Lissu alia mfumo wa uchaguzi kukibeba CCM

Muktasari:
- Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu anaendelea na ziara yake katika mikoa mbalimbali ambapo anazungumza na Watanzania kuhusu msimamo wa chama chake kutaka kuzuia uchaguzi ujao kama hakutakuwa na mabadiliko kwenye mfumo wa uchaguzi.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema kukosekana kwa mfumo huru wa uchaguzi kumekuwa fursa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupita bila kupingwa, hivyo hawapo tayari kuona jambo hilo likiendelea.
Lissu amebainisha kwamba hata kampeni za uchaguzi zimekuwa zikitumika kuwasumbua wagombea wa vyama vya upinzani, hasa wagombea wa Chadema kwa kuwekwa mahabusu bila sababu na baadaye kuachiwa.
Mwenyekiti huyo amebainisha hayo leo Machi 28, 2025 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Vwawa mkoani Songwe ambapo amefafanua sababu za chama hicho na Watanzania kutaka kuzuia uchaguzi ujao kupitia kaulimbiu yao ya “No reforms, No election” kama hakutakuwa na mabadiliko.
“Uchaguzi kwenye kampeni ni kuwasumbua wagombea wa upinzani, ukiwa mgombea wa urais, Polisi wanakusumbua, mwaka 2020 nilipigwa mabomu mara tatu,” amesema Lissu na kuongeza:
“Nimezuiwa kufanya kampeni siku 10, wanakuzuia tu huendi kwa sababu wao hawafanyi kampeni na wewe wanakuzuia, kila mahali wagombea wetu walizuiwa kufanya kampeni.”
Siyo kwenye kampeni pekee, Lissu amesema hata uapishaji wa mawakala, kupata nakala ya matokeo ni vita, hivyo wao hawahitaji tena vita kwenye masuala yanayoruhusiwa kisheria kama uchaguzi.
Lissu amesema mfumo wa uchaguzi unadhibitiwa na Rais kuanzia juu hadi chini na Rais mwenyewe ni Mwenyekiti wa CCM, hivyo lazima akipendelee chama chake.
Akijenga hoja yake kuhusu chama hicho kuzuia uchaguzi, Lissu amesema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ipo mikononi mwa kiongozi mkuu wa nchi na ndiye anateua watendaji wake wote.
“Mwenyekiti wa Tume ni mtu wa Rais, makamu wake, wajumbe wake, ni watu wa Rais, Mkurugenzi wa Uchaguzi, wakurugenzi wa halmashauri wanaosimamia uchaguzi, wasimamizi wa chini, wote ni watu wa Rais wote,” amesema.
Kutokana na mfumo huo wa usimamizi wa uchaguzi, Lissu amesema kuanzia mwaka 2015 haukuwahi kufanyika uchaguzi wa haki kwani wagombea wao walienguliwa wote tofauti na miaka ya nyuma ambapo wagombea wachache ndio walioenguliwa.
Akikumbuka uchaguzi wa mwaka 2010, amesema matumizi ya nguvu yaliyopo sasa ni tofauti na miaka ya nyuma ambapo askari wanaonekana kuanzia kwenye kampeni za uchaguzi ambazo hufika na vifaru na mabomu.
Mtindo huo ndio Lissu amesema umekilazimu chama chake kutangaza kusitisha uchaguzi huo usifanyike hadi pale wananchi watakapopewa haki ya kuwachagua viongozi wanaowataka na si kuchaguliwa kwa mabavu.
Awali, Makamu Mwenyekiti Chadema Kanda ya Nyasa, Frank Mwakajoka amesema Jeshi la Polisi pamoja na CCM wanapaswa kutambua kwamba hakuna haki kuu duniani kama haki ya kuishi na ile ya kupata kiongozi mwenye uwezo wa kuongoza.
“Haki ya kuishi ni lazima na haki ya kumchagua kiongozi unayemtaka ni lazima lakini Serikali ya CCM imeamua kupoka haki hii, haki mliyonayo wananchi ni kupiga kura.
Mwakajoka amesema ni lazima yawepo mabadiliko ya uchaguzi mwaka huu, huku akidokeza jukumu la kuzuia uchaguzi litatekelezwa na CCM na Jeshi la Polisi.
Amesema kwa kuwa haki haiombwi, watailazimisha ipatikane kwa nguvu huku akitoa wito kwa viongozi wa chama hicho wanaotaka kugombea wajiandae baadaye kama mifumo ya uchaguzi itabadilishwa.
“Haiwezekani watoto wetu wanakufa kwa sababu Mwakajoka anataka kwenda bungeni au Ikulu, ni jambo ambalo haliwezekani. Tunahitaji haki, tunahitaji uchaguzi huru kupata viongozi bora watakaoijenga Tanzania.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi amesema mabomu na silaha zote zinazotumika kudhibiti uchaguzi ni kodi za wananchi na zingepaswa kuelekezwa kununua dawa kuhudumia wananchi hospitalini.
“Mimi ni mwathirika wa mazingira magumu ya uchaguzi, ndiyo maana pamoja na kukomaa na kuwa mbunge kwa miaka 10, sipo tayari kurudi kwenye uchaguzi kwenye mazingira niliyopitia mwaka 2010. Nikigombea Mbeya Mjini, nilipata kura nyingi lakini hadi kutangazwa ilibidi mabomu yapigwe, tuchome matairi, tuweke mawe barabarani,” amesema.