Prime
Miaka 11 ya ACT - Wazalendo kujenga msingi

Dar es Salaam. Miaka 11 kwa umri wa chama cha siasa, inasadifu utambulisho wa itikadi, sera na falsafa yake, ukuaji na kujenga imani kwa wananchi.
Katika kipindi hicho, kwa mujibu wa wanazuoni wa sayansi ya siasa, aghalabu ni vigumu kwa chama cha siasa kushika hatamu ya uongozi, isipokuwa ni nyakati za kujenga msingi imara.
Ukiacha chama cha siasa, miaka 11 kwa umri wa binadamu ni mtoto anayejitambua, huku akipitia mchakato wa kujenga msingi wa maisha yake ya utu uzima.
Hivyo, ndivyo ilivyo kwa ACT Wazalendo, chama miongoni mwa vyama 19 vyenye usajili wa kudumu nchini, lakini chenyewe ndiyo kitinda mimba kati ya vyote.
Licha ya umri huo, kimekuwa kikinasibishwa na nafasi ya tatu kwa ukubwa upande wa Tanzania bara, huku kikiwa chama kikuu cha upinzani kwa upande wa Zanzibar.
Miaka 11 kwa mtazamo wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Revocatus Kabobe, ni umri wa kujenga msingi kwa ajili ya mafanikio ya baadaye.
Hata hivyo, anasema katika umri kilionao sasa ACT Wazalendo, kimefanikiwa kujipambanua kuwa chama cha siasa za hoja na sio mikikimikiki.
Anaeleza chama hicho kimejenga itikadi yake, sera na kuwa na misimamo inayotokana na hoja badala ya mihemko na maandamano.
“Wenyewe wamepoa hawana purukushani, wamejikita katika kujenga siasa za hoja. Leo hii ukiulizwa kuhusu ACT Wazalendo hivyo ndivyo utakavyowatambua,” anasema.
Katika kipindi hicho, anasema chama hicho kimepata ushawishi zaidi baada ya kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani Zanzibar.
“Hii imekipa nafasi kubwa na mafanikio hayo yametokana na kuanguka kwa CUF, kwa kuwa ACT Wazalendo imechukua nafasi ya CUF katika siasa za Zanzibar,” anasema.
Hata hivyo, anasema chama hicho pamoja na umri wake mdogo kinakumbwa na changamoto ya mazingira magumu ya kidemokrasia kwa sababu siasa za Tanzania hazijaimarika.
Katika miaka 11 hiyo, anasema chama hicho kimefanikiwa kujenga taasisi na kimethibitisha ukomavu kwa kuwa viongozi wake hawang’ang’anii madaraka.
“Wamefanikiwa zaidi kujenga taasisi, hawana hali ya kung’ang’ania madaraka, kila anayemaliza muda wake wa uongozi anaachia ngazi kupisha wengine,” anasema Dk Kabobe.
Anasisitiza, miaka 10 kisiasa ni michache, huwezi kujivunia mambo mengi, lakini ni umri wa kujenga msingi kwa ajili ya kushuhudia matunda zaidi baadaye.
“Bado ACT-Wazalendo wanahitaji muda kwa sababu hakijaleta ushindani upande wa Tanzania Bara na imefanikiwa upande wa Zanzibar, sasa bado nguvu zake ni ndogo kulinganisha na CCM na Chadema kwa upande wa Bara, kwa hiyo bado kina safari ndefu ya kujijenga," anasema.
Kwa upande wake, Mchanbuzi wa Masuala ya Siasa, Mwalimu Samson Sombi, anasema chama hicho kinapaswa kujiimarisha kwa wananchi kwa kutangaza sera zake.
"Bado sera zake hazijakubalika zaidi, kwa miaka 11 safari ndefu inahitajika kupata watu wengi zaidi ili kiwe na nguvu ya kuunda Serikali," anasema.
