Prime
No reforms No Election yashika mitandao, Serikali yatoa neno

Dar es Salaam. Sasa unaweza kusema kampeni maarufu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya No Reforms, No Election (Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi) sasa imechukua sura mpya baada ya kutawala katika mitandao ya kijamii maarufu hapa nchini.
Katika mitandao ya kijamii makundi mbalimbali yanahamasisha kupaza sauti za kampeni hiyo kwa kuchapisha ujumbe na kutoa maoni (Comments) ya No Reforms, No Election pale ukurasa fulani unapokuwa umechapisha maudhui yake yoyote.
Haijalishi ni ukurasa wa nani, iwe wa vyombo vya habari, kampuni, matangazo sehemu kubwa ya maoni ni No Reforms, No Election na wengine wanafupisha kwa kuandika NRNE.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya viongozi wamelazimika kuzuia maoni katika akaunti zao, huku hamasa zikiendelea kwa kampeni hiyo kuhamia katika mitandao mingine ya kijamii kama TikTok na mingineyo.
Maajabu ni kuwa kampeni hiyo kwa upande wa mtandaoni haisukumwi na viongozi wa Chadema, hata hivyo huenda wafuasi na wapenzi wa chama hicho ndiyo vinara.
No reforms, No Election imeenda mbali zaidi kwani imemgusa hadi msanii wa Nigeria Chellaboi ambaye amekuja nchini hivi karibuni na kushangazwa na ukurasa wake kumiminika maoni yanayohusu kampeni hiyo.
Katika ukurasa wake, Chellaboi amechapisha video akiomba Watanzania wamfafanulie hiyo No Reforms, No Election ni kitu gani akihoji kinamchanganya kwani ameona ‘komenti’ nyingi za aina hiyo katika ukurasa wake.
“Je, kuna kitu natakiwa kufahamu katika ukurasa wangu upande wa maoni maana sielewi, mimi ni msanii, sifanyi siasa wala sijui chochote kihusucho siasa lakini komenti zinaniogopesha naona tu No reforms, No Election na mpaka sasa nimeshaziona nyingi je kuna kitu Tanzania mnataka kuniambia tafadhali, nini kinaendelea mimi siyo mwanasiasa mimi ni msanii,” amehoji.
Hata hivyo, baada ya video hiyo aliyoichapisha jana akielezea kushangazwa watu takribani watu 2,000 walitoa maoni yao na sehemu kubwa ilikuwa ni kuhusu ujumbe wa No Reforms, No Election, huku wengine wakisema “Tunathamini muziki wako mzuri lakini No Reforms, No Election.”
Mchambuzi wa siasa, Ramadhani Manyeko amesema inawezekana baadhi ya watu wachache wamedukua mfumo wa mitandao hiyo na kupenyeza ujumbe wa No Refoms, No Election’ ikimaanisha Bila mabadiliko, Hakuna uchaguzi.
“Katika hali ya kawaida katika kundi la watu 100, haiwezekani wote mkawa mna mawazo yanayofanana No Reforms, No election, hapo kuna kitu kimefanyika. Kinachotakiwa weledi na taaluma inapaswa kuongezeka kwa TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) katika kudhibiti matumizi ya mtandao,” amesema.
Manyeko ameongeza kuwa “Hii inatupa ishara kwamba TCRA wanapaswa kuongeza nguvu zaidi katika kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya mtandao. Ujumbe ule umetengezwa na njia ya aina fulani ya inayolenga kuhamasisha maandamano kwa njia ya mtandao,” amesema.
Chadema yasema wameeleweka
Akizungumza na Mwananchi, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Bara John Heche amesema watu wasione kero lakini tafsiri yake Watanzania wameelewa na wamefanikiwa kufikisha elimu.
"Kinachoendelea mitandaoni tumefanikiwa kupitia kampeni yetu ya No Reforms, No Election. Maana yake Watanzania wameelewa na wanataka mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi ili wapate viongozi waliokubalika kupitia kura zao," amesema.
Heche amesema kwa muda mrefu mifumo ya uchaguzi haitendi haki na wanaosimamia chaguzi wanapoka uamuzi wa kura zinazopigwa na wananchi na hiyo yote inatokana na mifumo mibovu iliyopo.
"Wananchi wanapotoa sauti kama hiyo tafsiri yake wameelewa kampeni hii na wanahitaji kweli mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi na wakubwa wanapaswa kusikiliza sauti hizo," amesema Heche.
Kampeni ya No Reforms, No Election inayotekelezwa na viongozi wa chama hicho kwa kupita kufanya mikutano ya hadhara kutoa elimu kwa umma kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi ndipo Uchaguzi 2025 uweze kufanyika ilizinduliwa Machi23, 2025 mkoani Mbeya.
Imekuwa ikifanyika kwa mfumo wa kikanda kulingana na utawala wa chama hicho lakini inakusudiwa kufika mikoa yote, ingawa kuna nyakati viongozi wake wamekuwa wakipitia misukosuko ya hapa na pale ya kushikiliwa na jeshi la Polisi.
Kauli ya Serikali
Alipoulizwa kuhusu wimbi hilo la maoni ya No Reforms, No Election mitandaoni, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amejibu "Watu wameamua kufanya hivyo, tutafanyaje," amesema.
Ingawa katika maelezo yake aliwatahadharisha wanaofanya mchezo huo akidai hauna tija na 'upuuzi' zaidi ya kupoteza muda wao.
"Watu wajiepushe na kampeni zisizokuwa na tija, watumie mitandao kama fursa ya kujifunza teknolojia mpya, wanapaswa kutambua na kujua kutumia mitandao vibaya ni kupoteza rasilimali fedha kwa kuwa wanatumia bando," amesema.
Katika maelezo yake Msigwa amesema badala ya kupoteza muda kuendesha kampeni hizo watumie nafasi hiyo wajielekeze kujenga nchi yao.
"Kinachoendelea kwenye mitandao ni upuuzi. Huu ni upuuzi unaoendelea Watanzania wajielekeze kujenga nchi yao. Huwezi kuendesha kampeni ya kuzuia Uchaguzi wakati nchi imejiwekea kalenda yake," amesema Msigwa.