Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watano wafariki ajali ya basi la AN Classic

Muktasari:

  • Watu watano wamefariki dunia na wengine 49 kujeruhiwa baada ya basi la abiria linalofanya safari zake kati ya Dodoma na Kigoma la AN Classic.

Dodoma. Watu watano wamefariki dunia na wengine 49 kujeruhiwa baada ya basi la abiria linalofanya safari zake kati ya Dodoma na Kigoma la AN Classic kuligonga lori kwa nyuma na kuanguka katika eneo la Chigongwe jijini Dodoma.

Akizungumza leo Machi 4,2025 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishina Msaidizi Mwandamizi,  Anania  Amo amesema kuwa  ajali hiyo ilitokea Machi 3,2025 saa 4.00 usiku katika eneo hilo.

Amesema ajali hiyo ilitokea wakati basi  linalojulikana kama AN Classic  linalofanya safari zake kutoka Dodoma kupitia Tabora kuelekea Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma kuanguka wakati likitaka kulipita lori la mizigo.

“Lilianza safari kutoka Dodoma kwenda Kigoma na lilipofika maeneo ya Chigongwe wakati analiover take (anataka kulipita) lori moja la mizigo aliligonga mwishoni na hivyo kukosa mwelekeo na kuanguka,”amesema.

Amesema kati ya watu watano waliofariki wanaume watatu na wanawake wawili huku majeruhi wakiwa 49.

Kamanda Amo amesema katika majeruhi hao 26 ni wanaume na wanawake 23, ambapo 48 walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Dodoma huku mmoja akipelekwa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ajili ya matibabu zaidi.

Ikumbukwe Septemba 6, 2024, basi la AN Classic lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea mkoani Tabora lilipata ajali na kusababisha vifo vya watu 12, akiwamo mmiliki wa basi hilo, Amdun Nassor ambaye alikuwa dereva huku wengine zaidi ya 36 wakijeruhiwa.

Hata hivyo, Desemba 7, 2022 basi hilo lilipata ajali ambapo mtu mmoja alifariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa wakati likiwa safarini kutoka Tabora kwenda Mbeya na kupata ajali katika eneo la Makongorosi wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama wa Barabarani katika kipindi cha kati ya Julai hadi Septemba 2024, watu 453 walifariki dunia kutokana na ajali za barabarani.

Idadi hiyo ya vifo imepungua kutoka 477 vilivyotokea katika kipindi kama hicho mwaka 2023 huku waliojeruhiwa wakiwa ni 835, ikilinganishwa na 782 wa mwaka 2023.

Vyanzo vya ajali vikitajwa kuwa ni mwendo kasi, matumizi ya vilevi, miundombinu, kutozingatia sheria za usalama barabarani, matatizo ya kiufundi na uzembe wa madereva.