Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwisho wa ubishi Mbowe, Lissu Chadema

Muktasari:

  • Baraza Kuu la Chadema limewateua Freeman Mbowe Tundu Lissu na Charles Odero kuwania uenyekiti wa chama hicho, katika uchaguzi utakaofanyika kesho Jumanne, Januari 21, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Baada ya minyukano ya takriban mwezi mmoja, hatimaye kesho Jumanne, Januari 21, 2025 ni mwisho wa ubishi wa nani kati ya Freeman Mbowe,Tundu Lissu au Charles Odero atakayechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Hakuna yeyote kati ya wafuasi wa Lissu au Mbowe, wanaoamini mgombea wao atashindwa katika kinyang’anyiro hicho. Huo ndio ubishi ambao mwisho wake utakuwa katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Ingawa nafasi ya uenyekiti wa Chadema inawindwa pia na Charles Odero, ni Lissu na Mbowe ndio wanaotajwa kuwa karibu zaidi na ushindi, hata kusababisha makundi mawili ndani ya Chadema yanayowaunga mkono.

Wafuasi wa Lissu wanampinga Mbowe kwa hoja kuwa, wanahitaji mabadiliko baada ya miaka 21 ya uongozi wake bila mafanikio ya kushika dola.

Lakini, wanaompinga Lissu, wanajenga hoja, hatoshi kuwa mwenyekiti kwa kuwa anakibagaza chama hicho na kuweka hadharani siri za vikao nyeti.

Kila upande unajitetea kwa namna yake; wale wa Mbowe wanasema ni muhimu aendelee kuongoza,  kwani hawawezi kubadilisha kamanda katikati ya vita.

Wafuasi wa Lissu nao, wanasema kwa aina ya siasa za majira ya sasa, upinzani unahitaji kiongozi anayeweza kuishinikiza dola na kusukuma mageuzi kwa nguvu zote.

Vita ya ushindi wa uenyekiti na ubishani uliopo, umesababisha hofu ya kugawanyika kwa chama hicho kikuu cha upinzani baada ya uchaguzi. Dalili za hilo ni lugha chafu zinazotumika na kambi ya kila upande dhidi ya mwingine.


Mbowe asisitiza umoja

Katikati ya minyukano ya makundi yanayowaunga mkono wagombea hao wawili, Mbowe amesema wapo watu nje ya chama hicho wanaoangalia upinzani unaoendelea kwa jicho la husuda na wivu, kiasi cha kutamani chama hicho kivunjike vipande vipande.

"Tumekuja Dar es Salaam sio kupaniana, tumekuja kuyajenga kwamba chama hiki tutakijenga, tutakipanga ili mwishowe chama chetu kibebe ndoto za Watanzania," amesema Mbowe alipohutubia kikao cha Baraza Kuu la chama hicho leo Jumatatu.

Kwa mujibu wa Mbowe, Chadema ni kubwa kuliko tofauti za wanachama wake, huku akiamini wajumbe watatoka ukumbini wakiwa wamoja.

Mwenyekiti huyo anayemaliza muhula wake wa uongozi kesho, aliwataka wanachama wasitoe nafasi kwa yeyote anayetaka kuipasua Chadema, badala yake waonyeshe wanavyoweza kuijenga taasisi ndani ya tofauti zao.

"Siku ambayo dunia nzima inasubiri, watesi wetu wanaisubiri, marafiki zetu wanaisubiri, twendeni tukawaonyeshe kwamba Chadema ni mpango wa Mungu na huu ni mpango wa Mungu," amesema.

Amesisitiza wanachama wa chama hicho wataendelea kuwa familia moja, licha ya mivutano midogomidogo iliyopo.

Ni 50 kwa 50

Kile kinachosemwa kuwa ‘dalili ya mvua ni mawingu,’ hakiakisi ushindani wa Lissu na Mbowe, hakuna na wingu zito wala jua kali, nafasi ya ushindi wa wawili hao imebaki nusu kwa nusu, kama inavyoelezwa na Dk Revocatus Kabobe.

Dk Kabobe aliyebobea katika sayansi ya siasa, amesema wagombea hao wana nguvu na ushawishi unaofanana au kukaribiana ndani ya chama hicho.

“Wote hawa wanakaribia kuwa na ushawishi sawa ndani ya chama na hilo limejionesha kwenye kampeni zao na mgawanyiko uliopo hasa kwenye chaguzi za mabaraza zilizopita,” ameeleza.

Hata hivyo, ameeleza kwa hali ilivyo hatarajii mshindi apatikane kwa kumzidi mwenzake kura nyingi zaidi kama ilivyozoeleka.

“Utakumbuka tangu Mbowe apate nafasi ya uenyekiti mara zote kwenye chaguzi ameshinda kwa zaidi ya asilimia 95. Zamu hii naona tofauti kubwa kwenye hili,” amesema Dk Kabobe.

Mwanazuoni huyo alikwenda mbali zaidi ni kueleza hadi sasa haoni upande wenye uhakika wa kushinda kulingana na hali halisi ilivyo.

