Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyebuni jina ‘Tanzania’ afariki dunia

Muktasari:

  • Mohammed Iqbal Dar alitunukiwa tuzo ya Sh200 pamoja na medali baada ya jina alilobuni kupendekezwa na kubaki kuwa sehemu ya historia ya Tanzania.

Dar es Salaam. Mohammed Iqbal Dar mbunifu wa jina la Tanzania, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80 jijini Birmingham, Uingereza, ambako aliishi tangu ahamie mwaka 1965.

Kifo chake kimetokea baada ya kuugua kwa muda wa miaka takriban 10, ambapo alikuwa hawezi kutembea akiwa chini ya uangalizi wa karibu nyumbani.

Mohammed Iqbal Dar alizaliwa Agosti 8, 1944, mkoani Tanga. Baba yake, Dk Tufail Ahmad Dar, alikuwa daktari mashuhuri aliyefanya kazi katika mikoa ya Tanga na Morogoro.

Aidha, alisoma katika Shule ya Aga Khan kwa elimu ya msingi na sekondari, kisha akaendelea na masomo katika Shule ya Sekondari Mzumbe mwaka 1964. Akiwa Mzumbe, aliona tangazo katika gazeti la The Standard likiwataka wananchi kupendekeza jina jipya la taifa jipya lililoundwa kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa bahati ya kipekee, pendekezo lake lilichaguliwa kuwa jina rasmi la nchi, na alitunukiwa tuzo ya Sh200 pamoja na medali, iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Habari wakati huo, Sheikh Idrisa Abdul Wakil.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Ahmadiyya Muslim Jamaat Tanzania kuhusu mahojiano yake aliyowahi kuyafanya hapo awali, Mohammed aliwahi kufafanua jinsi alivyobuni jina ‘Tanzania’. Alisema kuwa, kwa mwongozo wa Mungu, alichukua herufi tatu za kwanza za Tanganyika (TAN) na Zanzibar (ZAN), kisha akaongeza ‘I’ kutoka kwa jina lake Iqbal na imani yake katika Uislamu. Hatimaye, akakumbuka uhusiano wake na madhehebu ya Ahmadiyya na akaongeza ‘A’ ili kuheshimu madhehebu hayo, hivyo kuunda jina ‘Tanzania’.

Licha ya kuhamia Uingereza, Iqbal Dar aliendelea kuwa na uhusiano wa karibu na Tanzania. Alifanya ziara mara kwa mara nchini na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kibinadamu bila kujali tofauti za kidini. Pia alikuwa mshiriki wa mara kwa mara wa kongamano la Ahmadiyya Muslim Jalsa Salana, linalofanyika kila mwaka Tanzania.

Katika maisha yake yote, Mohammed Iqbal Dar aliendelea kuwa mzalendo na mwenye mapenzi ya dhati kwa Tanzania, huku jina alilobuni likibaki kuwa sehemu muhimu ya historia ya Tanzania.