Msigwa akata  rufaa kupinga matokeo ya uchaguzi Nyasa, Chadema wamjibu

Aliyekuwa mgombea uenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa.

Muktasari:

  • Aliyekuwa mgombea uenyekiti wa kanda ya Nyasa Mchungaji Peter Msigwa amedai kuhujumiwa katika mchakato huo uliogubikwa na vitendo vya rushwa.

Iringa/Dar. Aliyekuwa mgombea uenyekiti wa Kanda ya Nyasa ya Chadema, Mchungaji Peter Msigwa amekata rufaa katika chama hicho, akidai ushindi alioupata Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ haukuwa halali.

Hata hivyo, wakati Msigwa akisema hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema kama kweli Msigwa amekata rufaa na kufuata mfumo unaotakiwa, rufaa yake itasikilizwa na kutolewa uamuzi, kwa sababu Chadema ni chama kinachoheshimu demokrasia.

“Bahati mbaya kama mtu amekata rufaa halafu anaanza kuzungumza mambo ya rufaa kabla haijafika alikokata rufaa ni bahati mbaya, lakini kwa hatua ya sasa kama amekata tusubiri uamuzi wa rufaa yake kwa mujibu wa taratibu,” amesema Mrema.

Akizungumza leo Jumatatu Juni 3, 2024 kwenye mkutano na waandishi wa habari alioufanyia nyumbani kwake Iringa Mjini, Msigwa amedai  kuwa mifumo ya chama imetumika kumhujumu ili asishinde, kitendo ambacho amesema kitaifanya Chadema kukosa uhalali wa kuikosoa CCM.

Amedai kulikuwa na mbinu chafu dhidi yake. Mchungaji Msigwa aliyekuwa anatetea uenyekiti kwa awamu nyingine, alishindwa mbele ya mpinzani wake Sugu kwa tofauti ya kura mbili katika uchaguzi uliofanyika Mei 29, 2024 Makambako mkoani Njombe.

“Nimekata rufaa kwa chama changu kuwa makatibu watatu wa mabaraza walizuiwa kupiga kura, ukiangalia kura zangu zilizoongezeka na kufikia sita, lakini wajumbe watatu walizuiwa.

“Rufaa yangu imefafanua mambo mengi sana yaliyokiukwa katika uchaguzi hata kufutwa kwa uchaguzi wa Njombe, ulikuwa mkakati wa kunihujumu ili nisishinde, lakini nimegundua sikuwa nashindana na mpinzani wangu peke yake, bali alikuwa ana nguvu nyingine nyuma yake,” amedai Msigwa.

Katika maelezo yake, amesema alijipanga ipasavyo ikiwamo kufanya kampeni za wazi za ushindani na hoja, akizifanya kwa uaminifu mkubwa pasipo uoga ndio maana aliasisi mdahalo baina yake na Sugu.

“Mimi uchaguzi sikushindwa na siwezi kushindwa,” amesisitiza Msigwa.

Mwananchi Digital limemtafuta Sugu kuzungumzia suala hilo na amesema;

“Sijamsikia ingawa najua alikuwa na mkutano na waandishi wa habari, lakini niseme siwezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa, nina kazi nyingi.”

Katika maelezo yake, Mchungaji Msigwa amemtuhumu pia msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo, John Mrema kuwa alikuwa anamfanyia kampeni Sugu kinyume cha utaratibu.

Amedai Mrema alikuwa akiwaambia wajumbe kuwa ametumwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anataka Sugu awe mwenyekiti wa Nyasa.

“Mwanzo niliandika mmoja wa wasimamizi wa uchaguzi (John Mrema), angeondoka ili kupisha mchakato huo. Kama Chadema tunalalamikia Serikali ya CCM kwamba wasimamizi wa uchaguzi hawatendi haki, basi tulitakiwa tuwe mfano wa kuigwa, lakini katika chaguzi zetu haki haitendeki.

“Kama mimi mjumbe wa kamati kuu natoa malalamiko haya halafu hayasikilizwi ndani ya Chadema, nani atasikiliza ndani ya nchi yetu,”amesema.

Mbali na hilo, Msigwa amedai kuna watu walianza kuleta vurugu mbele ya msimamizi wa uchaguzi huo, Benson Kigaila (naibu katibu mkuu-bara), lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na kiongozi huyo.

“Hali ile inaleta shaka na ina harufu ya uvundo wa ukiukwaji mkubwa wa haki ndani ya Chadema ambacho kinatakiwa kiwe mstari wa mbele katika demokrasia. Haya malalamiko sikuanza leo hata katika vikao nimeyasema niliandika barua Katibu Mkuu (John Mnyika), ambaye alikiri kuyapokea, lakini barua haikujibiwa.

“Jina la mwenyekiti (Freeman Mbowe) limetumika sana kwamba yeye anapanga safu yake, nilisema tangu mwanzo kuwa wanamchafua kwa kumshusha katika ngazi za chini ya kuwapigia simu na kutoa maelekezo ya nani achaguliwe, wanamchafua tu mwenyekiti wetu,” amesema.

Msigwa amedai kuwa vitendo vya viashiria vya rushwa vilikuwepo pia katika uchaguzi huo.

Amedai watu walipokea Sh500,000 hadi Sh1 milioni, lakini hawezi kulizungumzia kwa undani suala hilo wala asiulizwe maswali.

“Haya ni mambo ya aibu kwa chama chetu kilichojitabanisha kwa kukosoa ufisadi na kupinga rushwa, sasa kama ndani ya chama kuna rushwa kubwa namna hii, tunaweza kusimama na kuikosa CCM,” amehoji.

Akijibu hoja ya kuhusu kumpigia kampeni Sugu, Mrema amesema, “si amekata rufaa maana yake amewasilisha na ushahidi wa suala hili, nikianza kujibu sasa ni kama vile najibu rufaa yake, kama ana ushahidi nitafurahi akauweka katika rufaa yake.”

Hata hivyo, Mrema amemtaka Mchungaji Msigwa kukumbuka maneno aliyoyatamka baada ya uchaguzi huo kuisha ambapo alikiri mchakato kwenda vizuri na yeye mwanademokrasia atakwenda kujipanga katika nafasi zingine.