Rais Samia na Dangote wakutana tena Ikulu Dar, wajadili haya
Muktasari:
- Mfanyabiashara, Aliko Dangote amekutana tena na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni mara mbili ndani ya miezi miwili.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Dangote Group, Alhaj Aliko Dangote kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji zinazolenga kuharakisha maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
Hii ni mara ya pili wawili hao wanakutana katika kipindi kifupi. Awali, walikutana Mei 16, mwaka huu na walijadili kuhusu uwekezaji wa ujenzi wa kiwanda cha mafuta nchini.
Taarifa ya kukutana kwao, imetolewa leo, Jumapili Juni 28, 2026 na kutiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dangote ameeleza utayari wa kampuni yake kupanua ushirikiano wa uwekezaji na Serikali katika sekta mbalimbali za kimkakati zenye mchango kwa maendeleo ya Taifa.
Miongoni mwa maeneo yaliyojadiliwa ni miundombinu ya usafirishaji, uzalishaji wa mbolea nchini na sekta ya nishati, ambazo zinatajwa kuwa na uwezo wa kuchochea shughuli za kiuchumi nchini na katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Dangote, amesema Tanzania inaendelea kuwa moja ya nchi zenye mazingira mazuri ya uwekezaji barani Afrika kutokana na sera zake za kuvutia wawekezaji na fursa zilizopo katika sekta za uzalishaji na viwanda.
Amesema kampuni yake imebaini maeneo yenye manufaa makubwa ambayo yanaweza kuendelezwa kwa ushirikiano na Serikali kwa lengo la kuongeza thamani ya malighafi, kukuza biashara ya kikanda na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Rais Samia amesema Serikali imepokea kwa uzito mapendekezo na nia ya uwekezaji iliyowasilishwa na Dangote Group.
Amezitaka wizara na taasisi husika kuendelea na majadiliano ya kitaalamu ili kufanikisha maeneo yaliyoainishwa kwa kuzingatia sera, sheria na vipaumbele vya maendeleo ya nchi.
Rais Samia, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi katika kuvutia uwekezaji wenye tija unaochochea ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda, uhamishaji wa teknolojia pamoja na uundaji wa ajira kwa Watanzania.
Mbali na Rais Samia, miongoni mwa mawaziri walioshiriki kikao cha leo na wizara zao kwenye mabano ni, Profesa Kitila Mkumbo (Mipango na Uwekezaji), Deogratius Ndejembi (Nishati) na Judith Kapinga wa Viwanda na Biashara.
Pia, kulikuwa na makatibu wakuu, Dk James Mataragio (wa Nishati anayeshughulikia mafuta na gesi asilia na Felichesmi Mramba anayeshughulikia nishati.