Maeneo 10
Ukiacha mitazamo hiyo, chama hicho kimetaja maeneo 10 kinayojivunia katika umri huo tangu kuanzishwa kwake, Mei 5, 2014.
Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 11 ya kuanzishwa kwa chama hicho, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu anasema wanajivunia kuongoza siasa za hoja dhidi ya siasa za vituko na uchawa.
"ACT-Wazalendo tumetangulia mbele kusemea changamoto za wananchi na kupendekeza majawabu yake kupitia sera zetu makini, pili tumejenga jukwaa mbadala kwa wanasiasa wote wanaopenda siasa safi na ambao hawaridhishwi na demokrasia kwenye vyama vyao," anasema.
Dorothy anasema kielelezo cha mafanikio hayo ni kupokelewa kwa Hayati Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake mwaka 2019.
Kingine anachotaja Dorothy, ni ACT Wazalendo kujenga jukwaa la kuaminika kwa vijana na wanawapa nafasi kuonyesha vipaji vyao vya uongozi, akidokeza vijana waamini chama hicho ndio jukwaa lao.
"Pia tumejenga jukwaa la ukombozi wa wanawake na tumevunja minyonyoro ya kukandamiza Demokrasia na tunaishi kwa vitendo, dhana ya usawa wa kijinsia kwa kuhakikisha kunakuwa na usawa kwenye vyombo vyote vya maamuzi," anasema.
Uwepo wa ulingano kwenye nafasi za uongozi katika nafasi za maamuzi ndani ya ACT Wazalendo, Dorothy anasema ni kielelezo ya mapinduzi makubwa ya kisiasa nchini.
Jambo lingine analotaja wanajivunia nalo, ni ujenzi wa jukwaa la Wazanzibari kujivunia nchi yao moja yenye mamlaka kamili, kwani ACT Wazalendo inakwenda kuongoza wakazi wa nchi hiyo kulikomboa Taifa lao.
Pia Dorothy anasema kwa miaka 11 tangu kuanzishwa kwa chama hicho wamejenga jukwaa la kupigania haki kwa wote kwa kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kuwakomboa Watanzania.
"Tumesimama na makundi yote kwenye jamii na ACT Wazalendo inatazamwa kama sauti ya matumaini, tumejenga chombo madhubuti cha kupigania haki ndani na nje ya nchi,” anasema.
"Pia tumeonyesha demokrasia kwa vitendo ndani ya chama na uamuzi wa chama chetu wa kuzingatia ukomo wa madaraka wa miaka 10 ni mfano wa kuigwa ambao umewashinda wengi kwenye vyama vya siasa," anasema.
Vilevile Dorothy anasema wamejenga chama kinachokua kwa kasi na chenye ushawishi ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Isihaka Mchinjita anasema vyama vya siasa vinaishi katika mazingira ambayo demokrasia inaminywa.
Anasema tangu awamu ya hayati Rais Ali Hassan Mwinyi hadi utawala wa awamu ya sita kumekuwa na ulaghai wa kuimarishwa demokrasia nchini bila mafanikio.
Aidha, Balozi Nchimbi alisema baadhi ya wanachama wanaotaka nafasi za uongozi wameanza kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha wanapitishwa bila kupingwa, jambo ambalo alisema halikubaliki ndani ya chama.
“Tumeanza kuona matukio ya baadhi ya wabunge na madiwani wakipitisha fomu ili watangazwe kuwa wagombea pekee. Wengine wanahamasisha vikao kutoa matamko kwamba wapitishwe bila kupingwa. Wapo wanaoandaa kumbukumbu za misiba, siku za kuzaliwa na hata sherehe za ndoa, lakini wahudhuriaji wanapewa posho na wamevaa sare za CCM ili ionekane kama mkutano wa kisiasa,” alisema.
Aliongeza kuwa CCM ina utaratibu wa kufuatilia mwenendo wa wanachama wake, na wale wote wanaoendesha kampeni za chinichini wataenguliwa mapema.