Lissu: Narejea kushiriki maandamano

Muktasari:
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ambaye kwa sasa yupo nchini Ivory Coast kuiunga mkono timu ya Taifa Stars inayoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), amesema analazimika kurejea nchini ili kushiriki maandamano hayo.
Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku nne kufikia siku iliyotangazwa kufanyika maandamano ya Chadema, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Bara, Tundu Lissu amewataka wananchi wote kuungana nao katika maandamano hayo ili kuwa sehemu ya mabadiliko wanayotafuta.
Januari 13, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza kufanyika kwa maandamano ya amani kuanzia jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kupinga miswada ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa na muswada wa Sheria ya Uchaguzi.
Badala yake, Mbowe alisema wanataka Serikali ipeleke bungeni muswada wa mabadiliko ya Katiba.
Alipotafutwa leo Januari 20, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema wamepokea barua ya Chadema ikiwataarifu kuhusu maandamano hayo, lakini kuhusu kibali ametaka atafutwe Januari 22.
“Tarehe 24 bado mbali, sasa hivi tunashughulika na athari zilizosababishwa na mvua, hata hivyo Jeshi la Polisi kazi yetu ni kulinda wananchi na mali zao hivyo, nitafute tarehe 22 nitakupa taarifa kwa sasa kuna mambo mengi makubwa ya kushughulikia yanayowahusu wananchi,” amesema Muliro.
Akizungumza leo kupitia video katika mtandao wa Youtube, Lissu ambaye kwa sasa yupo nchini Ivory Coast alikoenda kuiunga mkono timu ya Taifa Stars inayoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), amesema analazimika kurejea nchini ili kushiriki maandamano hayo kwa sababu yanakwenda kutengeneza historia.
“Pamoja na umuhimu wa kuiunga mkono timu ya Taifa katika mashindano makubwa inayotuwakilisha barani Afrika, mustakabali wa baadaye wa nchi yetu ni muhimu zaidi.
“Mashindano ya Afcon yataendelea kuwepo nchi yetu inaweza kuingizwa kwenye maafa makubwa ya kisiasa endapo utawala utaendelea kukaa madarakani kwa misingi ya sasa ya kikatiba, kisheria na kiutawala hivyo basi mimi nitakuwepo Dar na nitashiriki maandamano ya amani ya Januari 24.
“Hili haliwezi kuwa jukumu langu peke yangu au la Mwenyekiti Mbowe peke yake au la wana-Chadema peke yao kwa sababu katiba mpya na mfumo bora wa uchaguzi vinatuhusu sisi wote naomba kila mmoja wetu ajitafakari na atafakari nafasi yake katika mapambano haya na katika ustawi wa Taifa letu wote,”amesema.
Amesema kwa muda mrefu jitihada zimefanyika za kuishauri CCM na Serikali zake kuifanyia mabadiliko katiba na mifumo ya uchaguzi, lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu hivyo nguvu ya umma inapaswa kutumika katika kushinikiza hilo.
“CCM na Serikali zake haitakubali mabadiliko yoyote bila kulazimishwa kwa nguvu ya umma wa wananchi wote wenye nia njema na nchi yao. Kwa sababu hiyo, wote tunaotaka mabadiliko chanya katika maisha yetu, tunaotaka mfumo bora wa utawala unaojali mahitaji na maslahi ya wananchi walio wengi badala ya kikundi kidogo cha watawala na familia zao.
“Wote tunaotaka mfumo bora wa uchaguzi utakaotupatia viongozi halali wa kuchaguliwa, wanaojali shida za wananchi, wenye uchungu na rasilimali za taifa letu na wanaowajibika kwetu, hatuna budi kuungana ili kumdai Rais Samia na CCM yake wabadili msimamo wao kuhusu Katiba mpya na mfumo mpya ulio huru wa uchaguzi,” amesema Lissu.