Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema yakoleza moto wa ‘No reform No election’

Muktasari:

  • Sugu asema haiwezekani kupata viongozi kwa gharama ya watu kuuawa au kupigwa mabomu. Alisisitiza kuwa uchaguzi lazima uwe na mifumo bora na tume huru.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amesisitiza kuwa hakutafanyika uchaguzi mkuu mwaka huu kama hakutakuwa na mifumo huru ya uchaguzi ambayo haitakipendelea Chama cha Mapinduzi (CCM) au chama chochote kingine.

Amesema hawatakuwa tayari kushuhudia uchaguzi ambapo ili wagombea wa upinzani walioshinda watangazwe, lazima vurugu zitokee au watu wapoteze maisha, huku akisisitiza kuwa uwanja huru wa kushiriki uchaguzi ni msingi wa hoja yao ya "No Reforms, No Election".

Lissu ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Machi 27, 2025, mkoani Songwe alipozungumza na wananchi kuhusu dhamira ya chama hicho kuzuia uchaguzi, ikiwa hakutakuwa na mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi.

“Hatutaki mfumo unaoipendelea Chadema wala CCM, tunataka mifumo inayosaidia hata askari wetu. Tukiwa na mifumo mibovu ya uchaguzi, wanaolipa gharama ni pamoja na hawa polisi,” amesema Lissu.

Kiongozi huyo wa Chadema amesema hawataki tena uchaguzi unaosimamiwa na ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) au Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuwa wote wapo kwenye mifumo ya CCM.

Lissu aliwambia wananchi wa Tunduma na Watanzania kwa ujumla kuwa kama CCM hawataki kuridhia mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi, basi uchaguzi hautafanyika.

Lissu alielezea ushindi wa Chadema katika jimbo la Momba na Tunduma katika uchaguzi mkuu 2010 na hata uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2014, ambapo Chadema ilishinda katika mitaa 56 kati ya 71.

“Mwaka 2015 wakagawanya majimbo, lakini tukasomba yote Tunduma na Momba kwenye udiwani kati ya kata 15, tulipata kata 14,” amesema.

Kutokana na takwimu hizo, Lissu amesema CCM hawataki mabadiliko kwenye mfumo wa uchaguzi kwa kuwa wana hofu ya kushindwa.

“Baada ya uchaguzi wa mwaka jana wa Serikali za mitaa, kamati kuu ikakaa kujadili jinsi ya kuendelea, tukasema kuanzia sasa jukumu letu ni kupigania mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi, na kama CCM watakataa, tutakinukisha,” alisema.

“Huko tunakokwenda ni kugumu sana; hii kauli ya 'kama hakutakuwa na mabadiliko, hakutakuwa na uchaguzi', nani amewahi kuisema? Ni kauli rahisi, kauli gani? Watu wanasema Chadema wanaogopa uchaguzi, sisi tuliotawala Tunduma na Halmashauri ikawa yetu, ni watu wa wapi?” amehoji.


Kuhusu hofu ya chama hicho kufa, Lissu amesema chama cha UDP ndicho kilichoshiriki uchaguzi tangu mwaka 1995 na kilikuwa na wabunge wengi kuliko Chadema, lakini kwa sasa ni kama hakipo.

Amesema wanaosema Chadema kitakufa kisiposhiriki uchaguzi wanaandika kupitia mitandao ya kijamii bila kufahamu akidi ya watu iliyopo ndani ya chama hicho, akisisitiza kuwa watakapozuia uchaguzi, dunia itatambua kinachoendelea nchini..


Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Kanda ya Nyasa, Tabia Mwakikuti, amewahimiza wanawake kushikamana kuhakikisha msimamo wa Chadema unatekelezeka, hasa kutoruhusu uchaguzi kufanyika kama hakuna mabadiliko.

Naye Makamu Mwenyekiti Chadema Kanda ya Nyasa, Frank Mwakajoka, amesema chama hicho kinakwenda kushinda uchaguzi kwa mifumo bora, na dhamira yao ni kuwaletea maendeleo wananchi.

“Kwa anayetaka kugombea lazima amwambie Rais abadilishe sheria za uchaguzi, na kama hakuna hayo, uchaguzi hautafanyika. Hatutakubali kuendelea kuzika watu wetu kwa sababu ya uchaguzi usio halali. Mwaka huu kama hakuna mabadiliko, hakutakuwa na uchaguzi,” amesema.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi “Sugu”, ambaye amesema CCM haiwezi kuondoka madarakani kwa mfumo uliopo, hivyo wanataka mifumo huru inayosaidia wananchi kumpata kiongozi wanayemtaka.

“Haiwezekani kupata viongozi wa kuwaongoza wananchi halafu wengine wauawe au kupigwa mabomu na jeshi la polisi.

“Mimi sioni raha yeyote kwamba ili niwe mbunge, watu wauawe. Tuchome matairi sasa ili kumaliza haya, lakini tupate mifumo bora ya uchaguzi. Tupo hapa kuhamasisha wananchi tupate tume huru ya uchaguzi,” amesema.

Sugu alitolea mfano mwaka 2015 alishinda ubunge, lakini ili atangazwe, wananchi walilazimika kufanya fujo na wengine kutangazwa.

Amesema faida ya wananchi kuwa na viongozi waliowachagua ni kwenda kuwajibika kwa wananchi, na shida iliyopo sasa ni wananchi kuchagua viongozi.