Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Salum Mwalimu na magumu ya maisha ya siasa

Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi.

Muktasari:

  • Mwalimu ambaye kwa zaidi ya muongo mmoja ameishi katikati ya siasa za upinzani, alizianza harakati hizo kwa kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiacha kazi ya taaluma yake.



Dar es Salaam. Ingawa siasa ndilo eneo linalompa furaha kulitumikia, Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amesema kupitia jukwaa hilo amepoteza marafiki na kuisababishia hofu familia yake.

Mwalimu ambaye kwa zaidi ya muongo mmoja ameishi katikati ya misukosuko ya siasa za upinzani, alizianza harakati hizo kwa kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiacha kazi ya taaluma yake.


Uamuzi mgumu

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mwalimu anasimulia namna alivyoingia kwenye siasa kwa uamuzi aliouita mgumu zaidi kuwahi kuufanya maishani mwake.

Safari hiyo ilianza mwaka 2014 alipoteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, hatua iliyomlazimu kuachana na ajira yake ya taaluma aliyokuwa ameifanya kwa zaidi ya miaka saba.

“Haukuwa uamuzi mwepesi, na sidhani kama nitakuja kufanya uamuzi mgumu kama ule tena,” anasema Mwalimu.

Anasema wakati huo watu wengi walishangazwa na uamuzi wake wa kuacha maisha ya ajira na kuingia moja kwa moja kwenye siasa za upinzani.

Anasema ingawa walikuwepo waliomuunga mkono, lakini wengi walimtilia mashaka, wengine wakiamini huenda alikuwa ametumwa au alikuwa na ajenda nyingine iliyojificha.

“Haukuwa uamuzi mwepesi kwenye maisha yangu. Niligeukia siasa kwa kuamini nchi inahitaji mabadiliko, nikasema wacha nikatoe mchango wangu,” anasema.

Anasisitiza kuwa hakukimbilia siasa kwa ajili ya kutafuta fedha wala maisha mazuri, kwa sababu hata kabla ya kuingia huko alikuwa tayari anaweza kumudu mahitaji yake na ya familia yake.

“Sikufanya hivyo kwa sababu ya pesa. Kama ni pesa nilikuwa nazo za kula na za kukidhi mahitaji ya familia yangu. Nilikwenda huko kwa kuwa furaha yangu ni kuona tunafanya mabadiliko katika siasa za Tanzania,” anasema.

Kwa zaidi ya miaka 11 sasa, Mwalimu amekuwa kwenye siasa za upinzani. Ameitumikia Chadema kwa zaidi ya muongo mmoja kabla ya kuhamia Chaumma, ambako sasa ni katibu mkuu.

Anasema safari hiyo haijawahi kuwa nyepesi.

“Kujitambulisha mbele ya dunia kuwa unapambana na Serikali si kitu chepesi,” anasema.


Magumu aliyopitia

Katika kipindi hicho, anasema amekaa mahabusu na gerezani mara nne, huku akikamatwa na kushikiliwa kwenye vituo mbalimbali vya polisi mara nyingi kiasi kwamba baadhi ya vituo hivyo asingevijua kabisa kama asingekuwa mwanasiasa.

“Kuna vituo vya polisi ambavyo nisingevifahamu kama nisingekuwa mwanasiasa. Siasa imenipitisha kwenye mitihani mizito,” anasema.

Lakini si yeye pekee aliyebeba mzigo wa safari hiyo, anaeleza kuwa hata familia yake imekuwa sehemu ya maumivu ya siasa zake.

Anasema kulikuwa na nyakati ambazo baadhi ya ndugu zake waliogopa hata kuonekana naye hadharani, wakihofia kuhusishwa na misimamo yake ya kisiasa. Wengine walimshauri asiende kwenye baadhi ya shughuli za kifamilia kwa sababu tu ya hofu iliyokuwapo.

“Ilifika mahali ndugu walikataa nisiende kwenye shughuli za kifamilia kwa sababu waliogopa watu wajue mimi ni ndugu yao,” anasema.

Marafiki waliokuwa karibu naye kabla ya kuingia kwenye siasa, anasema walijitenga taratibu baada ya yeye kujiingiza kwenye siasa za upinzani.

“Nilipoingia kwenye siasa tu walinitenga. Watu tuliokuwa tunakutana, tunakula bata pamoja, wengi waliondoka,” anasema.

Hata hivyo, pamoja na kuachwa na baadhi ya watu wa karibu, Mwalimu anasema hakuwahi kujutia njia aliyochagua.

“Kwa kuwa niliingia kwenye jambo nililoliamini na kufurahi kulifanya, niliona ni lazima niendelee. Furaha yangu kubwa ni kuona uwezekano wa mabadiliko unafanikiwa hata kama njia yenyewe ni ngumu,” anasema.

Lakini kati ya watu wote waliobeba maumivu ya safari yake ya kisiasa, anasema hakuna aliyekuwa na hofu kubwa kama mama yake na mtoto wake.

