Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Migogoro yatikisa uongozi ndani ya vyama vya upinzani




Mapengo ya uongozi yanayoendelea kujitokeza ndani ya baadhi ya vyama vya upinzani yameanza kuibua maswali kuhusu uimara wa taasisi hizo katika kipindi ambacho vinaendelea kujipanga kisiasa.

Kujiuzulu kwa viongozi, kuhama kwa baadhi yao kwenda vyama vingine na wengine kuomba kujiondoa kwa muda katika majukumu yao, kumeacha nafasi muhimu zikisubiri kujazwa, huku vyama vikisisitiza kuwa vinaendelea kufuata taratibu za kikatiba kuziba mapengo hayo.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi ndivyo vinavyokabiliwa na hali hiyo, baada ya viongozi katika ngazi mbalimbali kuondoka kwa sababu zinazotofautiana. Wapo waliotaja kutoridhishwa na mwenendo wa uongozi ndani ya vyama vyao, huku wengine wakiamua kuhamia vyama vingine vya siasa.

Nafasi zilizoachwa wazi zinagusa ngazi muhimu za uongozi, zikiwamo za wenyeviti wa kanda, makamu wenyeviti, wakurugenzi wa idara, makatibu wa mikoa na wilaya. Katika baadhi ya maeneo, nafasi hizo zinakaimiwa wakati taratibu za uchaguzi au uteuzi zikiendelea, huku nyingine zikisubiri uamuzi wa vikao vya juu vya vyama husika.

Licha ya hali hiyo, viongozi wa vyama hivyo waliozungumza na Mwananchi wanaeleza kuwa hakuna ombwe la uongozi, wakisisitiza kuwa taratibu za kujaza nafasi hizo zinaendelea kwa kuzingatia katiba na kanuni za kila chama. Hata hivyo, kwa NCCR-Mageuzi na CUF, changamoto ya upatikanaji wa fedha imeelezwa kuwa kikwazo kikubwa, hasa pale nafasi zinapohitaji kujazwa kupitia Baraza Kuu au Mkutano Mkuu.

Miongoni mwa matukio yaliyoibua mjadala ni kurejea kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Bara, Joseph Selasini, ndani ya Chadema Mei 22, 2026.

Akitangaza uamuzi huo, Selasini alisema kuondoka kwake Chadema hapo awali kulikuwa "ajali ya kisiasa", huku akiwaomba radhi wote walioathiriwa na hatua aliyowahi kuichukua.

Chama cha Wananchi (CUF), pia kilimpoteza aliyekuwa Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano kwa Umma, Mohamed Ngulangwa, aliyejiuzulu mwezi uliopita.

Katika barua yake, alieleza kutoridhishwa na hatua ya kuzuiwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari uliolenga kulaani kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, iliyovitaka vyama vya siasa kuzingatia taratibu za kufanya mikutano ya hadhara.

Huku chama hicho kikitafakari namna ya kuziba nafasi hizo, Juni 28, 2026 viongozi wengine 16 kutoka Unguja na Pemba walitangaza kujiuzulu, wakieleza kutoridhishwa na mfumo wa uongozi pamoja na migogoro ya mara kwa mara ndani ya chama hicho.

Ndani ya Chadema, mabadiliko ya uongozi pia yameonekana katika baadhi ya kanda. Waliokuwa wenyeviti wa Kanda za Kati, Victoria na Kusini, Devotha Minja, Ezekia Wenje na Aidan Mayala waliondoka katika nafasi zao. Wenje na Mayala walihamia CCM, huku Minja akijiunga na Chaumma.

Kuondoka kwa Devotha Minja pamoja na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Kati, Jackson, kulisababisha Kamati Kuu ya Chadema kuwateua Godbless Lema na Salma Kasanzu kusimamia kwa muda shughuli za kanda hiyo inayoundwa na mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro, wakati taratibu za kupata viongozi wapya zikiendelea.

Mbali na hao, wapo viongozi wa wilaya na mikoa walioondoka mwaka 2025 na kuhamia vyama vingine, huku Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema ikiendelea kutoa maelekezo ya namna ya kujaza nafasi zilizoachwa wazi.


Wasemavyo wachambuzi

Kwa wachambuzi wa siasa, matukio hayo yanaonyesha jinsi migogoro ya ndani inavyoweza kuathiri uimara wa taasisi za kisiasa, hasa pale inaposababisha mabadiliko ya mara kwa mara katika safu ya uongozi. Hata hivyo, viongozi wa vyama husika wanasisitiza kuwa kinachoendelea ni sehemu ya taratibu za kawaida za kisiasa, huku wakiahidi kukamilisha mchakato wa kuziba mapengo hayo kwa kuzingatia katiba za vyama vyao.


