Makalla: Chadema kutoshiriki uchaguzi ni mseleleko kwetu

Muktasari:
- Makalla amesema miaka ya nyuma mkoa wa Morogoro uliwahi kuonja sumu (kuchagua upinzani) na waliowaonjesha (Chadema) safari hii wamepumzika hawatashiriki uchaguzi, sasa ni mwendo ni mseleleko kwa CCM.
Morogoro. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema kitendo cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoshiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu ni mseleleko wa ushindi kwa chama hicho tawala nchini.
Makalla amebainisha hayo leo Alhamisi Mei 8, 2025 akiwa safarini kuelekea Ifakara, ambapo alisimama njiani kuzungumza na wakazi wa Ruaha wilayani Kilosa, akiwaomba wampe kura nyingi mgombea urais wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.
“Niseme nisisemeee, zamani tuliwahi kuonja sumu (kuchagua upinzani) na waliotuonjesha sumu safari hii wamepumzika, hawatashiriki uchaguzi, kina nani hao...Chadema...mwendo ni mseleleko, CCM oyeee...” amesema Makalla.

Aprili 12, 2025 Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhan Kailima alitangaza Chadema kutoshiriki uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu chaguzi nyingine ndogo zitakazofuata ndani ya miaka mitano, baada ya kutosaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.
Hata hivyo, Mwanasheria wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala aliwataka watendaji wa INEC wajitathimini kama wanaweza kutekeleza majukumu yao baada ya kueleza kuwa, Chadema hakitashiriki uchaguzi mkuu wa 2025 kutokana na kugomea kusaini kanuni za maadili.
Akizungumzia hoja ya Dk Nshala, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele alisema kilichozungumzwa na tume hiyo ni tafsiri yao, huku akisema kama Chadema wanatafsiri tofauti basi mtafsiri wa mwisho wa mambo hayo ni mahakama.
Akiwa kwenye ziara yake, Makalla ameeleza hayo akijenga hoja ya hali iliyokuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ambapo kwa mara ya kwanza Chadema kilishinda majimbo matatu ya Mikumi (Kilosa), Kilombero na Mlimba yaliyopo wilayani Kilombero.

Kutokana na hilo, Makalla amewataka wananchi wa Morogoro kujitokeza kwa wingi katika mchakato wa uboreshaji wa daftari la wapigakura, kwa kujiandikisha ili kupata fursa ya kushiriki katika uchaguzi mkuu ili kukipa ushindi CCM.
Makalla amewahakikishia wananchi wa Morogoro kuwa CCM itaendelea kuwa nao bega kwa bega katika kuisimamia Serikali ili kutatua changamoto zinazowakabili, akitolea mfano kukamilika kwa daraja la kisasa linalounganisha wilaya za Kilombero na Kilosa.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amesema wilaya hiyo imenufaika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi Sh100 bilioni.

Mbunge wa Mikumi, Dennis Londo ametoa shukurani Serikali kwa niaba ya wananchi wa Mikumi kwa kukamilisha ujenzi wa daraja la Kidatu - Ifakara, akisema ujenzi wa kiwanda cha sukari unaendelea ukikamilika utawezesha soko la uhakika kwa wakulima wa miwa wa Ruaha.
“Mwenezi wewe ni shahidi, changamoto kubwa ya siasa za hapa ni uhakika wa soko la miwa ambalo tuliwaahidi katika kampeni za mwaka 2020 kwamba tutakwenda kutatua.
“Najisikia fahari kwamba tunakwenda kukamilisha kiwanda hiki na kupata uhakika wa soko la miwa kwa wakulima wetu wa Bonde la Luembe,” amesema Londo ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.