“Kambi hizi mbili zimevuta sana hisia za wapiga kura. Kwa hiyo tutarajie yeyote kati yao kuibuka mshindi ingawa kwa tofauti ndogo sana ya kumshinda mwenzake,” amesema.

Miaka 30 ya Chadema

Pamoja na mkutano mkuu huo kumaliza ubishi, kesho Jumanne  pia ni kumbukizi ya miaka 30 ya kuzaliwa kwa Chadema, kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Mnyika jana Jumatatu, aliandika ni zaidi ya siku ya mkutano mkuu wa Chadema, kwa kuwa ni kumbukizi ya chama hicho kupata usajili kamili mwaka 1993 baada ya kuasisiwa 1992.

Kwa mujibu wa Mnyika, Januari 21 ni siku ya Chadema inayobebwa na ujumbe wa ‘Stronger Together’.

“Tunapoelekea kuadhimisha siku hii ni rai yangu kuwa leo tuwakumbuke kwa kuwataja kwa majina na kuwaombea wote waliouawa katika mapambano ya kudai haki tangu kuanzishwa kwa Chadema,” aliandika.

Katika chapisho lake hilo, aliwataja baadhi ya watu hao ni Ally Kibao, Alfonce Mawazo na Daudi Mwangosi.

Mkutano utakavyokuwa

Akitangaza ratiba ya mkutano mkuu huo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema utaanza rasmi saa 5:00 asubuhi na ajenda zote zitarushwa mubashara.

Katika mkutano huo kwa mujibu wa Mrema, watapatikana viongozi wa nafasi ya uenyekiti wa chama hicho taifa na makamu wake bara na Zanzibar.

Pamoja na wajumbe halali, Mrema amesema wageni zaidi ya 50 watashiriki mkutano huo wakiwemo mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali na viongozi wa kisiasa kutoka nje ya nchi.

Amesema baada ya mkutano huo, keshokutwa Jumatano kitafanyika kikao cha baraza kuu ambacho pamoja na mambo mengine, kitachagua wajumbe wanane wa kamati kuu.

Sambamba na hilo, alieleza ni kikao hicho pia, ndicho kitakachopendekeza jina la Katibu Mkuu wa Chadema, atakayerithi nafasi ya Mnyika. Hii ni kama Mwenyekiti atakayeshinda ataamua kubadili mtendaji huyo mkuu ama kuendelea na aliyepo.

‘Uteuzi wajumbe kamati kuu

Moja ya mijadala iliyoteka hisia za watu wengi kwa siku mbili hizi,  ni uteuzi wa wajumbe wa kamati kuu walioteuliwa na kamati kuu. Msingi wa mjadala huo ni madai kwamba  wanaomuunga mkono Lissu wamefyekwa huku wale wa Mbowe wakiachwa.

Miongoni mwa wanaopigiwa ‘debe’ warudishwe ni Twaha Mwaipaya, Rose Mayemba na Askofu Maximilian Machumu maarufu ‘Askofu Mwanamapinduzi'.

Baada ya mijadala hiyo, Mnyika katika majibu yake kwa mmoja wa wachangiaji kwenye mtandao wa X alimjibu hoja hiyo akisema: “Tumejifunza katika mikutano mikuu ya mabaraza ya Bawacha, Bavicha na Bazecha athari ya kupitisha wagombea wengi bila kufanya uchujaji.”

Amesema vikao vya uchaguzi vimefanyika kwa siku mbili mpaka tatu. Hivyo Kamati Kuu katika hatua hiyo,  imeamua kutumia mamlaka yake ya usaili, uchujaji na uteuzi kwa ukamilifu.

Amesema vigezo vilivyotumika ni kwa mujibu wa kanuni ya 7.5 hususani 7.5.1 mpaka 7.5.4 baada ya wagombea kupewa fursa ya kutoa maelezo yao mbele ya Kamati Kuu na pia Kamati Kuu kupitia maelezo yao waliyojaza kwenye fomu za kugombea.

“Kwa makundi haya mawili ya wanaume na wanawake Tanzania Bara ambayo ndio nimesoma uteuzi umejadiliwa sana kazi sasa imebaki kwa Baraza Kuu kwenye wagombea wanane kwa kila kundi kuchagua wajumbe watatu na matokeo ya ujumla kuzingatia pia uwakilishi wa watu wanaoishi na ulemavu,” amesema Mnyika.

Wagombea wanaume waliopitishwa kuwania nafasi tatu kwa upande wa bara ni Bashir Abdallah Selemani na Daniel Ngogo.

Wengine ni John Pambalu, Nyamatari Tengecha, Patrick Sosopi, Patrick Assenga, General Kaduma na William Mungai.

Kwa upande wa nafasi za wanawake bara ni, Dorcas Mwilafi, Ema Boki, Grace Kiwelu, Josephine Lemoyan, Monica Nsaro, Pasquina Lucas, Rehema Mkoha na Sina Manzi.

Katika nafasi za watu weye ulemavu, taarifa imeeleza wamepitishwa Salum Barwani, Amina Sollah na Sara Katanga.

Kwa upande wa nafasi za wanawake Zanzibar waliopitishwa ni Time Suleiman, Zeudi Abdulahi na wanaume ni Nuhu Khamis na Yahya Omar.