Simbachawene: Ubunge wa safari hii nauhitaji kuliko wakati mwingine, nitafia huku

Muktasari:
- Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, ambaye pia ni Mbunge wa Kibakwe, amesema kuwa wakati wa uchaguzi, kama ilivyo sasa, ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kunakuwa na ushindani mkali zaidi kuliko sehemu nyingine yoyote.
Arusha. Joto la Uchaguzi Mkuu 2025 linaendelea kupanda. Hii ni baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, kusema kuwa ubunge wa safari hii anauhitaji kuliko ubunge wowote na kuwa ‘atafia’ katika harakati hizo.
Amesema kuwa wakati wa uchaguzi, siyo tu vyama vya siasa vinashindana, bali hata ndani ya CCM kuna ushindani mkali, na kwamba wanakanyagana kuliko sehemu nyingine yoyote.
Wakati waziri huyo akiyasema hayo, CCM ilifanya mabadiliko katika Katiba yao, ambayo yanahusu ongezeko la idadi ya wajumbe watakaoshiriki katika kupiga kura za maoni kwa wagombea wa udiwani na ubunge.
Wajumbe hawa ni pamoja na wanachama wa kamati ya siasa katika kila tawi, kata za jimbo, au wilaya husika.
Simbachawene amesema kuwa duniani kote, wakati wa uchaguzi unapokaribia, hamasa inakuwa kubwa na mawazo ya watu hayazingatii amani, utulivu au hatma ya taifa, badala yake lengo kuu linakuwa ni kushinda uchaguzi.
Simbachawene ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 8, 2025, wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ulioanza leo hadi Mei 10 jijini Arusha.
“Hii haipo tu kwenye vyama vya siasa peke yake, kwamba vyama vya siasa vinataka kushindana na CCM, hata ndani ya CCM yenyewe inapofika wakati wa uchaguzi tunakanyagana kweli kweli, tena huko ndiyo tunakanyagana kuliko sehemu nyingine yoyote,” amesema.
Simbachawene ameongeza; “Ukiniambia mimi mbunge wa Kibakwe, upinzani wa nchi hii, kule wapinzani wangu ni CCM. Nashughulika nao kweli ili nibaki, kule ni CCM watupu, tunakanyagana wenyewe. Watu wakishakosa kura za maoni, wanateuliwa mtu, ndiyo wanahamia kutafuta vyama vingine.”
Waziri huyo amesema kuwa shida wakati wa uchaguzi iko ndani ya CCM kuliko hata nje ya chama hicho na kwamba wakati wa uchaguzi mawazo mengi yanajikita kwenye kushinda uchaguzi pekee.
“Hata mimi hapa nina kipindi cha nne, naenda cha tano, lakini ubunge wa safari hii nauhitaji kuliko wote waliopita, nauhitaji kweli kweli maana sasa ndiyo umekolea.
“Nimeshaona siwezi kuajirika, sina ‘alternative’, kwenye uwakili wenyewe sija ‘practice’ vizuri, joho langu nimeliweka. Akina Mwabukusi wameshanizidi huku mpaka nije nifungue 'chamber' nipate hela leo? Najiuliza, wakati mwingine, nifanye nini?”
“Kwa hiyo mimi nafia hukohuko, na raha ya siasa ni mpaka utolewe. Siyo unasema unajua mimi namuachia mtu, hakunaga mtu anamuachia mtu kwenye siasa mpaka utolewe. Na mimi nangojea Mwabukusi ukija kule, kugombea utake kunitoa mtani wangu, wewe njoo lakini tutakanyagana kweli kweli,” amesema Simbachawene.
Pia, amevitaka vyama vya siasa na wanasiasa wasije wakasukuma ajenda zao mpaka taifa likajikuta likiwajibika kwa maamuzi ambayo leo wanajuta.
“Mifano ya mataifa mengine inaonyesha ajenda ya kisiasa wakati wa uchaguzi ilileta maamuzi ambayo leo wanajuta wakitafuta njia ya kurudi nyuma, lakini hiyo haitakuwepo.
“Kwa hiyo mawazo yataendelea kuboreshwa, lakini hatua zinapigwa katika kujenga demokrasia ya nchi. Vyama na siasa zilizofanyika kuanzia miaka ya 1995 hadi 2000 ni tofauti na hali ya sasa. Mabadiliko yametokea, tutaangalia tunavyokwenda,” amesema.
Amesema hakuna mtu anayeweza kukataa kwamba mawazo yanayolenga kuboresha si mabaya. “Tunapokea mawazo hayo kama Serikali na ninasema kwa nafasi yangu ya msimamizi wa utawala bora kwamba tuendelee kuboresha. Hakuna kitu kilichokamilika; hata taasisi nyingine na vyombo vingine havijakamilika,” amesema.
Simbachawene amesema; “Mimi kama Mkristo, Biblia inasema kuwa huku duniani kila kitu ni ubatili mtupu, hakuna kilichobadilika kikamilifu. Hivyo, hakuna kilichokamilika, labda umekipata kutoka kwa Mungu. Mapungufu yatakuwepo na yakiwepo ni wajibu wetu kuendelea kuyashughulikia, kukosoana na kurekebishana ili tujenge nchi ya watoto na wajukuu.”
“Tukicheza na haya mambo leo, gharama itakuwa kubwa kwa vizazi vinavyokuja. Lazima tukubaliane kuboresha, kulinda tulichonacho, kwani mwisho wa siku ni taifa libaki moja.”
Katika mjadala huo wa mabadiliko, Simbachawene amesema kuwa mawazo ya kuboresha yanafaa kutolewa, lakini pia, mawazo yanayolenga kuvunja au kuchochea machafuko pia yapo.
“Kuna watu wengine wangetamani tuingie kwenye vita. Kwa sababu, leo nchi ikivurugika, hatuendi,” alisema.
Akizungumzia nafasi ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Waziri amesema, “TLS mmejipa jukumu la kuwa shangazi wa ukweli. Kwa mara ya kwanza, TLS inahama kutoka kwenye miguu ya siasa na inakaa katikati kama shangazi, inachapa kidogo huku na huko, inatoa onyo, iko katikati.”
Kwa upande mwingine, Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, alisisitiza kuwa uchaguzi siyo zoezi la vita bali ni zoezi la kidemokrasia.
“Kila suala lifanyike kwa uwajibikaji, na pale ambapo tunafikiri hapako sawa, lazima wakutane kuzungumza,” amesema Mwabukusi.
“Hatutakiwi kusubiri kupigana, hatuna mtu wa kumpiga, wala hatutakiwi kusubiri kuuana, hatuna wa kuua. Hii ndiyo maana siku moja nilimwambia mtu katika mchakato wa kidemokrasia huwa najisikia kuugua nikimuona mtu eneo la uchaguzi anabeba silaha,” amesema.
Mwabukusi amesema CCM kikiwa chama kikongwe kilichoongoza mapambano ya uhuru, kilikuwa kinatakiwa kuonyesha ukongwe wake sasa kwa kuzuia kauli zote zinazochochea hali ya kutengana.
“Walete kauli ya baba wa familia anayetaka kuitisha familia yake tukae kama taifa. Tuweke mbele maslahi ya taifa na tusiruhusu watu kuja kutusaidia kwenye mambo tunayoweza kufanya wenyewe,” amesema Mwabukusi.