Polisi watanda Ruanda Nzovwe kudhibiti maadhimisho ya Bavicha

Askari Polisi wakiwa katika Uwanja wa Ruanda Nzovwe jijini Mbeya leo Jumatatu Agosti 12, 2024. Picha na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

  • Askari Polisi wameuzunguka Uwanja wa Ruanda Nzovwe wakiwa na bunduki na gari la washawasha, ikiwa ni hatua ya kudhibiti maadhimisho ya vijana yaliyoandaliwa na Bavicha Taifa.

Mbeya. Askari wa Jeshi la Polisi wametanda katika Uwanja wa Ruanda Nzovwe, jijini Mbeya kulipopangwa kufanyika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyokuwa yameandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).

Maadhimisho hayo yalikuwa yafanyike leo Jumatatu, Agosti 12, 2024, lakini Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Awadh Juma Haji lilitangaza kuyasitisha baada ya kutilia shaka tukio hilo akieleza kutokuwa rafiki kwa mustakabali wa nchi.

Polisi ilitangaza uamuzi huo ukitanguliwa na barua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwenda Chadema ya Agosti 8, 2024 kukitaka kusitisha shughuli hiyo, kwani lugha za viongozi wa Bavicha zinahatarisha usalama na zinakiuka sheria.

Mwananchi imefika eneo la Uwanja wa Ruanda Nzovwe na kushuhudia idadi kubwa ya polisi wakiwa na bunduki pamoja na gari la washawasha, huku wakiwa wamezunguka kona zote za uwanja huo.

Pamoja na kuimarisha ulinzi huo, wananchi waliohitaji kukatiza eneo hilo kwenda katika shughuli zao wamekuwa wakihojiwa kabla ya kuruhusiwa kuendelea.

Pia magari ya polisi yameendelea kupishana barabarani, ikiwa ni kuweka ulinzi na usalama kudhibiti maadhimisho hayo.

Licha ya ulinzi huo, bado viongozi wa Chadema wakiwamo Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lisu, Katibu Mkuu, John Mnyika, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya, Elisha Chonya na baadhi ya makada wengine wanadaiwa kuendelea kushikiliwa na Polisi tangu jana Jumapili Agosti 11, 2024.

Alipotafutwa kamanda wa Polisi mkoani humo, Benjamin Kuzaga, simu yake ilipokelewa na aliyejitambulisha kuwa msaidizi wake akieleza kamanda huyo yupo kwenye kikao kwa sasa.

Jana usiku katika akaunti yake ya X (zamani Twitter), Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alilaani kamatakamata hiyo akisema: “Tunalaani vikali Jeshi la Polisi kukamata viongozi wetu wakuu wa chama, wakiwemo viongozi wa Baraza la Vijana wa Chadema, Bavicha.”

“Aidha, tunalaani mkakati wa Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na Polisi kuzuia kongamano la Bavicha katika kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani hapo kesho Jumatatu 12 Agosti (leo).”

Katika andiko lake hilo, Mbowe alisema: “Tunadai kuachiwa haraka na bila masharti viongozi, wanachama na wapenzi wetu wote waliokamatwa maeneo mbalimbali ya nchi. Chama kinafuatilia kwa makini yanayoendelea na kitaendelea kuuhabarisha umma kila linalojiri hatua kwa hatua.”


Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali