Prime
Saa 72 ‘moshi mweupe’ CCM
Muktasari:
- CCM inatarajia kutangaza majina matatu ya wagombea ubunge na udiwani kwa kila jimbo na kata ndani ya saa 72 kuanzia leo, baada ya kikao cha Kamati Kuu Julai 19, 2025. Mchujo umehusisha maelfu ya watia nia, huku viongozi wakisisitiza subira na kufuata taratibu rasmi.
Dar es Salaam. Hatima ya kujulikana majina ya kina nani yaliyopenya katika mchujo wa vikao vya kitaifa vya Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kupatikana wagombea wa ubunge na udiwani, inatarajiwa kujulikana ndani ya saa 72 kuanzia leo.
Ndani ya saa hizo, mamlaka za CCM zinatarajiwa kuweka wazi majina matatu kwa kila kata kwa ajili ya udiwani, matatu kila jimbo kwa ajili ya ubunge na uwakilishi, wote hao watasubiri kupigiwa kura za maoni na wajumbe.
Majina matatu hayo ya ubunge na udiwani yanayotarajiwa kuwekwa hadharani ndani ya saa hizo ni baada ya mchujo mkali wa maelfu ya watiania waliojitokeza kuomba nafasi hizo kupitia chama hicho tawala.
Kwa upande wa ubunge wa majimboni, makada 4,109 walitia nia kuomba ridhaa katika majimbo 272, huku madiwani ni 30,000 wakizitaka kata 3,960.
Mchujo ulianza kwa kuzikutanisha Kamati za Siasa za Kata, kisha Wilaya, zilizokuwa na jukumu la kupendekeza majina matatu ya watiania na kuwasilisha kwa kamati hizo ngazi ya mkoa kwa upande wa udiwani na ubunge.
Kamati hizo ngazi ya mkoa nazo zilikuwa na jukumu la kupendekeza watiania watatu kwa upande wa udiwani, zilitoa mapendekezo ya watiania watatu kwa upande wa ubunge na kuyawasilisha ngazi ya Taifa.
Julai 14, 2025, Sekretarieti ya CCM Taifa ikiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi, ilipokea kijiti cha jukumu hilo na kuanza mchujo wa majina hayo hadi Julai 18.
Hatua hiyo itafuatiwa na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho cha Julai 19, 2025, kitakachoongozwa na mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, kikiwa cha mwisho kufanya uteuzi.
Uteuzi wa Kamati Kuu, utaambatana na mwongozo wa kuweka hadharani majina hayo matatu ya watiania wa ubunge, huku siku hiyohiyo mikoa nayo inaelezwa itaweka wazi majina matatu ya udiwani kwa kila kata na wale wa viti maalumu.
Siku hiyo ndiko mjadala wa nani amepenya na nani amekwama utafungwa rasmi, na turufu itasalia mikononi mwa wajumbe kuangalia nani kati ya watatu hao anafaa kupigiwa kura za maoni Agosti 2, 2025.
Mmoja wa vigogo ndani ya CCM aliyezungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina, amesema mchakato unaendelea na muda ukifika, baadaye vikao vya Kamati Kuu kumalizika, majina yatatolewa.
“Unajua mwaka huu kuna ushindani mkubwa huko kwa madiwani na wabunge, tunataka majina ya madiwani na wabunge yatoke pamoja ili kama ni vurugu au kuwekana sawa kwa waliopita na kufyekwa ifanyike kwa pamoja,” amesema kigogo huyo.
Saa 72
Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Julai 16, 2025, Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Langael Akyoo amesema orodha rasmi ya majina ya wagombea udiwani na ubunge itatangazwa kuanzia Julai 19, 2025, baada ya kikao cha Kamati Kuu kukamilika.
Amesema uvumi wa mitandaoni kuwa majina ya watiania udiwani yatawekwa hadharani Alhamisi Julai 17, 2025 ni upotoshaji usio na msingi wowote.
"Uhakika wa majina kuwekwa hadharani ni baada ya kikao cha Kamati Kuu. Taarifa kwamba yanaweza kutangazwa leo si za kweli. Kuanzia Julai 19 ndiyo muda sahihi kulingana na mwongozo wa chama," amesema Akyoo.
Kutokana na utaratibu uliowekwa na chama hicho, amesema wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge huenda wataenda kujitambulisha kwa wajumbe kwa pamoja katika kila kata, hivyo lazima majina ya wagombea wote yatangazwe kwa wakati mmoja.