“Tunapambana kama vile tunasali tukitamani kufika peponi. Nafahamu namna ambavyo siasa zimegeuka kuwa hofu kwenye maisha ya watu wangu wa karibu,” anasema.

Anasimulia jinsi mama yake anavyokesha usiku akisubiri kujua kama mwanawe yupo salama, huku mtoto wake naye akiwa na wasiwasi kila anapochelewa kurudi nyumbani.

“Kama sijarudi nyumbani, mwanangu anapiga simu usiku kuniuliza, ‘baba uko wapi?’ Mama yangu halali, anataka tu kujua kama nipo salama,” anasema.

Licha ya hofu hiyo, anasema familia yake haijawahi kumzuia kuendelea na siasa, badala yake wamekuwa wakimtia moyo na kumkumbusha kumtegemea Mungu katika kila hatua.

“Huwa wananisisitiza kuomba. Wananambia ukiamka asubuhi sali, yaweke maisha yako ya siasa mikononi mwa Mungu. Ndicho ninachokifanya,” anasema.

Kutokana na majukumu ya kisiasa, Mwalimu anasema mara nyingi ameshindwa hata kushiriki baadhi ya matukio muhimu ya kifamilia, ikiwamo misiba ya ndugu wa karibu.

Anasema mwanzoni hali hiyo iliwaumiza sana ndugu zake, lakini kadiri muda ulivyopita walikuja kuelewa aina ya maisha aliyochagua.

“Baadaye walinielewa. Wakanikubali na hata kunishauri kwamba nikipata nafasi nifike kutoa pole,” anasema.


Maisha kama baba

Hata hivyo, nje ya siasa na misukosuko yake, Mwalimu anasema akiwa nyumbani hubadilika kabisa. Nyumbani kwake yeye si katibu mkuu wala mwanasiasa, bali ni mume na baba wa kawaida anayependa kucheza na familia yake.

“Napenda mke wangu amuone mumewe, si katibu mkuu. Napenda kucheza na watoto wangu, hata kuwaandalia kifungua kinywa,” anasema.

Anasema ndani ya nyumba yake mijadala ya kisiasa huachwa nje ya mlango. Simu hupoteza umuhimu wake na muda mwingi huutumia na familia yake.

“Kuna muda mwanangu ananiambia, Daddy wewe ulikuwa mgombea urais. Lakini mimi nikiwa nyumbani napenda kucheza na mtoto wangu, nikae na mke wangu na hata niamke mapema kuwaandalia kifungua kinywa,” anasema.

Mwalimu anasema yeye ni mpishi mzuri wa mayai na anaweza kutengeneza kifungua kinywa kizuri kwa familia yake.

“Nafahamu kuchemsha mayai, kutengeneza spanish na toast. Nikiamua naweza kukaanga kuku na chipsi kwa ajili ya familia yangu,” anasema.

Anasema simu yake nayo imekuwa sehemu ya maisha ya familia kiasi kwamba mtoto wake ameshazoea baadhi ya majina ya watu wanaompigia.

“Simu ikiita mwanangu atasema anko Mrema anapiga au anko Kigaila anapiga,” anasema.

Katika simulizi yake, Mwalimu pia anagusia namna anavyoamini kwenye unyenyekevu katika uongozi. Anasema watu wengi humwona kama mwanasiasa wa diplomasia sana, lakini kwake huo si udhaifu.

“Huwa naambiwa wewe Mwalimu upo diplomatic sana. Nasema sawa, na kama kuwa mnyenyekevu ni udhaifu basi wacha niwe dhaifu,” anasema.

Anasema siku zote amekuwa mtu anayependa kujifunza na kuepuka kutengeneza maadui wa lazima.

“Hata huko nilikotoka wapo tunaowasiliana nao hadi leo. Nikikutana na mtu popote nitakuwa wa kwanza kumsalimia,” anasema.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, Mwalimu alikuwa mgombea urais kupitia Chaumma. Hata hivyo, alipoulizwa kama ana ndoto ya kugombea tena mwaka 2030, anasema hana mpango huo.

“Mimi kugombea tena 2030? Hapana. Urais ni nafasi nzito sana,” anasema.

Kwa mtazamo wake, urais si nafasi ya kutafuta heshima au umaarufu, bali ni jukumu kubwa lenye uzito wa maamuzi yanayogusa maisha ya watu.

“Kama wewe ni mtu mwenye hofu ya Mungu, si jambo jepesi. Ukiacha Mungu anayefuata ni Rais. Anaweza kusema huyu afungwe asiulizwe na mtu. Mvua ikinyesha ikaleta maafa ni wewe, jua likipiga sana ni wewe pia,” anasema.

Hata hivyo, licha ya yeye kutokuwa na mpango wa kugombea tena urais, ana matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa chama chake kuelekea mwaka 2030.

“Labda litokee jambo kubwa sana la kutuzuia, lakini kwa hii misukosuko ya kawaida ya kisiasa tutakomaa na tutapambana. Naamini 2030 tutakuwa mbali zaidi,” anasema.