Chadema Njombe yaandaa ‘nyama choma’ kuelimisha wananchi No reforms, no election

Muktasari:
- Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Njombe kimeandaa siku maalumu ya nyama choma kama sehemu ya mkakati wa kutoa elimu kwa umma kuhusu ajenda ya No reforms, no election.
Njombe. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Njombe kimeandaa siku maalumu ya kuchoma nyama, kwa lengo la kutoa elimu kwa wanachama wake kuhusu ajenda ya chama hicho ya No reforms, no election.
Tukio hilo limepangwa kufanyika Juni 14, 2025 ikiwa ni sehemu ya juhudi za chama hicho za kurejesha mshikamano na kuimarisha uelewa wa wanachama kuhusu ajenda ya No reforms, no election (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi).
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 5, 2025 na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Njombe, Seth Vegula alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Halmashauri ya Mji wa Makambako, wilayani Njombe.
Amesema baadhi ya wanachama bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu ajenda muhimu ya chama, jambo lililosababisha sintofahamu hata baadhi yao kukihama chama.
“Kuna wanachama wengi bado hawajafahamu vyema ajenda hii. Sisi tumeona ni vyema kutumia siku hii ya nyama choma kutoa elimu kwa wanachama wetu kuhusu kwa nini Chadema inasisitiza ajenda hiyo,” amesema Vegulla.
Mbali na kutoa elimu ya kisiasa, siku hiyo pia wamepanga kusajili wanachama wapya wa chama na kugawa kadi za kidijitali bila malipo.
“Pia, tutafanya changizo la kujenga ofisi ya chama katika jimbo la Makambako. Hii ni sehemu ya mkakati wetu wa kuimarisha umoja baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa ndani ya chama,” ameongeza Vegulla.
Kwa upande wake, mjumbe wa kamati ya utendaji na ujenzi wa jimbo la Makambako, Antony Mdekwa amesema, "waliohama chama walikuwa wamevurugwa na vyama vingine, lakini tukio hili litaturudisha pamoja kama Chadema," amesema Mdekwa.
Naye mmoja wa wanachama wa Chadema jimbo la Makambako, Christopher Mhadze ameeleza kuwa tukio hilo, litasaidia kuleta mshikamano, kuibua ari mpya na kujenga umoja miongoni mwa wanachama.