi kiti cha Ufalme. Hali ilikuwa hivyo kwa sababu Mfalme Charles II na wabunge wengi walikuwa Anglikana.

Damu ni nzito kuliko maji. Mfalme Charles II alikataa mdogo wake kuondolewa kwenye haki ya kurithi ufalme, alipinga pia Wakatoliki kuondolewa kwenye ofisi za umma.

Hata baada ya uchunguzi kuthibitisha kuwa Titus alisema uongo chini ya kiapo, wabunge walisisitiza Wakatiloki waondolewe, hivyo ukatokea mgawanyiko mkubwa. Wabunge walisema wana haki zote za kuuagiza utawala, wakati Mfalme Charles II alisema, uamuzi wa wabunge ulikuwa unaingilia mamlaka ya ufalme.

Kutokana na hali hiyo, wananchi waligawanyika. Waliomuunga mkono Mfalme Charles II kuwa ufalme usiingiliwe, walijiita Tories, jina ambalo asili yake ni Wakatoliki walioteseka sana Ireland. Upande wa wabunge walijiita Whigs, ambalo ni msimiati wa zamani wa Scotland wenye maana ya kuipinga Serikali.

Kwa mvutano huo, kwamba ama Mfalme ndiye awe na nguvu za kuamua katika ufalme wake bila kuingiliwa au wananchi kupitia wawakilishi wao, yaani wabunge ndiyo wawe na nguvu ya kumpangia Mfalme, ndiyo mwanzo wa kuzaliwa kwa vyama vya kisiasa vya Whigs na Tories.

Katikati ya Karne ya 19, vyama vya Tories na Whigs vilibadili majina. Tories ndiyo Conservative, na Whigs ni Liberal. Conservative kilibadilishwa jina kutoka Tories mwaka 1834, wakati Liberal ilizaliwa kutokana na Whigs mwaka 1859.

Kutoka katikati ya Karne ya 19 mpaka muongo wa pili wa Karne ya 20, Conservative na Liberal vilitawala siasa za UK.

Ukuaji wa tabaka la wafanyakazi Karne ya 20, na vyama vya wafanyakazi kujenga hamasa ya kushiriki uamuzi wa masuala ya nchi, ndiyo sababu ya Labour kuwa chama cha siasa. Na ilipofika Januari 22, 1924, Labour iliweza kupata viti vingi na kuongoza serikali, chini ya Waziri Mkuu, Ramsay MacDonald.

Tangu wakati huo mpaka sasa, Labour na Conservative vimeendelea kutawala siasa za UK. Je, kuelekea Uchaguzi Mkuu UK 2029, Forum UK itapindua meza, kama Labour ilivyoipindua Liberal? Je, Forum UK na Green, vitabadili mfumo wa siasa za kutazama vyama viwili, na kufanya iwe gombania goli kwa vyama vingi. Acha Starmer aondoke, halafu itajulikana, lipi tui, yapi maziwa!