Serikali DRC yakamata mali za Kabila, kundi la M23 latajwa

Muktasari:
- Mara baada ya kuachia madaraka, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila amekuwa akiishi uhamisho Afrika Kusini kabla ya kurejea nchini humo.
Kinshasa. Hali ya DR Congo haijatulia licha ya jitihada mbalimbali za kusaka amani nchini humo. Mataifa kadhaa ya Afrika ikiwemo Tanzania, yalijitosa kuhakikisha DR Congo inakuwa na amani kutokana na machafuko yanayoendelea. Majeshi ya Serikali na makundi ya waasi yakiongozwa na M23 yamekuwa yakikabiliana na mpaka sasa miji kadhaa iko chini ya himaya za waasi.
Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea serikali ya DR Congo, inayoongozwa na Felix Tshisekedi imepiga marufuku shughuli zote za chama cha kisiasa cha rais wa zamani, Joseph Kabila cha People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD). Pia, imetangaza kutaifaisha mali zote za Kabila kwa kile kilichoelezwa kuwa na msimamo usioeleweka. Kabila anahusishwa pia na muunganiko na kundi la M23 kwa kuwa ameshindwa kulaani unyama dhidi ya raia wasio na hatia unaofanywa na wanamgambo wa kundi hilo.

Shirika la Habari la BBC limeripoti kuwa hatua hiyo imechukuliwa Aprili 19, 2025 kufuatia ripoti kuwa Kabila amerejea nchini DRC baada ya kutumia miaka miwili uhamishoni Afrika Kusini.
Kabila (53) alikuwa akiishi uhamishoni tangu alipoondoka madarakani baada ya kuibuka maandamano makubwa na yenye umwagaji damu dhidi ya utawala wake.
Alishika madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2001 baada ya kuuawa kwa baba yake, Laurent-Désiré Kabila, na alibaki madarakani hadi mwaka 2019.
Kwa sasa inaelezwa kwamba, Kabila amerejea nchini humo kupitia mpaka wa Goma, jiji ambalo waasi wa M23 walilitwaa mapema Januari, 2025 wakati wa mapigano kati yao na jeshi la serikali.
Hata hivyo, wakati serikali ikiwa na hofu ya kurejea kimyakimya kwa Kabila, taarifa nyingine zinadai kuwa ameonyesha nia ya kusaidia kumaliza mzozo unaoendelea kwa sasa.

Mwanasiasa na ofisa wa kijeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila ambaye alihudumu kama Rais wa nchi hiyo kutoka Januari 2001 hadi Januari 2019.
Aprili 19, 2025 Wizara ya Mambo ya Ndani ya DRC ilitoa taarifa ikikosoa uamuzi wa makusudi wa Kabila kurejea nchini humo kupitia Jiji la Goma linalodhibitiwa na M23
“Wizara inauarifu umma kuwa shughuli zote za PPRD zimesitishwa katika eneo lote la taifa,” ilisema taarifa hiyo ya wizara.
Katika taarifa nyingine, Wizara ya Sheria ya DRC ilitangaza kuwa imeamriwa kukamata mali zote zinazohamishika na zisizohamishika za Kabila.
“Hatua za kuzuia usafiri zimechukuliwa dhidi ya washirika wake wote wanaohusika na kesi hii ya usaliti dhidi ya taifa,” ilisema wizara hiyo.
Kulingana na taarifa hizo mbili, waendesha mashitaka wameagizwa kuanzisha mashitaka dhidi ya Kabila kwa ushiriki wake wa moja kwa moja katika uasi kupitia kundi la kigaidi la AFC/M23.
M23 wameteka miji mikubwa miwili Mashariki mwa DRC ya Goma, Bukavu na Nyabibwe tangu mwanzo wa mwaka huu.

Serikali ya Tshisekedi mara kwa mara imekuwa ikiituhumu Rwanda kwa kuchochea mgogoro huo wa muda mrefu madai ambayo nchi hiyo jirani kupitia kwa Rais Paul Kagame imeyakanusha.
Hatua dhidi ya Kabila na chama chake zimechukuliwa huku mazungumzo ya amani kati ya Kinshasa na M23 yakipigwa kalenda hadi tarehe ambayo haijatangazwa hadharani.
PPRD haijatoa tamko lolote
Wakati hatua hizo zikichukuliwa dhidi yake, Kabila amewahi kukanusha kuwa na uhusiano na M23. Mpaka sasa hakuna taarifa zozote kutoka kambi ya Kabila kuhusu uamuzi huo wa Serikali ya DRC.
Maofisa waandamizi wa PPRD wamekanusha kuhusu uwepo wa Kabila mjini Goma. Msemaji wake, Barbara Nzimbi aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa X, kuwa Kabila atalihutubia taifa katika saa ama siku chache zijazo.
Msemaji wa M23 hakuthibitisha wala kukanusha uwepo wa Kabila mjini Goma huku akisema: “Sioni tatizo yeye kuwepo hapa.”
Joseph Kabila ni nani?
Baada ya kula kiapo cha urais kufuatia kifo cha baba yake, Kabila alishinda uchaguzi mara mbili.

Joseph Kabila wakati anaapishwa kuwa Rais wa DR Congo mwaka 2001.
Muhula wake wa pili na wa mwisho ulimalizika Desemba mwaka 2016, lakini alikataa kuondoka madarakani akisema haiwezekani kuandaa uchaguzi, jambo lililosababisha maandamano yenye umwagaji damu.
Aliendelea kubaki madarakani kwa miaka miwili zaidi hadi uchaguzi ulipofanyika mwaka 2018.
Januari 2019, alikabidhi madaraka kwa Félix Tshisekedi, aliyeshinda uchaguzi uliogubikwa na utata na ambao, wachunguzi wengi wa uchaguzi walidai kuwa Martin Fayulu ndiye aliyeshinda kihalali.
Fayulu alimtuhumu Kabila na Tshisekedi kwa kufanya makubaliano ya kumtenga kutoka madarakani jambo ambalo wote wawili walikanusha.
Hata hivyo, uhusiano kati yao uliharibika na ushirikiano wa vyama vyao kukatishwa rasmi Desemba mwaka 2020 ambapo, Kabila aliondoka DRC mwaka 2023 kwenda Afrika Kusini.
Januari 2024, utafiti wake wa uzamivu kuhusu jiografia ya kisiasa ya mahusiano kati ya Afrika na Marekani, China na Russia ilikubaliwa katika Chuo Kikuu cha Johannesburg.
Kwa nini Kabila amerudi?
Katika taarifa ya maandishi ya kutangaza kurudi kwake, Kabila alisema anarejea kwa sababu ya nia ya kusaidia kutatua mgogoro wa taasisi na usalama unaozidi kuwa mbaya nchini DRC.
Pia aliliambia jarida la Kifaransa Jeune Afrique kuwa anataka kuchukua nafasi ya kusaidia kutafuta suluhisho.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira