Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maswali tata ‘No Reforms, No Election’ ya Chadema

Muktasari:

  • Chadema inakusudia kuzuia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 endapo Serikali haitafanya mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi utakaowezesha kuwa na uchaguzi huru na wa haki, tofauti na chaguzi zilizopita.

Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiweka msimamo wa kuzuia uchaguzi mkuu ujao endapo mabadiliko wanayoyataka hayatafanyika, mchambuzi wa siasa na mwanaharakati wa maendeleo, Ansbert Ngurumo amehoji maswali manne kwa Chadema na wafuasi wao.

Ngurumo ambaye pia ni mwanahabari mkongwe, anahoji hatma ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini endapo kaulimbiu yake ya “No Reforms, No Election” (hakuna uchaguzi bila mabadiliko) haitafanikiwa.

Chadema kimepitisha kaulimbiu hiyo kwenye mkutano mkuu wa Januari 22, 2025 na mwenyekiti wake, Tundu Lissu amekuwa akisimamia utekelezaji wake kwa kusisitiza kwamba “kama mabadiliko hayatafanyika, watazuia uchaguzi kufanyika”.

Mabadiliko ya msingi wanayoyataka ni katika mfumo wa Tume ya Uchaguzi ambayo yatawezesha kuwa na uchaguzi huru na wa haki. Pia, wanataka mabadiliko hayo yahusishe mabadiliko ya Katiba, sheria na kanuni zake.

Katika hotuba yake ya kwanza kwa Taifa, Lissu alisema mtu akitaka waende kwenye uchaguzi, wamuulize “ili iweje?” kwa kuwa mazingira yaliyowezesha kuvurugwa kwa chaguzi za mwaka 2019, 2020 na 2024 bado ni yaleyale.

Akizungumzia msimamo wa Chadema wa “No Reforms, No Election”, Ngurumo ameibua maswali manne.

Anasema kwa mtazamo wa mwenyekiti, anaposema “ili iweje” hiyo ni kauli ya kususia uchaguzi. Anahoji, Chadema kikiamua kususia uchaguzi, vyama vingine vyote vitasusa?

“Mwenyekiti anasema watazuia uchaguzi iwapo mabadiliko hayatafanyika, kweli katika mazingira ya kisiasa ya Tanzania tunayoyafahamu, kweli Chadema ina uwezo wa kuzuia uchaguzi?

“Kama Chadema ina uwezo wa kuzuia uchaguzi, mimi nashauri Chadema ishiriki uchaguzi ili itumie nguvu hiyo hiyo ya kuzuia, ishinde. Yeyote mwenye uwezo wa kuzuia uchaguzi mkuu, ana uwezo wa kushiriki na kushinda,” amesema.

Swali la tatu, Ngurumo anahoji iwapo mabadiliko yakishindikana kufanyika na vyama vingine vikashiriki, wakati Chadema wakisema watazuia uchaguzi, je, ikitokea Chadema ikashindwa kuzuia uchaguzi wa Oktoba, hatma ya Chadema kama chama cha siasa itakuwaje?

“Hili ni swali ambalo linapaswa liwafikirishe wanasiasa, liwafikirishe viongozi wa Chadema, liwafikirishe washauri wa Chadema, liwafikirishe wahisani wa Chadema na yeyote ambaye anaona kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko kwanza ili uchaguzi ufanyike…

“…na vilevile yeyote anayekubaliana na kauli ya Chadema kwamba mabadiliko yakishindikana tuharibu, tuzuie uchaguzi. Je, Chadema ikishindwa kuzuia uchaguzi, hatma yake kama chama cha siasa itakaa wapi? Itakuwaje?” anahoji Ngurumo.

Swali jingine, anasema hayo yote yakishindikana na hatimaye uchaguzi ukaendelea, Chadema ikashindwa kuhudhuria, anahoji kwamba msimamo huo siyo uchochoro wa kuruhusu Chama cha Mapinduzi (CCM) kishinde kirahisi bila ushindani wa maana?

“Chadema kisiposhiriki, wengine wakashiriki, CCM kitashinda kirahisi na inawezekana katika kushinda kirahisi, wakalegeza hata mazingira magumu wanayotumia kwenye uchaguzi miaka yote, ikatengenezwa sura ya kuonesha uchaguzi ulikuwa huru na haki, watu hawakutekwa.

“Wewe ambaye hukushiriki, kwa hiyo hukushindwa, kwa hiyo kwa mujibu wa sheria, ukakosa uhalali wa kuhoji uchaguzi ambao hukushiriki, lakini vilevile kwa kuwa umeshindwa kuuzuia ukakuta umeshuka kutoka hadhi yako ya kuwa chama cha siasa, ukawa asasi ya kiraia ya kawaida isiyotafuta madaraka,” anasema mchambuzi huyo.

Anasema Chadema kinapaswa kukaa upya kufikiri upya, kutafakari upya, kujipanga upya, kwamba pamoja na ugumu ulio mbele yao, watu hao hawatakaa hata siku moja wawaonee huruma kwa sababu wamesema hawatashiriki uchaguzi.

“Chadema kitafute mikakati imara, mikakati mipya ya kushinda uchaguzi bila kusubiri huruma ya watawala,” anasema Ngurumo.


Wanazuoni watia neno

Akizungumzia msimamo huo wa Chadema, mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Paul Loisulie amesema ajenda yao ni nzuri lakini Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndiyo chenye dola, hakitakubali uchaguzi kuzuiwa.

Amesema ni rahisi CCM kuzima utekelezaji wa agenda hiyo huku akisisitiza suala la vyama vingine kushiriki uchaguzi unatoa uhalali wa uchaguzi wenyewe.

Dk Loisulie amesema japo wananchi wengi wanaunga mkono agenda ya Chadema, hofu yake ni kama wananchi hao wataamua kuivalia njuga ajenda hiyo ya kuzuia uchaguzi.

“Wananchi wanawaunga mkono Chadema lakini hatua waliyochukua ni ya juu sana, sidhani kama CCM ambayo ndiyo yenye dola watakubaliana nao,” amesema.

Amesema hata Chama cha Wananchi (CUF) waliwahi kuamsha vurumai Zanzibar lakini si kuzuia uchaguzi, kwa sababu hatua ya kuzuia ni uamuzi mkubwa zaidi.

Naye mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Richard Mbunda akizungumzia kaulimbiu ya Chadema, amesema kwa namna vyama vya siasa vilivyobanwa nchini, ni lazima kufanyika kitu.

Amesema kwa tathmini ya haraka, mtu hawezi kuona namna Chadema itazuia uchaguzi huo, lakini ili uchaguzi wowote duniani ufanyike lazima uwe halali na upate uungwaji mkono duniani.

“Hatuwezi kuponda kinachofanyika, kwanza itategemea Chadema italivalia njuga kiasi gani jambo hili ili kupata uungwaji mkono mkubwa,” amesema.

Amesisitiza kuwa hata madikteta duniani hutafuta uhalali wa kisiasa ili kupata uungwaji mkono, hivyo kinachofanywa na Chadema ni jambo muhimu.

Umuhimu wa agenda hiyo ni kuwasaidia kupata hitaji la kisiasa, kwa hali ilivyo sasa, wakiingia kwenye uchaguzi watapigwa mchana kweupe.