Uhaba wa maji, Makalla awatoa hofu wakazi wa Manispaa ya Morogoro

Muktasari:
- Mkataba wa ujenzi wa mradi wa Sh185 bilioni unatarajiwa kusainiwa Julai mwaka huu ambapo yatajengwa matanki mawili la ujazo wa lita milioni 12 na lita tisa.
Morogoro. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema ujenzi mradi wa maji utakaosainiwa Julai 2025 kati ya Serikali na mkandarasi utakuwa suluhisho la kudumu la upatikanaji wa uhakika wa maji katika Manispaa ya Morogoro.

Makalla amesema ameelezwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kuwa mradi huo utakaogharimu Sh185 bilioni utakuwa mwarobaini wa tatizo la maji katika Manispaa ya Morogoro sambamba na kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo.
Makalla amesema hayo jana Jumanne Mei 6, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mwembesongo katika mwendelezo wa ziara yake ya siku saba mkoani Morogoro.
"Niwaondoe hofu wananchi wa Morogoro, Serikali imedhamiria kutatua tatizo la maji kwa kuleta mradi mkubwa, mimi kama msemaji wa chama nitafuatilia utekelezaji wake," amesema Makalla.

Hata hivyo, Makalla amesema katika mazungumzo yake na Aweso alielezwa Serikali imechukua hatua za haraka za kuchimba visima 17 na tayari vinne vimeshachimbwa maeneo ya pembezoni mwa manispaa hiyo ili kuboresha huduma.
"Mbunge wenu (Abdul Aziz Abood) amefuatilia na waziri amemhakikishia kulifanyia kazi suala hili, Aweso ameniambia wataboresha chanzo cha maji Mafiga ili kuwapo uhakika wa huduma ya maji maeneo yenye mgao," amesema Makalla.
Makalla amempongeza Abood kwa kusema ukweli, kwamba licha ya mafanikio yaliyopatikana lakini ameeleza changamoto zinazoikabili jimbo hilo ambayo ni upatikanaji wa maji safi katika manispaa ya Morogoro.
"Nimezipokea changamoto alizozisema mbunge wenu, kwanza suala la maji naelewa tatizo hili, mimi ni mkazi Morogoro na nilishawahi kuwa naibu waziri wa maji najua suala hili," amesema.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo, Mbunge wa Morogoro Mjini (CCM), Abood amesema mradi maji huo utakuwa na matenki mawili yenye ujazo wa lita milioni 12 na lita milioni utapunguza kero ya upatikanaji wa maji katika manispaa hiyo.
"Naomba msisitizo katika mradi huo ambao ni wa muda mrefu, lakini tunaambiwa bado kusainiwa tunakuomba mwenezi ulipokee hili na ukasisitize huko," amesema Abood.

Mbunge wa viti maalumu wa mkoa wa Morogoro, Dk Christina Ishengoma amesema Serikali ya awamu ya sita imejitahidi kuboresha huduma za afya na miundombinu, lakini ujenzi wa bwawa la Mindu ukikamilika wataondoka na changamoto ya maji.