"Ni muhimu wagombea wote wawe na subira. Hili si jambo la mtaani au mitandaoni. Tufuate taratibu rasmi. Watia nia wasiwe na hofu, bali waendelee kuwa watulivu na wasisikilize taarifa zisizo rasmi," ameongeza.
Kiongozi mwingine wa CCM Mkoa, aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema matumaini ya kurudi kwa majina hayo ya udiwani ni baada ya kukamilika kwa vikao vya Sekretarieti ya chama hicho na Kamati Kuu.
Ameeleza kurudi kwa majina ya wagombea wa udiwani, kutaambatana na yale ya wagombea ubunge na kwa pamoja watakwenda kujitambulisha kwa wajumbe kata kwa kata.
“Wagombea wote kwa pamoja wa ubunge na udiwani watakwenda kujitambulisha kwa wapigakura za maoni kata kwa kata, kwa hiyo majina yatarudi pamoja,” ameeleza.
Kiongozi huyo amesema majina yanayotarajiwa kutangulia pengine ni ya waliotia nia ya udiwani wa viti maalumu.
Msisitizo wa kauli hiyo umetolewa pia na kiongozi mwingine wa chama hicho ngazi ya wilaya, aliyesema uwezekano wa majina hayo ya udiwani kutolewa ni Julai 19.
Ameeleza yatatolewa kwa pamoja na wagombea ubunge, kila kata watatu kwa upande wa madiwani na kila jimbo watatu kwa maana ya ubunge.
Ingawa taarifa zinaeleza hivyo, amesema vikao vya Sekretarieti na hatimaye Kamati Kuu, ndivyo vitakavyotoa maelekezo ya lini wilaya na mikoa ziweke wazi majina hayo.
“Mipango inapangwa na ngazi ya Taifa, wao ndiyo watakaotupa maelekezo ya lini tutoe hayo majina, lakini uwezekano ni Julai 19 baada ya Kamati Kuu kumaliza kikao chake, kwa sababu Sekretarieti inachambua, ikimaliza inakabidhi ripoti kwa Kamati Kuu kuhitimisha kazi,” amesema.
Kwa upande wake, Diwani wa Mbagala, Michael Makwega, anayewania kuendelea na nafasi hiyo, amesema anaamini majina hayo yatatolewa rasmi Julai 19, baada ya Kamati Kuu kumaliza mchujo wa majina ya wagombea wa ubunge.
"Ni lazima majina yatangazwe kwa pamoja kwa sababu uteuzi wa wagombea udiwani unaweza kutoa picha ya mwenendo wa kisiasa, hivyo ni busara kuyaweka pamoja. Tunasubiri mwongozo rasmi," alisema Makwega.
Diwani wa Kipeta, mkoani Rukwa, Bahath Mbuza, anayetetea nafasi yake, amesema uhakika wa kurudi kwa majina ni Julai 19, lakini presha aliyonayo ni kweli jina lake litakuwa kwenye tatu bora?
“Unajua sahizi porojo zimekuwa nyingi na kama unavyojua wakati wa uchaguzi ni kawaida yake, lakini kusema kweli tunajiandaa Julai 19, 2025 kujua kama jina langu litachomoza kati ya watano tuliotia nia Kata ya Kipeta,” amesema.
Kulingana na Mbuza, uchaguzi huo utakuwa mgumu, kwanza mtihani unaanza kwenye kuchomoza jina kwenye watatu bora. “Ni jambo ambalo kusema kweli tunashinda kusali kwa kuwa hatima inakaribia.”
Ahadi ya CCM
Aprili 24, 2025, akiwa jijini Dodoma katika Wilaya ya Kongwa kwenye muendelezo wa kukagua utekelezaji wa Ilani na uhai wa chama hicho, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, alisema watapeleka wagombea kwa kuwasikiliza wananchi ili wapate mtu anayekubalika na wote.
"CCM safari hii hatutaki kujichosha, hatutaki kubeba mizigo kama umepakia kwenye mkokoteni halafu unasukuma, hatutaki. Mnasema mtu fulani mitano tena, je anakubalika? Lakini uamuzi wa mwisho ni wajumbe," alisema Wasira.
Alisema chama hicho kinahitaji kushinda uchaguzi kwa kishindo na ili kifanikiwe ni lazima kipate makada wanaokubalika kwa wananchi, hata akisimama wote wanasema mwenzao.