Prime
Shonza na wenzake wa CCM waibwaga ACT Wazalendo kortini
Muktasari:
- Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Augustine Mwarija, Amour Hamis na Gerson Mdemu, baada ya kuridhika na hoja za wabunge wanane wa viti maalumu wa CCM walioomba uamuzi huo upitiwe.
Dodoma. Mahakama ya Rufani Tanzania imefuta uamuzi na amri za Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma zilizowapa ACT Wazalendo kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama kupinga uteuzi wa wabunge 115 wa viti maalumu.
Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi, Julai 23, 2026 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Augustine Mwarija, Amour Hamis na Gerson Mdemu, baada ya kuridhika na hoja za wabunge wanane wa viti maalumu wa CCM walioomba uamuzi huo upitiwe.
Wabunge hao ni Juliana Shonza, Asha Baraka, Rebecca Nsemwa, Mwanahamisi Munkunda, Lucy Mwakyembe, Husna Sekiboko, Fatma Rembo na Christina Mndeme. Walifungua maombi namba 126 ya mwaka 2026 dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya ACT Wazalendo, huku Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wakiwa wajibu maombi wa pili na wa tatu.
Wakati Mahakama ya Rufani ikitoa uamuzi huo, ACT Wazalendo walikuwa tayari wamefungua maombi ya mapitio baada ya kupewa kibali na Mahakama Kuu.
Katika maombi yao, Shonza na wenzake walidai walinyimwa haki ya kusikilizwa licha ya kuwa wahusika muhimu ambao masilahi yao ya ubunge yangeathiriwa na uamuzi uliokuwa ukitafutwa. Walieleza kuwa Novemba 7, 2025 waliteuliwa na INEC kuwa wabunge wa viti maalumu kupitia CCM, lakini walifahamu kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu kupitia vyombo vya habari bila kushirikishwa katika shauri hilo.
Walidai mwenendo wa shauri uliendeshwa bila kuwahusisha wahusika wote muhimu na maombi ya ACT Wazalendo yalisikilizwa upande mmoja (ex parte), jambo lililowaathiri.
Katika maombi yake ya kupata kibali cha kufungua mapitio, ACT Wazalendo ilieleza kuwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 ilipata kura 2,222,162 katika majimbo 181, sawa na asilimia 6.77 ya kura za ubunge. Chama hicho kilidai kilitimiza kigezo cha kikatiba cha kupata viti maalumu, lakini INEC iliteua wabunge 115 wa viti maalumu bila kukihusisha. Hivyo kiliomba uamuzi wa INEC wa Novemba 7, 2025 ubatilishwe na wanachama wake waliomo kwenye orodha wateuliwe kuwa wabunge wa viti maalumu.
Katika uamuzi wao, majaji walisema nyaraka za Mahakama Kuu zinaonyesha kuwa ingawa waombaji walitajwa mahususi na ACT Wazalendo, hawakujumuishwa kama wahusika katika maombi ya kupata kibali. Walisisitiza kuwa walikuwa wahusika muhimu kwa sababu wangeathirika moja kwa moja endapo uteuzi wao ungebatilishwa.
Majaji walisema kutowashirikisha kulisababisha ukosefu wa haki na kwamba suluhisho ni kufuta mwenendo mzima wa Shauri Na. 28632 la 2025 pamoja na uamuzi na amri zake. Hata hivyo, walieleza kuwa ACT Wazalendo ina uhuru wa kuanzisha upya shauri hilo kwa mujibu wa sheria, huku kila upande ukibeba gharama zake.