Kauli za viongozi

Kauli za viongozi wa vyama hivyo zinaonyesha kuwa pamoja na mapengo yaliyojitokeza, uongozi unaamini taratibu za ndani ndizo zitakazorejesha utulivu na kuhakikisha shughuli za vyama haziathiriki.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Yusuf Mirambo, anasema nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma, Mohamed Ngulangwa, haiwezi kujazwa mara moja kwa sababu Katiba ya chama inahitaji Baraza Kuu kuthibitisha jina la atakayependekezwa.

Anasema jukumu la mwenyekiti ni kupendekeza jina, lakini uamuzi wa mwisho unabaki mikononi mwa Baraza Kuu, hivyo chama hakiwezi kukiuka taratibu zake hata kama kuna uhitaji wa haraka wa kupata kiongozi mpya.

Mirambo pia amefichua kuwa wapo viongozi wawili wa wilaya walioomba kujiondoa kwa muda katika nafasi zao, lakini hadi sasa uongozi haujafanya uamuzi rasmi kuhusu maombi hayo, ukisubiri mamlaka husika kukamilisha mchakato.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Katiba na Sheria wa NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura anasema nafasi ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bara, Joseph Selasini itajazwa, lakini mchakato wake ni mrefu kwa kuwa unahitaji uamuzi wa Mkutano Mkuu wa chama.

Anasema tofauti na nafasi za wilaya zinazoweza kujazwa kwa urahisi, nafasi za juu zinahitaji kuitishwa kwa vikao vya kikatiba vinavyohusisha wajumbe kutoka maeneo mbalimbali nchini, jambo linalohitaji maandalizi na rasilimali fedha.

Akizungumzia uteuzi wa Evaline Munisi kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Sungura anasema bado anaendelea kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, akisisitiza uteuzi wake serikalini haujaondoa hadhi yake ndani ya chama.

Ndani ya Chadema, viongozi wa kanda wanasema mchakato wa kuziba mapengo unaendelea kwa kufuata maelekezo ya makao makuu ya chama. Kaimu Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini, Belchomas Ponera, alisema uchaguzi wa viongozi unaendelea kuanzia ngazi ya matawi, kata, wilaya hadi mikoa, huku utaratibu wa kujaza nafasi za uongozi wa kanda ukisubiri mwongozo wa chama taifa.

Kwa mujibu wa Ponera, msimamo wa chama ni kufanya uchaguzi badala ya kuendelea kukaimisha viongozi kwa muda mrefu, ili viongozi watakaopatikana wapate uhalali kupitia wanachama.

Pamoja na hatua hizo, wachambuzi wanaona changamoto ya kifedha ikiwa moja ya sababu zinazochelewesha kujazwa kwa baadhi ya nafasi za uongozi. Mchambuzi wa masuala ya siasa, Arnold Malik, anasema vyama vingi, hasa vya upinzani, vinakabiliwa na ugumu wa kuendesha shughuli zake kutokana na upungufu wa fedha.

Anasema tatizo hilo haliishii katika kushindwa kuajiri au kujaza nafasi za wataalamu pekee, bali linaathiri pia uwezo wa vyama kuitisha vikao vya maamuzi, kufanya uchaguzi wa ndani na kuendesha shughuli za kila siku.

Kwa mtazamo wake, mfumo wa ruzuku kwa vyama vya siasa unapaswa kuendelea kuimarishwa ili kuvipa uwezo wa kujiendesha kwa ufanisi, kuimarisha demokrasia ya ndani na kushiriki kikamilifu katika ushindani wa kisiasa.

Anasema chama cha siasa kinapokuwa na uwezo wa kifedha huwa na nafasi kubwa ya kuendesha shughuli zake kwa weledi, kujenga taasisi imara na kutoa mchango unaotarajiwa katika maendeleo ya mfumo wa vyama vingi nchini.

Wakati vyama hivyo vikianza taratibu za kuziba mapengo yaliyojitokeza, mtihani uliopo si kupata viongozi wapya pekee, bali kurejesha mshikamano wa ndani na imani ya wanachama. Namna vitakavyoshughulikia migogoro hiyo na kuimarisha uongozi wake ndiyo itakayoamua kama vitaweza kugeuza changamoto hizo kuwa fursa ya kujijenga upya au vitaendelea kukabiliwa na misukosuko inayovuruga utendaji wake.