Lissu: Hatuogopi uchaguzi, tunataka mabadiliko ya mfumo

Iringa. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Tundu Lissu, amesema wanaodai chama hicho kinaogopa uchaguzi mkuu si kweli, bali wanachohitaji ni mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi huo.
Kauli hiyo ya Lissu inaelekea kumjibu Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, aliyoitoa hivi karibuni jijini Mbeya wakati wa mkutano wake, akieleza kuwa Chadema wanaogopa uchaguzi ndio sababu wamekuja na kampeni yao ya ‘No Reforms No Election’.
Akizungumza leo Jumapili, Machi 30, 2025, katika mkutano uliofanyika Mwembetogwa mkoani Iringa, Lissu amesema wanaodai chama hicho kinaogopa uchaguzi si sahihi, bali wanahitaji mabadiliko ya mfumo kwenye uchaguzi.
Amesema hali ilipofikia sasa, upigaji wa kura unaonekana kutokuwa na maana tena na hata kura yenyewe haina thamani kwa sababu uhuru wa kuamua nani awe kiongozi haupo.
“Kupiga kura hakuna maana tena, kura haina thamani yoyote kuamua mwenyekiti, diwani, mbunge au Rais,” amesema Lissu.

Amesema katika hali ya kushtua, miaka 10 iliyopita, kwenye uchaguzi wa 2014 Iringa mjini, kati ya mitaa 126, wenyeviti 54 sawa na asilimia 43 walishinda kupitia Chadema, lakini mwaka jana kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, chama hicho kiliambulia patupu.
“Katika uchaguzi wa 2015, Iringa mjini, katika kata 18, madiwani 14 walioshinda ni wa Chadema, sawa na asilimia 78, mbunge aliyeshinda ni wa Chadema, lakini kwa sasa hatuna kitu. Tujiulize hizi sifuli zimetokana na nini?”
“Mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi na vyombo vya uchaguzi vyote ni vya CCM, sheria na Katiba kuhusu uchaguzi ni za CCM, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi haina uhuru, waliopo wote ni wateule wa Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM,” amesema Lissu.
Hivyo, amesema lazima ifike hatua kura za wananchi ziheshimiwe, huku akisema kwa miaka 10 iliyopita, Chadema ilishinda vijiji 1,754, lakini mwaka jana waliishia vijiji 97, huku wabunge 75 na sasa ni mmoja.
“Tumechoka kudhulumiwa kwa kweli, tupiganie mabadiliko, tusisimamiwe uchaguzi na mfumo huu. Tumepiga kelele muda mrefu kuhusu mfumo huu, hakuna kinachobadilika. Mfumo uliopo kwa sasa ni wa CCM,” amedai Lissu.
Awali, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa, amesema CCM inang’ang’ania uchaguzi usio wa haki, akibainisha kuwa hali hiyo haina afya kwa maendeleo ya Taifa.
“Wizi wa kura si jambo jema, sawa na rushwa. Hata katika dini, wizi siyo mzuri, hivyo lazima mjue kwamba CCM inachofanya haiwatendei haki wananchi wake na Taifa kwa ujumla,” amedai Dk Slaa.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, amesema iwapo wananchi watakikabidhi chama hicho madaraka, maisha ya kubeti yataisha, badala yake vijana watapata kazi migodini.
Amesema inashangaza kuona nchi inashindwa kutumia rasilimali zake, zikiwamo nyanya zinazolimwa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kutengeneza ‘Tomato Sosi’, badala yake inaagizwa kutoka nje.
“Blanketi zinatoka nje, badala ya kutumia zao la pamba tulilonalo. Tunahitaji kuongoza nchi hii, tutengeneze ajira za kudumu kwa vijana. Walimu hawana mishahara, wanajikita kubeti. Chadema itaboresha eneo hili na kukomesha mikopo kausha damu,” amesema Heche.
Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, amesema katika operesheni ya ‘No Reforms No Election’, wamegundua wananchi wana kiu kubwa ya maendeleo na mabadiliko.
Amesema lengo la ziara ya chama hicho ni kuwaunganisha wananchi wote ili kufikia maendeleo ya kila mmoja kwa nafasi yake, badala ya kuishi katika mazingira magumu.
“Walimu wamekuwa wakiisaidia Serikali katika suala la elimu. Ifike mahali tuyatafute maendeleo na si kupoteza haki zetu. Watumishi wote, wafanyabiashara wanaumizwa sana na uongozi wa CCM,” amesema Sugu.