Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fukuto wagombea kamati kuu Chadema wakikatwa

Shughuli ya uhakiki wa wajumbe kutoka mikoa mbalimbali wanaoingia kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ikifanyika nje ya Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Januari 20, 2025.

Muktasari:

  • Wakati Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akisema usaili na uteuzi wagombea wa kamati kuu ulifuata katiba na kanuni za chama, baadhi ya waliokatwa wamesema utaratibu haukufuatwa na wamekata rufaa.

Dar es Salaam. Kufuatia orodha ya wagombea nafasi za kamati kuu ya Chadema walioteuliwa Januari 19, 2025, hisia za uonevu zimeibuka, ambapo baadhi wameelekeza lawama kwa kambi zinazosigana katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema usaili na uteuzi uliofanywa na kamati kuu Januari 19, 2025 ulifuata utaratibu uliopo katika katiba na kanuni za chama na kutumia demokrasia kama nyenzo ya maamuzi katika siasa.

Uchaguzi mkuu wa Chadema unaokwenda kukamilika kesho Januari 21 jijini Dar es Salaam kwa kuwachagua wagombea uenyekiti na makamu mwenyekiti umeibua mvutano mkali kati ya Mwenyekiti Freeman Mbowe na makamu wake, Tundu Lissu.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema Januari 19, 2025 imesema wagombea waliotolewa ni kwa mujibu wa Kanuni ya 7.2.6.

Wagombea hao wamegawanywa katika makundi, zikiwamo nafasi za wanaume Bara ambazo walioteuliwa ni Bashir Abdallah Selemani, Daniel Natal Ngogo, John Pambalu, Nyamatari Tengecha, Patrick Kapurwa Sosopi, Patrick Assenga, General Kaduma na William Mungai.

Kwa nafasi za wanawake wamo, Dorcas Mwilafi, Ema Boki, Grace Kiwelu, Josephine Lemoyan, Monica Nsaro, Pasquina Lucas, Rehema Mkoha na Sina Manzi.

Kwa nafasi za wenye ulemavu wamo Salum Barwani, Amina Sollah, na Sara Katanga.

Kwa upande wa Zanzibar, wanawake walioteuliwa ni Time Ali Suleiman na Zeudi Mvano Abdulahi, huku Nuhu Jaffar Khamis na Yahya Alawi Omar wakiteuliwa kwa upande wa wanaume.

Wakitoa maoni yao mitandaoni, baadhi ya wadau na makada wa Chadema wamekosoa usaili huo, wakisema umefanywa kwa upendeleo.

Mdude Nyagali ambaye ni kada wa chama hicho anayeishi mkoani Songwe ameandika katika ukurasa wake wa X, akimzungumzia Sadrick Malila kutoka mkoani Rukwa aliyekatwa.

“Huyu mzee amekuwa makamu mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, amekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Rukwa kwa miaka 10,  ana Master’s degree (shahada ya uzamili) ya uchumi, ni mfanyabiashara na mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoa wa Rukwa.

“Kwa CV yake hiyo amekatwa kugombea kamati kuu. Inasikitisha,” ameandika.

Mgombea aliyeibua hisia zaidi ni aliyekuwa Katibu mwenezi wa Baraza la Vijana (Bavicha), Twaha Mwaipaya, ambapo baadhi ya wadau wamehusisha kuenguliwa kwake na msimamo wake wa kumuunga mkono mgombea uenyekiti, Tundu Lissu.

Hata hivyo, Mwaipaya alipoulizwa na Mwananchi amesema haoni kama hicho ndio kigezo kilichotumiwa na kamati kuu.

“Inawezekana imevuta hisia za watu wengi kwa sababu waliomuunga mkono Lissu wengi wamekatwa lakini sidhani kwamba kamati kuu imefanya uamuzi kwa mrengo,” amesema.

Tayari Mwaipaya ameshakata rufaa kupinga kuenguliwa kwake, akisema hawakuelezwa sababu ya kukatwa majina yao.

“Hatukupewa sababu zozote kwa nini hatujateuliwa. Kama majina ya kuteua watu yalitoka basi muda wa kutoa sababu za ambao hawajateuliwa ulikuwepo, kwa hiyo hawakutoa hiyo sababu.

“Tayari tumeshawasilisha rufaa yetu kwenye ofisi ya katibu mkuu kwamba hatujateuliwa na bado hatujapewa sababu. Baraza linakaa leo, ikipendeza lisikilize rufaa zetu,” amesema.

