Othman akerwa na Wasira, Mbeto kupotosha kuzuiwa kwao Angola

Mweenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Masoud Othman akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Masoud Othman Masoud, ametaka hatua zichukuliwe dhidi ya viongozi wanaopotosha taarifa kuhusu kuzuiwa kwao nchini Angola.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Masoud Othman, ameeleza kushangazwa na upotoshaji uliofanywa na baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu kilichowatokea nchini Angola.
Othman ameenda mbali zaidi na kutaka mamlaka zinazowasimamia ziwachukulie hatua kwa kile alichoeleza kuwa upotoshaji walioufanya unaipaka matope Serikali.
Othman, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, viongozi wengine wa ACT-Wazalendo, na wastaafu wa mataifa mengine ya Afrika walizuiwa juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Quatro de Fevereiro nchini Angola walikokwenda kwa Mkutano wa Jukwaa la Demokrasia Afrika (PAD).
Baada ya kuzuiwa viongozi hao, Chama cha ACT-Wazalendo kilitoa taarifa ya kushangazwa na ukimya wa Serikali ya Tanzania, huku wakiitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itoe msimamo wa Serikali kuhusu hilo.
Baada ya tamko hilo la ACT-Wazalendo, Ijumaa, Machi 14, 2025, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, akiwa ziarani mkoani Songwe, akizungumza kwenye mkutano wa ndani uliofanyika Vwawa, wilayani Mbozi, alisema hatua ya viongozi hao kuzuiwa wasimtafute mchawi kwa kuinyooshea kidole Serikali.
"Leo nimesoma viongozi walikuwa wanakwenda Angola lakini wamenyang'anywa paspoti huko ni Angola, sio hapa, hapa hatuja wanyang'anya paspoti, na hata ikimaliza muda wake tunawapa, ili waende wanakotaka halafu warudi salama.
"Wamelalamika kwanini Serikali imekaa kimya, kwani sisi tunasimamia Uwanja wa Ndege wa Angola? Uwanja huo unasimamiwa na watu wa Angola, pia huenda walikuwa na jambo lao ambalo wanalilitilia shaka, wangeuawa tungesema kwanini wamewaonea watu wasiokuwa na hatia," alisema Wasira.
Baada ya maelezo hayo ya Wasira, leo Jumapili, Machi 16, 2025, Masoud akiwa na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, wamekutana na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Magomeni jijini Dar es Salaam kuzungumzia sakata hilo.

Katika maelezo yake, Othman hakutaka kuzungumza suala hilo zaidi kwa kuwa alishafanya hivyo pamoja na chama kwa kutoa taarifa, lakini kitendo cha Wasira, kupotosha umma, akiwemo Mwenezi wa CCM Zanzibar, Hamis Mbeto, kimemfanya kujitokeza tena.
Amesema upotoshaji huo unaipaka matope hata Serikali na kwamba viongozi hao wanapaswa kuchukuliwa hatua na mamlaka zinazowasimamia.
"Upotoshaji wao umeipaka matope Serikali na kuwafadhaisha wananchi, wanapaswa wachukuliwe hatua kwa sababu wamekwenda kinyume na wajibu wao na huo ndio wito wetu," amesema.
Amerejea kile kilichoelezwa na Mbeto kwamba kuzuiwa kwao pengine ni kwa sababu hawakufuata utaratibu wa kusafiri, akifafanua maana yake Makamu wa Kwanza wa Rais hajui itifaki za kwenda nje ya nchi.
Masoud ameeleza taratibu zote za kusafiri kama kiongozi amezifuata, ikiwemo kuomba ruhusa kwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, na amejibiwa kwa maandishi.
Utaratibu mwingine uliofanyika, amesema ni kutoa taarifa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Idara ya Usalama wa Taifa kwa ajili ya kupeleka watangulizi, na hiyo ilifanyika.
Amesema timu ya watangulizi ilikwenda siku tano kabla ya mkutano na ilifika hadi eneo ambalo mkutano huo ulipaswa kufanyika.
"Niwahakikishie Watanzania kwamba watangulizi walipelekwa na walikwenda hadi kwenye kituo ambacho tulikuwa tufanyie mkutano.
"Taratibu zote zilizostahili zilifanywa kama makosa yalifanywa na Angola, kwa sababu tulipofika, taratibu hata kama walikuwa na tatizo hawakupaswa kukaa kimya, walipaswa kutwambia," amesema.
Masoud amesema hakuna aliyeelezwa kinachofuata wala sababu ya kuzuiwa.
Hata hivyo, amesema haoni kama kuna uhusiano wa siasa za Tanzania katika hatua ya kuzuiwa kwao kuingia nchini Angola.
"Mimi niseme ukweli kabisa, sioni kwa namna gani Serikali inaweza kuwa na maslahi na kuzuia masuala yaliyokuwa yanaendelea Angola wasifanyike," amesema.
Amesisitiza kwa mazingira yalivyokuwa hawana sababu ya kuona kwamba kilichotokea Tanzania inahusika kwa namna yoyote.
"Hatuna sababu ya kuona kwamba Tanzania inahusika, lakini mazingira yaliyomo Angola yanatosha kuona kwamba hiki kinachoendelea kimefanyika," amesema.
Kwa upande wa Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, amesema baada ya yaliyotokea hawakusikia chochote kutoka serikalini kujua nini sababu hadi viongozi kuzuiwa.
"Tunaitaka Serikali itoke hadharani na kueleza nini kimetokea na tunataka Balozi wa Tanzania nchini Angola aitwe kueleza kilichotokea," amesema.
Kwa kuwa Rais wa Angola ndiye Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) kwa sasa, amesema wana mashaka kama anaweza kuendelea kuwa msimamizi wa ajenda ya demokrasia na heshima kwa viongozi wa Afrika.
"Tunawaomba viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) watafakari nafasi waliyompa Rais wa Angola kwamba hataimudu nafasi hiyo, ni muhimu apatiwe mtu anayeonyesha mfano wa kusimamia ajenda ya demokrasia," amesema.
Jukwaa la PAD lilianzishwa mwaka 2023 na huo ulikuwa mkutano wake wa tatu na mara nyingi hukutanisha wadau kujadili demokrasia.
Mwaka 2023 wadau hao walikutana Poland, mwaka 2024 walikutana Afrika Kusini, na mwaka huu wanakutana Angola.
"Hili ni jukwaa muhimu tunalolihitaji kwa wanaoitakia mema Afrika kwenye masuala ya siasa," amesema Dorothy.