Mwingine aliyekata rufaa ni Rose Mayemba aliyesema, “kwa mujibu wa Katiba ya chama, rufaa inakatwa ndani ya siku 14 toka siku ya maamuzi, tuko ndani ya muda, barua tayari ziko ofisi ya katibu mkuu, tunaamini uchaguzi hautafanyika mpaka tusikilizwe kama katiba inavyoelekeza.”

Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu rufaa hizo, John Mrema amesema kwa utaratibu wa Chadema baada ya wagombea kuenguliwa, katibu mkuu atawaandikia barua rasmi ya sababu za kuwaengua.

Kwa mujibu wa Mrema, mfululizo wa vikao unaowakabili viongozi kwa sasa umesababisha kiongozi huyo ashindwe kuwaandikia barua hiyo wagombea hao jana, lakini wataandikiwa.

Alisema wanayo nafasi ya kukata rufaa zinazopaswa kusikilizwa na baraza kuu, bahati mbaya tayari baraza hilo linaendelea na kikao chake leo.

Alipoulizwa anadhani muda uliobaki unatosha kwa walalamikaji kukata rufaa, Mrema amesema wanayo nafasi hiyo, ingawa hawezi kuwasemea.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu ameandika katika ukurasa wake wa X akimweleza Mwaipaya kama mchapa kazi.

“Kwa miaka mitano niliyofanya nawe kazi, nimekufahamu kama kijana mwenye commitment (jitihada) ya hali ya juu katika kuleta mageuzi.

“Nimetembea nawe magereza yote nchini kuwaona, kuwafariji na kuwatia moyo wafungwa wa kisiasa baada ya wewe kutoka gerezani ulikowekwa siku 133. Nimeumia sana kusikia umekatwa kugombea ujumbe wa kamati kuu.”

Kada wa chama hicho, Godbless Lema ameandika X akisema, “Twaha Mwaipaya jina lako limekatwa? Nimeumia kama nimefiwa na mzazi, wewe ni kijana mwema sana na committed kwa mageuzi.”

Akizungumzia uteuzi huo, Clement A Manang ameandika katika ukurasa wake wa X akimwambia Katibu Mkuu Mnyika kuwa, uliofanyika ni ubabe.

“Mkatoliki mwenzangu, juzi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa tulikatwa kibabe tukalalamika sana na kulaani, leo wagombea ndani ya chama wamekatwa kibabe bila sababu za msingi mheshimiwa tunaelekea wapi? Nani katupiga upofu?” amehoji. 


Mnyika ajibu

Akijibu malalamiko kupitia ukurasa wake wa X, Mnyika amesema uteuzi huo, ulifuata utaratibu uliopo katika katiba na kanuni za chama na kutumia demokrasia kama nyenzo ya uamuzi.

“Rejea Katiba ya chama ibara ya 7.7.12(d) nafasi za ujumbe wa Kamati Kuu za kugombewa kwenye Baraza Kuu ni nane tu. Kwa upande wa Tanzania Bara ni tatu wanaume na tatu wanawake.

“Waliorudisha fomu kwa wanaume Bara walikuwa 25 na wanawake 11.  Hawa ni nje ya wagombea kutoka Zanzibar na kundi la watu wanaoishi na ulemavu,” ameandika Mnyika akimjibu Clement A Manang.

Amesema wamejifunza katika mikutano mikuu ya mabaraza ya Bawacha, Bavicha na Bazecha athari ya kupitisha wagombea wengi bila kufanya uchujaji.

Amefafanua kuwa vigezo vilivyotumika ni kwa mujibu wa Kanuni ya 7.5 hususani 7.5.1 mpaka 7.5.4 baada ya wagombea kupewa fursa ya kutoa maelezo yao mbele ya Kamati Kuu na pia Kamati Kuu kupitia maelezo yao waliyojaza kwenye fomu za kugombea.

“Kwa makundi haya mawili ya wanaume na wanawake Tanzania Bara ambayo ndio nimesoma uteuzi umejadiliwa sana kazi sasa imebaki kwa Baraza Kuu kwenye wagombea wanane kwa kila kundi kuchagua wajumbe watatu, na matokeo ya ujumla kuzingatia pia uwakilishi wa watu wanaoishi na ulemavu,” amesema.